UMAARUFU NA AFYA YA AKILI

 

NA GEOFREY DISMAS

Tatizo la akili si tatizo dogo hasa kwa watu maarufu wakiwemo waigizaji, wanamichezo na wanamuziki. Kila aliyefanikiwa katika tasnia hizo, aliwahi kupitia changamoto ya tatizo la akili na wengine walishindwa vita hiyo wakapoteza na wengine hawakupoteza, walishinda. Wapo waliotoka hadharani na kuelezea namna walivyokutana na changamoto hiyo lakini wapo ambao hadi leo hawakuwahi kujitokeza hadharani na wengine walipoteza maisha kwa kutumia dawa za kulevya na wengine walijiua kwakukosa msaada.

Kila mtu maarufu na mwenye mafanikio aliwahi kupitia changamoto hii ya tatizo la akili wafuatao ni baadhi ya wasanii na wanamichezo waliowahi kupitia changamoto hii;

Amanda Byenes

AMANDA BYENES

Muigizaji Amanda Bynes, Mnamo mwaka wa 2014, nyota huyo wa Easy A aliwekwa kwenye kituo maaluu cha kutibu watu wenye matatizo ya akili ambapo huko alikaa kwa takribani miaka 9 akitibiwa baada ya kugunduliwa na ugonjwa unaotambulika kama Bipolar Affective Disorder and Manic Depression kwa tafsiri isiyo rasmi tunaweza kuuita ugonjwa wa hisia na unyogovu wa kihemko. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Bynes kukutwa mitaa ya jiji la LA akiwa uchi. Mnamo Machi 2022, Bynes aliachiliwa kutoka kwenye kituo hicho ambako alikaa kwa miaka 9 chini ya uangalizi wa wataalamu na wazazi wake.

Ryan Reynolds

RYAN REYNOLDS

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 45 amekabiliana na tatizo la kuwa na wasiwasi mkubwa tangu akiwa mtoto, Reynolds alisema kwenye kituo cha TV kiitwacho CBS.

"Nimekuwa na tatizo la kuwa na wasiwasi maisha yangu yote kwa kweli. Na unajua, ninahisi kama nina sehemu mbili za maisha yangu, ambayo moja inachukua nafasi hiyo inapotokea," Reynolds alisema.

Reynold anaongeza kwa kusema watu wanavyomtazama kwenye TV ni tofauti na maisha yake akiwa nje ya TV.

Britney Spears

BRITNEY SPEARS

Mwanamuziki maarufu kutoka nchini marekani Britney Spears aliwahi kukiri waziwazi kuhusu tatizo lake la akili kupitia mtandao wake wa kijamii. Tatizo lake la akili linatokana na wale waliowahi kumuumiza katika maisha yake na hata mitandao ya kijamii. Watu wa karibu na mwanamuziki huyu waliwahi kukaririwa wakisema Spears anaonekana kukata tamaa kabisa. Katika mtandao  wa kijamii wa Instagram kupitia akaunti yake aliwahi kusema kuwa maisha ya mastaa kwenye mitandao ya kijamii siyo maisha halisi.

Aaron Carter

AARON CARTER

Mwimbaji Aaron Carter ambaye sasa ni marehemu, alifichua kuwa anapambana na matatizo mengi ya afya ya akili, multiple personality disorder, schizophrenia, acute anxiety na manic depression katika kipindi cha The Doctors. Carter ambaye wakati huo alikuwa na miaka 31, alijulikana sana kama nyota wa muziki wa pop tangu akiwa mdogo, katika kipindi hicho aliorodhesha takribani dawa sita ambazo anatibiwa nazo.

"Huu ndio ukweli wangu," Carter alisema huku akiinua mfuko wa plastiki wa chupa nyingi za dawa kwenye klipu moja iliyotrend sana wakati huo katika mtandao wa facebook.

Carter pia aliwahi mpeleka mama yake mzazi Jane, kwenye onyesho, na kuwaomba waandaaji waandaaji Dr. Travis Stork na Dk. Judy Ho wamsaidie mama yake aachane na matumizi ya pombe ya kupindukia kwani alikuwa anahofu kuwa mama yake anaweza kujikuta katika hali mbaya Zaidi.

Carter alifariki novemba 25 mwaka jana akiwa na miaka 34. Mwili wake ulikutwa bafuni na msaidizi wake wa nyumbani huko Lancaster, California nchini marekani huku chanzo cha kifo kikitajwa ni kuzidisha dawa za kulevya.


Howie Mandel

HOWIE MANDEL

Howie Mandel kwa muda mrefu amekuwa wazi kuhusu matatizo ya kiafya ambayo ameshughulika nayo kwa miaka mingi - linapokuja suala la maradhi ya mwili na shida za afya ya akili Mandel amekuwa mstari wa mbele kabisa kupambana.

Jaji huyu maarufu kutoka katika shindano maarufu la America's Got Talent, ambaye anapambana  kwa muda mrefu na matatizo ya akili na msongo wa mawazo kama vile Obsessive Compulsive Disorder (OCD) na Attention Deficient Hyperactivity Disorder (ADHD) ni wakili mzuri wa kukomesha unyanyapaa unaowakabili wagonjwa wa matatizo haya ya akili.

"Tunatunza afya yetu ya meno, hatujali afya yetu ya akili." Alimwambia Jay Leno mwaka wa 2014

Alidai kuwa unyanyapaa na ukimya kuhusu afya ya akili unatokana na ukosefu wa elimu katika jamii ya wamarekani.

"Tuko nyuma sana ulimwenguni kiasi cha kutokuwa na shule mahali ambacho inafundisha kila mtu jinsi ya kutambua na kuikubali hali hii,"aliongeza. "Nadhani suluhisho la kufanya ulimwengu huu kuwa bora ni ikiwa tungekuwa na afya njema, kiakili." Alimalizia.

Naomi Osaka

NAOMI OSAKA

Jina hili siyo geni kwa wapenzi wa tenesi duniani. Nyota huyu wa mchezo wa tenesi tayari ameonja tamu na chungu ya kuwa maarufu.

Osaka aligeuka kuwa nyota akiwa na miaka 15 tu. Osaka katika maisha yake ya kuwa mcheza tenesi nyota amekwisha nyakua mataji manne ya Grand Slam na kuorodheshwa kama mchezaji namba moja bora wa tenisi na Chama cha Tenisi cha Wanawake duniani. Mnamo 2020, alishinda tuzo ya Associated Press kama Mwanariadha bora wa Kike wa Mwaka.

Lakini nyota huyo wa Marekani mwenye asili ya Kijapani ambaye sasa ana miaka 25, amekuwa akikabiliana na wasiwasi na mfadhaiko kwa muda mrefu. Masuala haya ya afya ya akili yameathiri uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake ya kikazi, kama vile kushiriki katika mikutano ya wanahabari na vyombo vya habari. Wakati Osaka anafanya maamuzi ya kujiondoa kwa hiyari kwenye mashindano ya French Open ya mwaka 2021 ili kuipa kipaumbele afya yake ya akili, alipokea upinzani kutoka kwa vyombo vya habari hasa pale alipokwepa kufanya mazungumzo na wanahabari.

"Kunaweza kuwa na wakati kwa yeyote kati yetu ambapo tunashughulikia masuala fulani nyuma ya pazia," Osaka aliandika kwenye TIMEs. "Kila mmoja wetu kama wanadamu anapitia kitu kwa kiwango fulani." Aliongeza.

Osaka alikuwa anasumbuliwa na matatizo ya afya ya akili tangu mwaka 2018 katika mashindano ya US Open. Alipigwa faini ya Dola 15,000 za marekani kwa kukwepa mkutano na wanahabari.


Serena Williams

SERENA WILLIAMS

Hakuna asiyemfahamu nyota huyu na legendary katika mchezo wa tenesi na mwanaharakati wa masuala mbalimbali. Kuhusu suala la afya ya akili yeye anasema huwa anaweka mipaka mikari au madhubuti hasa linapokuja suala kama hilo la afya ya akili. Serena alisema hayo akiwa katika video call na Popstar na muigizaji kutoka katika kiwanda cha filamu cha Hollywood.

Serena alisema yeye hupanga muda wa kujifanyia tathmini ya afya ya akili ili asije kufikia katika hali mbaya. Serena amenyakuwa Grand Slam 23 katika wakati wote ambao amekuwa active katika mchezo wa tenesi.

Michael Phelps

MICHAEL PHELPS

Kila siku Michael Phelps hufanya mazoezi katika gym iliyopo nyumbani kwake kuweka mwili wake sawa lakini huwa hasahau kamwe kushughulikia afya yake ya akili kila siku. Phelps ni mshindi wa Olympic wa mchezo wa kuogelea wa Marekani wa muda wote

“Katika kipindi chote cha kucheza mchezo huu, nimekuwa nikizungukwa na timu ya watu ambao kazi yao nikuhakikisha nakuwa bora kimwili. Kama nahitaji kuwa imara, kuna kuwa na watu 10 ambao kazi yao ni kutafuta njia za kunifanya nakuwa imara sana. Lakini linapokuja suala la akili, hakuna mtu hata mmoja” Phelps aliuambia mtanao wa Healthline.

Baada ya kuishi na msongo wa mawazo, hofu, na mawazo ya kujiua kwa miaka kadhaa, aliamua kuweka kipaumbele katika afya ya mwili na akili yake.

Mwaka 2004, baada ya kushinda medali 6 za dhahabu na 2 za shaba katika mashindano ya Athens Olympics, Phelps anasema alianza kuhisi msongo wa mawazo wa baada ya ushindi (post-Olympic depression)

“Unajibidiisha kwa miaka 4 ili kufikia katika hatua hiyo, halafu unafika katika hatua hiyo uliyoitamani sana…Juu kabisa ya kilele cha mlima, halafu unajiuliza sasa natakiwa kufanya nini baada ya hapa? Natakiwa kwenda wapi? Mimi ni nani?” Alisema.

Aliamua kuchukua mapumziko mafupi, lakini akarudi tena katika mazoezi muda mfupi mwaka 2004 baada ya mashindano ya Olympics kutamatika, akaenda kushindana kwenye Olympic ya mwaka 2008 na 2012.

Phelps aliendelea kutaabika na kujitenga na wenzake, kujifungia chumbani kwa muda mrefu “Kisha nikaamua ni muda sasa wa kuchukua hatua kutafuta mkondo mwingine, njia tofauti” alisema.

Mwaka 2014, baada ya kukubali kuwa anahitaji msaada,Phelps aliamua kwenda katika kituo cha kusaidia watu wenye uhitaji wa matatizo ya akili ambako huko alikaa kwa siku 45 akipatiwa matibabu.

“Mara baada ya kutoka nje, niliendelea na matibabu (therapy) ambayo niliyapata kwenye kile kituo nilichokuwa natibiwa. Kwangu mimi, unajua, wakati naanza niliona ni kitu cha kutisha, kitu cha kuogofya, kitu ambacho ni kipya na sikujua namna ya kukipokea, na nadhani hapo nipo udhaifu wangu ulipojitokeza kwa mara ya kwanza.” Alisema Phelps.

Phelps anasema baada ya kutoka katika kituo alichokuwa anapatiwa matibabu alijihisi amepona kabisa tatizo la afya ya akili na kwamba yuko tayari kwa kazi. Anaendelea kwa kusema alianza kujitambua yeye ni nani na mwenye jukumu gani na si tu ni binadamu bali pia ni mwogeleaji ambayo ndiyo kazi yake.

Chloe Kim

CHLOE KIM

Mapema mwaka jana wa 2022, binti wa miaka 22, mmoja wa washindi wa Olympic katika mchezo wa kuteleza kwenye barafu na mshindi wa medali ya dhahabu, Chloe Kim alitangaza kuwa atakaa nje ya michezo kujipa mapumziko ili ajikite katika kushughulikia afya yake ya akili. Katika mkutano wa 2022 wa Teen Vogue Summit uliofanyika huko Los Angeles, alifunguka kuhusu uamuzi wake huo.

“Nimetambua katika Olympics yangu ya kwanza yam waka 2016, nilichukia mchezo wa kuteleza kwenye barafu,” alisema na kuongeza, “Sikuhitaji kufanya tena kabisa, na sikuwa mawazo ya kurudi kabisa huko…Niliamua kwenda shule kwa muda, na niliona ni kwa namna gani ilivyo na manufaa sana kwangu. Hivyo baada ya kurudi kutoka Beijing kwenye Olympics yangu ya pili, niliona ninahitaji kupumzika kidogo kwa sababu nilipoteza kabisa yale mapenzi yangu na mchezo huo.”

Chloe aliunga mkono hoja ya mshindi wa medali ya dhahabu katika Olympic, Simone Biles ambaye alisema kuweka kipaombele katika afya ya akili kwa mwanamichezo ni jambo la lazima.  Katika maelezo yake Chloe anasema sababu nyingine iliyompelekea katika hali hiyo, ni kutokana na kukosa uhuru wa kufanya baadhi ya vitu mara baada ya kuwa maarufu. Anasema mara baada ya kushinda medali ya dhahabu hakuweza kwenda katika migahawa aliyozoea kwenda, hakuweza kwenda katika sehemu alizozoea kwenda. Hali hiyo imfanya achukie medali ya dhahabu aliyo shinda na aliichukua pamoja na vifaa vyake vya kutelezea kwenye barafu akavitupa kwenye chombo cha takataka.

Kwa kuhitimisha, Kwa mujibu wa shirika la afya duniani kwenye ripoti yao yam waka 2019, walieleza kuwa mtu 1 kati ya watu 8, au watu milioni 970 duniani kote wanasumbuliwa na matatizo ya akili ikiwemo woga mkubwa au anxiety na unyongovu au depressive disorders.

Afya ya akili haiwaathiri tu watu maarufu japo kuwa wao wapo kwenye hatari zaidi lakini kila mtu anaweza kukumbwa na ugonywa huu wa afya ya akili. Kwa nchi nyingi za kiafrika hasa Tanzania bado uelewa ni mdogo sana miongoni mwa jamii, ni wito wangu kwa serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dini pamoja na viongozi wa kimila kuona umuhimu wa kuitambua uwepo wa tatizo hili la afya ya akili na kuchukua hatua muhimu na kuweka nguvu kukabiliana nalo angali halijawa kubwa kwani likiwa kubwa udhibiti wake utakuwa wa gharama kubwa sana.

 

Post a Comment

0 Comments