ILIPOISHIA......................
Kisha alimkumbuka Nuru. Kiasi hofu ikamrudia alipojiuliza kama atafanikiwa kunusurika katika mapambano haya. Alikuwa amempa maelekezo yote muhimu na kusisitiza wakati gani aanze safari ya kutoroka zake endapo asingemwona.
Bila shaka hakuna hatakayehangaika kumtafuta msichana mmoja ambaye hana tofauti na wasichana wengine wakati mamia ya watu yakiungua, maelfu yakikimbia kwa fujo na mamilioni yakiwa yamepigwa na butwaa, wakati majumba na viwanda vitakuwa vikiteketea kwa moto mkali ambao mfano wake haujapata kutokea katika historia ya nchi hii na dunia kwa ujumla, wakati chombo kisichoonekana kwa macho ya nguvu ya kawaida kitakuwa kikielea angani; na baadaye kuanguka; nguvu yake inayokifanya kielee angani na za madini inayokifanya kutoonekana zikiwa zimekwisha.
Hapana, Joram hakuona kama Nuru angeshindwa kuitumia fursa hiyo. Bila shaka baada ya kumchanganya kwa hila alipokuwa akimfuata, atayafuata maelezo yote.
Joram asingejisamehe endapo lolote lingemtukia msichana yule na kumpotezea maisha. Licha ya kwamba uzuri wa Nuru haukustahili kuharibiwa kwa mkono wa Kaburu yeyote katili, ushujaa wake ulikuwa nguzo ambayo Joram aliitegemea sana. Yote aliyoyatenda, hekima na juhudi za Nuru zilimsaidia. Mungu msaidie arudi salama, alimwombea.
SASA SONGA NAYO...................
Utulivu aliokuwa nao pindi akiwaza hayo ulimfanya
panya mmoja amrukie kifuani na kujaribu kumwuma. Joram alimkwepa na kuliachia
teke dhaifu ambalo panya alilikwepa vilevile. Hata hivyo, panya huyo alimfanya
ayatoe mawazo yake nje na kuyarudisha katika pango hilo la mauti. Harufu mbaya
ya binadamu waliooza ikamrudia tena akilini na moyoni. Akajisikia kutapika
lakini akajikaza kisabuni.
Kisha alikumbuka kumtupia jicho jingine yule Mrusi.
Akashangaa kuona kundi dogo la panya likiwa juu ya uso wake, wakimla. Kwanza
alishangaa, kisha akaelewa. Mrusi huyo alikuwa amekata roho! Kichefuchefu
kikamrudia tena Joram. Alitamani afumbe macho asiendelee kuona ukatili wa panya
hao kumla mtu ambaye dakika chache walikuwa wakizungumza naye, mtu ambaye bila
shaka ni mwema sana. Vinginevyo angewezaje kujitolea aliwe akiwa hai? Joram
aliuliza.
Ghafla mwujiza ulitokea.
Joram aliuona mlango ukitikisika na hatimaye
kufunguka. Yeyote ambaye angeingia Joram alitegemea kumlazimisha ama amwue kwa
risasi ama amtoe chumbani humo. Hivyo, alisubiri kwa hamu akitazama kwa makini
tayari kwa lolote, heri au shari.
Bastola ilichungulia ikiwa katika mkono wa kike.
Ilifuatwa na uso mzuri, wenye jasho na damu. Uso wa Nuru.
“Joram?” alipiga ukelele wa furaha mara alipomwona
Joram kasimama kando akimtazama.
“Naweza kuyaamini macho yangu?” Joram alimwuliza akiwa
bado amesimama palepale. “Wewe ni Nuru kweli au malaika?” aliongeza.
Hakupata muda wa kujibiwa. Tayari Nuru alikuwa kifuani
mwake kamkumbatia kwa nguvu huku akilia kwa sauti ndogo. Wakati ikimpambazukia
Joram kikamilifu kuwa haikuwa ndoto – huyu alikuwa Nuru halisi aliyekuja
kumwokoa – alianza kuinua mikono yake ili naye amkumbatie. Lakini Nuru tayari
alikuwa amejitoa mikononi mwake na kumvuta nje harakaharaka huku akisema,
“Twende zetu. Wakati umewadia.”
Joram alimfuata kikondoo.
Wakiwa nje baada ya kupigwa na hewa safi, fahamu
zilimrudia Joram kikamilifu. Saa yake ilikuwa imevunjwa katika mapambano na
jitu lile, aliitazama ya Nuru na kuelewa kwa nini aliambiwa wakati umewadia.
Uhai ukamrudia mara moja rohoni, ingawa kimwili alikuwa bado dhaifu. “Niambie
Nuru tafadhali. Niambie, mitego tuliyoitega haijafyatuka tu? Mji haujaungua?”
Badala ya kumjibu Nuru alimwambia, “Sikiliza.”
Kwa mbali mjini kulikuwa na kelele nyingi za hofu.
Vilio na milipuko ya kutisha ilisikika kutoka katika kila upande. Walisikiliza
kwa nusu dakika, kisha Joram alitabasamu na kusema polepole, “Nadhani inatosha.
Wanakufa wenye hatia na wasio na hatia. Sasa iliyobaki ni ile kazi moja ya
mwisho. Kuulipua huu mtambo.”
Alimshika Nuru mkono na kuanza kukiendea tena chumba
cha mitambo. Nuru, akiwa na ramani halisi ya jengo hilo, alimshauri Joram
wapitie wapi. Dakika mbili baadaye tayari walikuwa wamewasili katika chumba
hicho.
Wahandisi watatu walikuwa chumbani humo, jasho
likiwatoka kwa mshughuliko wa kutoelewa kinachotokea, hawakuweza kuwaona Joram
na Nuru walioingia ghafla. Walipotanabahi walikuwa wakitazamana na bastola
mbili. Wakaduwaa. Mshangao wao ulikoma pale risasi za mfululizo zilipopenya
katika miili yao na kuwafanya waangukiane, damu zikiwavuja.
Joram aliikimbilia mitambo hiyo na kuanza kuikoroga
kama alivyokusudia. Alipotosheka aliyatoa mabomu yake ya mkono na kuyatega
sehemu mbalimbali za mtambo huo. Mara tu alipomaliza alimshika Nuru mkono na
kutoka naye mbio.
Nje ya jengo, kwa mbali, waliona moto mkali uliokuwa
ukipaa angani kwa namna ya kutisha. Kisha waliona kitu kingine cha kutisha.
Kundi la askari wenye silaha likija mbio kiwandani huko.
Joram aliduwaa kidogo, akijiuliza wafanye nini. Kurudi
ndani isingewezekana kwani jumba hilo pia lingelipuka wakati wowote. Na
kukimbia ingewachukua hatua chache kabla ya kukamatwa na risasi za askari hao.
Lakini Nuru, alijua la kufanya. Alimwongoza Joram katika upenyo alioutumia na
Von hadi nje ya uwa ambako walipiga mbio wakitegemea kumkuta rubani akiwemo,
ili wamlazimishe kwa bastola kuendeshwa kutoka nchini humo. Hakuwemo. Bila
shaka “miujiza” iliyokuwa ikitokea ilimtia kiwewe hata akaondoka zake, au
alikimbilia familia yake kwa matumaini ya kuiokoa. Hivyo, kiasi Nuru alikata
tamaa. Lakini Joram alimrejesha matumaini alipomwamuru kupanda mara moja.
Wakaingia.
Joram alikuwa na ujuzi wa nadharia juu ya kuendesha
helikopta. Alilazimika kujikumbusha ujuzi huo kwa vitendo, jambo ambalo
liliwagharimu zaidi ya dakika mbili. Wakati huo askari walikwishawaona na
kuanza kuwafuata kwa nguvu zaidi.
Askari mmoja aliamua kutokimbia, badala yake aliilenga
bunduki yake na kuiandaa kupiga.
Wakati huohuo jambo jingine la kushangaza lilitokea.
Jumba hilo, ambalo lilikuwa hifadhi ya mitambo haramu lililipuka kwa mshindo
mkubwa. Moto wa kutisha ulipanda juu na kusambaa kote.
Wakati askari hao walipokuwa wakitazama hilo, pia kwa
mshangao, helikopta ilikuwa angani. Walipokumbuka kupiga risasi ilikuwa
ikigeuzwa kuelekea Botwasana.
*****SURA
YA KUMI NA MBILI*****
“… NA kama anafanya mauaji hayo kulipiza kisasi dhidi
ya maafa ambayo utawala huu utayafanya katika nchi hii saa chache zijazo, bado
si kitendo cha kujivunia sana, kwani haitasaidia kitu,” Kombora alinong’ona.
Alikuwa akisema peke yake, akiwa kimya katika ofisi yake.
Hayo yalimtoka mara baada ya kutazama televisheni na
kusikia habari za kutatanisha kutoka BBC, bila shaka zikiwa zimekuja kutoka
Afrika Kusini bila hiyari ya utawala huo, kwamba Joram alikuwa ametoweka kutoka
katika jumba alilowekwa nchini humo. Kwamba mauaji ya ajabuajabu dhidi ya
makaburu katika nchi hiyo yalitokea usiku huo. Na kwamba kulikuwa na mashaka
kuwa mwuaji au wauaji hao hawakuwa wengine zaidi ya Joram na Kiango na yule
msichana anayefuatana naye, Nuru.
Habari hizo, zikiwa zimewasili pindi vyombo vyote vya
habari nzito zaidi ya hiyo zilipokelewa kama habari ndogo na kupuuzwa mara
moja. Kwa wananchi wa Tanzania na nchi nyingine ambazo zilikuwa mashakani
zikisubiri maafa makubwa kwa hofu na mashaka makubwa, walizipokea kwa shangwe
na vigelegele kwa dakika mbili tatu, dakika zilizofuata ikawa imesahauliwa.
Hofu ikachukua nafasi yake. Wakaendelea kusubiri, kusubiri kifo.
Waumini wa dini walikisubiri kifo katika makanisa na
misikitini. Wakristo walichubuka magoti kwa sala ndefu zilizoambatana na vilio.
Waislamu walivunjika migongo kwa kwenda rakaa huku wakimlilia Mola. Wasiomjua
Mola walikisubiri kwa namana mbalimbali. Wako waliotulia kwa utulivu, wako
waliopiga kelele na kuna wachache ambao waliamua kufa wakiwa wamelewa; hivyo,
chochote walichokuwa nacho walikitumia kununulia pombe. Watoto ambao walipata
hisia fulani kutokana na tofauti katika tabia za wazazi wao walitulia kimya,
kwa mara ya kwanza maishani mwao wakionja ladha ya hofu. Hata wanyama
wanaofugwa, kama kuku, mbwa, mbuzi na ng’ombe hawakuwa katika hali ya kawaida
kwani ilikuwa siku yao ya kwanza ambayo hawakushuhudia binadamu akila mayai,
kuchinja mbuzi wala kumkamua ng’ombe.
Jeshi liliwekwa katika hali ya hadhari, tayari kwa
lolote ambalo lingeweza kutukia. Lakini kwa vile madhara hayo yalikuwa
hayafahamiki yangetokea upande upi, na silaha ipi ingeweza kuyazuia, ilikuwa
dhahiri kuwa jeshi hilo lisingeleta upinzani wowote. Ilikuwa kama waliowekwa
tayari kusubiri kifo.
Rais na mawaziri wake, pamoja na viongozi wa ngazi za
juu katika Chama walijiinamia juu ya viti vyao vya Ikulu. Mengi yalikuwa
yamesemwa, mengi yalifanywa, lakini halikuwepo lolote lililoelekea kuwa
kipingamizi kwa maafa yaliyokuwa yakiendelea dakika baada ya dakika. Wao pia
ilikuwa kana kwamba waliamua kusubiri kifo kwa pamoja. Mara kwa mara walitazama
saa zao kisha wakatazamana. Kisha kiongozi mmoja aliinuka baada ya
kumnong’oneza jirani yake kuwa anakwenda haja. Hakurudi. Mwingine aliondoka
taratibu kwa madai hayohayo. Yeye pia hakurudi. Yuko ambaye alikwenda moja kwa
moja msikitini. Kuna aliyekwenda kanisani. Mwingine alikwenda nyumbani ambako
aliungana na familia yake, kusubiri kifo.
Tahamaki Rais alijikuta kabaki na Waziri wake Mkuu.
Walitazamana kwa muda, kisha mmoja aliyaepuka macho ya mwenziwe, wakizitazama
saa zao. Zilisalia dakika tano tu. Wakatazamana tena. Wakazitazama tena saa
zao. Dakika tatu… Dakika mbili… mmoja alimsika mwenziwe akiguna. Mwingine
aliinuka akiwa kaloa jasho ambalo hakufahamu lilivyoishinda air conditioner
ambayo ilikuwa ikifanya kazi kikamilifu. Kisha aliketi tena na kuyafumba macho
yake.
Dakika moja…
******
Dakika yoyote kuanzia sasa! Kombora aliwaza akitoka
dirishani alikokuwa akichungulia na kukirudia kiti chake. Alikuwa ameamua
lolote ambalo lingetukia limkute katika ofisi yake. Hakuiona haja ya ya
kutaabika wala kwenda kushuhudia maisha yanavyowatoka wanawe endapo nyumba yake
ingetukia kuwa moja kati ya nyumba zisizo na bahati.
Mara mawazo ambayo hakutaka yamjie akilini yakamtoka.
Mawazo ya upweke, unyonge na msiba mkubwa, mawazo ambayo yalikuwa yakimfunulia
hali ambayo angekuwa nayo endapo ingetukia yeye kuwa mmoja kati ya wale
watakaosalimika na familia yake nzima kuteketea. Angeishi vipi bila ya mama
watoto wake, yule mwanamke mpole ambaye hajaacha kumwonea haya kwa kiwango
kilekile walipokuwa wachumba hadi leo ambapo wamekuwa pamoja zaidi ya miaka
thelathini. Angeishi vipi bila ya watoto wake wanne, mmoja akiwa mwanamume
ambaye amehitimu Chuo Kikuu na kuajiriwa mwaka jana na wale wa kike ambao wote
wameolewa na kumpatia wajukuu watano? Maisha yangekuwa vipi endapo yote hayo
yangebadilika ghafla kwa ajili ya ukatili wa utawala dhalimu wa weupe wachache
huko kusini?
Kisha alikumbuka saa yake. Dakika kumi zilikuwa
zimepita! Hakuyaamini macho yake. Akayainua na kupiga hatua mbili tatu
kuliendea dirisha. Akachungulia chini. Mitaa yote ya Dar es Salaam ilikuwa
imetulia kabisa. Kelele ndogo zilisikika kwa mbali kutoka katika viwanda kadhaa
ambavyo vilikuwa vikiendelea na kazi. Kombora aliirudia meza yake na kuketi.
Masikio yake yalikuwa wazi yakisubiri kwa hofu kudaka mlio wowote wa mashaka
ambao ungesikika. Macho pia yalikuwa wazi yakitazama angani kupitia dirishani.
Dakika ishirini!
“Wakati wo…” alitaka kutamka. Sauti yake ilikatizwa na
ukelele wa ghafla ambao ulivuma ghafla katika anga. Bila ya kutegemea
aliyafumba macho yake kwa nguvu na kutamani kuweka vidole masikioni ili
asisikie zaidi. Kelele ziliendelea kwa mvumo mkubwa zaidi. Hisia zilimfanya
Kombora adhani kuwa zilikuwa kelele za kushangilia badala ya vilio na
maombolezo kama alivyotarajia. Akasikiliza kwa makini zaidi. Naam. Watu
walikuwa wakipiga vigelegele na kucheka kwa nguvu.
Watu wote!
Kama waliopatwa na wazimu!
Dakika moja baadaye Kombora alikuwa miongoni mwa watu
wengine katika chumba cha habari, ghorofa ya mwisho. Askari hao walikuwa
wakitokwa na machozi ya furaha huku wakisikiliza redio BBC ambayo ilikuwa
ikiendelea na taarifa.
…hadi sasa inaaminia kuwa utawala wa Afrika Kusini haujafanikiwa
kuuzima moto huu mkali ambao unateketeza majumba mbalimbali ya mjini
johanesburg. Kadhalika, haijafahamika watu wangapi wamefariki na wangapi ni
majeruhi japo inaaminika kuwa idadi hiyo itakuwa kubwa sana.
Kadhalika, mtambo wa siri ambao ulikuwa umejengwa na
utawala huo ukiendesha setilaiti ya aina yake, isiyoonekana kwa macho,
umelipuliwa na wahandisi wake wote kuteketea. Inasemekana kuwa baada ya mtambo
huo kulipuka chombo hicho cha ajabu kimeanguka katikati ya mji wa Johanesburg
na kusababisha madhara makubwa kwa maisha na mali za wananchi. Kadhalika,
inaaminika kwamba afya za wananchi katika mji huo zitakuwa mashakani kutokana
na nguvu ya nyuklia zilizoshirikishwa katika kukiunda chombo hicho. Kwa kila
hali inaonyesha dhahiri kuwa Joram Kiango alishirikiana na mwenzi wake, yule
msichana mzuri, Nuru, wameshiriki kwa njia moja au nyingine katika kufanya haya
yaliyofanyika huko Afrika Kusini. Na endapo wasingekifanya walichokifanya
dakika hii Afrika nzima ingekuwa katika msiba kwani kulikuwa na mipango ya
mtambo huo kuzishambulia nchi zote za mstari wa mbele kwa pamoja…
Kombora hakustahimili. Machozi mengi yalimtoka na
kuteleza juu ya mashavu yake, machozi ya furaha. Joram Kiango tena! Kwa mara
nyingine ameliokoa taifa lake na Afrika nzima kuepuka kipigo cha kikatili
ambacho kisingesahaulika. Joram, ambaye alimfikiria vibaya kwa kutoweka kwake
na pesa nyingi za umma ambazo amezichezea duniani kote.
Ghafla, ikampambazukia Kombora. Joram hakuwa ameziiba
zile pesa. Alizichukua kwa mtindo ule ili ionekane kama ameziiba ili azitumie
kwa shughuli hii pamoja na kuaminika kama msaliti mara aingiapo nchini Afrika
Kusini. Angeweza kuchukua hata zote! Kombora aliwaza. Angeweza kuzitumia
apendavyo! Kijana huyu ni nani kama sio malaika aliyeletwa kuishi kama binadamu
kwa manufaa ya binadamu wengine?
Kombora alirejea ofisini kwake. Mara tu alipoketi simu
zilianza kumsumbua. Nyingi zilikuwa za waandishi wa habari zikiuliza hili na
lile. Swali kubwa lilikuwa kutaka kujua kama kweli ni Joram Kiango aliyeifanya
kazi hiyo ambayo majeshi yote ya nchi za Kiafrika yasingeweza kufanya. Zaidi
walitaka kujua Joram yuko wapi.
Simu ambayo ilimsumbua Kombora kuliko zote ni ile
iliyotoka Ikulu. Alizungumza na Rais mwenyewe. “Tunamtaka haraka kijana huyu
ndugu Kombora. Kuna tuzo maalumu ya ushujaa ambayo inamsubiri…”
Kwa kadri Kombora alivyomfahamu Joram, hakuamini kama
angepatikana kwa urahisi kiasi hicho, na hasa kujitokeza aipokee tuzo hiyo
hadharani.
Siku mbili baadaye uhai ulilirudia jiji la Dar es
Salaam kama kawaida. Pilikapilika za mitaani, viwandani na maofisini
ziliendelea mtindo mmoja. Kila uso ulikuwa na furaha, tabasamu likiwa
karibukaribu. Jina la Joram lilikuwa katika fikra za kila mmoja. Ambao
hawakupata kumfahamu waliuliza huyu Joram ni nani?
“Humfahamu?” waliulizwa huku wakitazamwa kama
wapumbavu.
Tawi la Benki ya City Drive lilikuwa na uhai vilevile.
Wateja wengi walifurika kama kawaida wakiweka au kuchukua pesa, kuangalia
hesabu zao na shughuli nyingine mbalimbali. Pilikapilika hizo ziliwafanya
wasimtazame zaidi ya kawaida mzee huyu aliyevaa kanzu nyeupe na koti jeusi,
ambaye alikuwa na nywele na ndevu nyingi nyeupe kwa wingi wa mvi. Mkononi
alikuwa na mfuko mnene wa ngozi. Aliwapita wateja wote, akipokea shikamoo zake
hadi chumbani kwa meneja ambaye alimpokea kwa heshima zote, kwani haikuwa mara
kwa mara kutembelewa na watu wenye umri kama huo.
“Marahaba,” Babu huyo aliitikia. “Wewe ndiye meneja
mwenyewe?”
“Ndiye.”
“Ndiyo wewe uliyeibiwa zile pesa za kigeni?”
“Ni mimi, mzee.”
“Basi huu hapa mzigo wako,” mzee huyo alisema
akifungua mfuko huo na kutoa mabunda ya noti. Pesa za kigeni na shilingi chache
za Tanzania. “Nimetumwa na kijana mmoja anayesema anaitwa Joram nikuletee.
Amesema nikuombe radhi sana kwa kuzichukua. Alikusudia kuzitumia kwa safari
yake lakini alipata pesa nyingine kutoka kwa jasusi moja ambalo alilikamata
kule New Africa Hotel. Hivyo, alizitumia pesa zile badala ya hizi. Hata hivyo,
amesema zimepungua kidogo atalipa…”
Meneja alikuwa hamsikilizi kwa makini. Mshangao
ulikuwa umemshika. Alimtazama mzee huyo kwa muda kisha aliinama na kuanza
kuzihesabu kwa mabunda. Katika hesabu ya harakaharaka zilipungua dola mia
mbili. Akazirudisha katika mfuko wake na kuinua uso ili amshukuru mzee na
kumwambia la kufanya. Hakumwona. Mzee alikuwa ameondoka bila ya kuaga alipokuwa
kainamia meza.
Meneja huyo aliduwaa. Kisha alikumbuka la kufanya.
Akauchukua mfuko huo wa pesa na kuondoka nao hadi katika gari lake. Akalitia
moto hadi katika ofisi ya Kombora ambako alimwona moja kwa moja na kumsimulia
mkasa mzima.
“My God,” Kombora
alifoka. “Aliyezileta pesa hizo kwako hakuwa mzee. Alikuwa kijana sana, Joram
Kiango mwenyewe!”
Meneja huyo alizidi kushangaa. “Mbona alikuwa mzee,
Inspekta? Hata sauti yake ilionyesha…”
“Huyo ni Joram,” Kombora alimkatiza. “Ametumia moja ya
mbinu zake ili asipatikane na kupewa heshima yake. Amejifanya mkongwe kama
alivyofanya katika mkasa ule ulioitwa Salamu Toka Kuzimu.” Kombora alijiinamia
kwa muda. “Tulimhitaji sana,” alisema kama aliyemsahau Meneja huyo wa Benki na
badala yake kujizungumzia peke yake. “Anahitajika. Kumtafuta haitasaidia kitu.
Kwa jinsi ninavyomfahamu hatajitokeza hivi karibuni hadi hapo mchango wake
utakaposahauliaka, au litakapotokea suala jingine linalohitaji ushujaa."
***MWISHO****
0 Comments