ILIPOISHIA...............
Waliifika hoteli na kukiendea chumba chake kwa siri
kubwa. Mlango waliukuta ukiwa wazi. Wakaufungua na kuingia huku wakiufunga
nyuma yao. Macho yao yalivutwa na dalili za vurugu katika chumba hicho. Vitu
vilikuwa vimetupwa ovyoovyo, matandiko yakiwa yamepinduliwa na masanduku
kufunguliwa. Juu ya meza kulikuwa na karatasi yenye damudamu. Upande wa pili wa
karatasi hiyo kulikuwa na maandishi ambayo yalikuwa barua ya wazi kwa Joram
Kiango, barua ambayo haikutofautiana sana na ile ambayo Kombora aliiandaa: Ndugu
Joram,
Tunayo furaha kukufahamisha kuwa tumemchukua msichana
wako na tutakuwa nae hadi hapo tutakapomaliza shughuli zetu. Hii ni kwa ajili
ya kukuonya usithubuti kujihusisha na mambo yoyote yanayoitokea nchi hii.
Endapo utakuwa mtoto mtiifu kama ulivyo siku hizi, hatadhurika, nawe utakuwa
salama. Vinginevyo, utakipokea kichwa chake kwa njia ya posta na kisha
kitafuata kifo chako.
Amri
Kombora aliisoma tena barua hiyo, kisha akamgeukia
msaidizi wake na kumnong'oneza, "Tumechelewa sana. Wenzetu
wametuwahi." akampa barua hiyo ili aisome.
"Sasa tutafanya nini?" askari huyo aliuliza
baada ya kuisoma.
"Rudisha kila kitu kama kilivyokuwa. Fanya hima
tuondoke hapa haraka," alimhimiza akianza kusogea mlangoni.
"Nilidhani tungemsubiri Joram!"
"Hakuna haja. Akirudi atajua la kufanya."
Wakatoka na kuifuata njia ya kawaida. Wakiwa katika mavazi ya kiraia, watu
wachache sana waliwatupia macho zaidi ya mara moja. "Jambo moja la
kupendeza ni kwamba," Kombora alikuwa akisema. "Wamemchokoza Joram.
Hawamfahamu vizuri. Wataujutia uamuzi wao"
SASA SONGA NAYO...........................
Joram alifika chumbani kwake dakika kadhaa baadaye.
Akiwa mchovu, jicho moja likiwa limevimba kwa pambano lake na chonde,
alipitiliza hadi bafuni ili ayaepuke maswali ya Nuru. Huko ndani alioga vizuri,
akaisafisha damu yote na kushevu kikamilifu. Kisha akarudi chumbani ambako macho
yake yalivutwa na vurugu iliyokuwa imetokea.
Alitazama vitanda vyote na kutoiona dalili ya Nuru.
Akaenda mezani ambako hakushangaa kukuta ujumbe ule ukiwa juu ya karatasi yenye
damudamu. Akausoma kwa makini, akiuchunguza mwandiko huo ambao ulikorogwa katika
hali ya kupoteza uhalisi wake. Akatikisa kichwa na kutokwa na tabasamu
jembamba.
Usiku huo alilala huku kalisahau tabasamu hilo katika
uso wake.
ASUBUHI hiyo, baada ya kuoga na kufungua kinywa, Joram
alichukua simu na kupiga namba mbili tatu akitaka kuzungumza na rafiki zake wa
zamani. Alipowapata aliwapa maekelezo fulanifulani kwa lugha ambayo wangeielewa
wao tu. Baada ya hapo akajitokeza mitaani na kuanza matembezi. Akiwa kavaa
vizuri suti yake ya kijivu aina ya three peace, kofia ikiwa imezifunika nywele
zake ili kuficha mchubuko uliokuwa upande wa kushoto na miwani myeusi
ikilificha jicho lake ambalo lilikuwa halijatii dawa kikamilifu, alionekana
kama alivyotaka, mwungwana asiye na tatizo lolote mwilini wala akilini.
Msafara wake wa kwanza uliishia Barabara ya Sokoine
katika tawi la Benki ya Taifa ya Biashara City Drive. Aliingia ndani na kuomba
kuonana na meneja. Akaelekezwa hadi katika chumba ambamo alikaribishwa vizuri
na afisa huyo ambaye uso wake ulimdhihirishia Joram kuwa hakuwa akiwajibika ili
kuitikiwa wito bali kuwajibika kulikuwemo katika damu yake tangu alipozaliwa.
"Nikusaidie nini ndugu yangu?"
"Naitwa Joram Kiango. Ninayo akaunti hapa."
"Nakufahamu sana, ingawa ni mara yangu ya kwanza
kukuona ukija huku kwetu. Mara nyingi unaishia huko huko kwenye pesa."
Baada ya kutabasamu kidogo kwa mzaha huo aliongeza harakaharaka. "Umefuata
mkopo?"
"Hapana mzee," Joram alimjibu.
"Nikikopa nitashindwa kulipa. Ninachohitaji ni kutazama uwezekano wa
kuweka mali yangu fulani ya thamani katika akaunti mnayoita Self-Custody.
Ningependa mnifahamishe utaratibu ulivyo."
Meneja alitikisa kichwa huku akisema, "Hilo tu?
Kwanini wamekusumbua hadi huku? Utaratibu wake si mrefu sana. Ziko fomu maalumu
ambazo utajaza. Baada ya hapo utakabidhiwa ufunguo mmoja, ufunguo wa pili
tutakuwa nao. Utakwenda huko chini na kuhifadhi mali yako hadi siku ambayo
utapenda kuikagua au kuichukua. Malipo yake ...."
Joram alimsikiliza kwa makini, akitupa swali moja
moja. Kisha alimwomba meneja akatazame hali ilivyo huko chini kabla hajajaza
fomu zozote. Meneja akainuka na kushuka nae hadi shimoni. Walipita vyumba vya
kuhifadhi nyaraka, baadhi vinahifadhiwa pesa na kimoja alielezwa kuwa
kiliazimwa na Benki Kuu baada ya jengo lao kuharibika kwa moto. Baada ya kupewa
picha kamili ya ulinzi na usalama wa hifadhi hiyo Joram aliaga na kuahidi kuwa
angerudi baadaye kukamilisha kazi hiyo.
Toka hapo Joram alipita hapa na pale akifanya hili na
lile, sigara baada ya sigara zikiteketea mdomoni, mwendo wake ukiwa wa utulivu
kama mtu asiye na tatizo lolote ulimwenguni. Ungemwona kamwe usingefikiria kama
mtu ambaye usiku wa jana mpenzi wake alitekwa nyara, bila shaka baada ya
kuteswa sana.
Ni hali yake hiyo ya utulivu ambayo ilimshangaza
Inspekta Kombora alipokutana nae katika mtaa wa Samora. Kombora alisimamisha
gari lake na kumfuata Joram kando ya duka alipokuwa kasimama.
"Joram," alisema baada ya kumsalimu. "Nasikia yule msichana wako
ametekwa nyara".
"Hata mimi nasikia hivyo," lilikuwa jibu la
Joram.
"Mbona hufanyi lolote."
"Nifanye nini? Barua imenionya nisithubutu
kufanya lolote. Vinginevyo, msichana wa watu atauawa. Unapenda afe,
Inspekta?"
Kombora alitikisa kichwa kwa mshangao. "Joram
niliyemfahamu mimi alikuwa hapokei amri kwa watu kama hao, hasa katika suala
hili ambalo ni la uhai na kifo cha mtu na taifa zima. Mimi nilidhani
wamekuchokoza. Nikategemea kuwa wangejutia uamuzi wao. Nilikosea?"
"Umekosea sana Inspekta. Joram unayezungumza naye
si yule wa awali. Usishangae, Inspekta. Usiupoteze bure mshangao wako. Bado
kuna mengi utayasikia juu ya Joram huyu ambayo yatakushangaza zaidi,"
Joram alisema huku akitupa kipande kimoja cha sigara na kuwasha nyingine.
Alipomuona Kombora kama mtu ambaye hajui la kufanya au asiyeyaamini masikio
yake, akaamua kuondoka polepole. Kombora alimsindikiza kwa macho yake yaliyojaa
mshangao na huzuni.
Baada ya pitapita hii ya hapa na pale, Joram alirejea
chumbani kwake ambako alijipumzisha kwa muda. Wafanyakazi na baadhi ya
wapangaji wenzake, ambao walikuwa wamemzoea Nuru, walimsumbua Joram kwa
kutomuona.
"Anaumwa?"
"Hapana. Kapata safari ya ghafla."
"Bila kuaga?"
"Ilikuwa ghafla."
Aliujenga vyema uongo wake huo hadi ukafanana na
ukweli. Jioni hiyo, baada ya kula, kuoga na kupiga simu nyingine alijitokeza
mitaani na kuanza matembezi yake. Safari hii matembezi hayo yaliishia Ilala,
nyumbani kwake. Alielekea chooni ambako alifunua mahala fulani pa siri ukutani
na kutoa kijisanduku alichokuwa kakificha hapo. Alishangaa kukuta kikiwa kitupu
bila ya bastola na risasi zake ambazo alikuwa ameziweka huko. Hifadhi hii
ilikuwa siri yake binafsi. Mtu pekee ambaye aliifahamu siri hiyo ni Neema Idd
ambaye sasa ni Marehemu. Mtu mwingine ambaye angeweza kufahamu ni Nuru. Uko
usiku mmoja, kati ya zile chache ambazo waliwahi kulala katika nyumba hii,
alimtoroka Nuru akidhani yuko usingizini, akaja hapa na kuisafisha bastola hii.
Pengine Nuru aliwahi kumchungulia. Lakini Nuru huyo sasa yuko mikononi mwa
wateka nyara. Nani mwingine aliyeijua siri hii? alijiuliza kwa hasira, hasira
ambazo zilimfanya atupe kasha hilo na kutoka nje baada ya kuifunga milango yote
kwa ukamilifu. Msafara huu uliishia katika hoteli ya Embassy. Akaagiza vinywaji
na kuanza kunywa. Baada ya bia mbili akaenda kaunta kuzungumza na yule msichana
wa mapokezi.
"Shem, za kutwa."
"Nzuri sana, shemeji," msichana huyo
alizungumza kwa furaha huku akimtazama Joram kwa mshangao. "Pole sana
shemeji," aliongeza.
"Kwa?" "Ule mchezo wa jana. Unajua mimi
mpaka sasa siamini kama mlikuwa mnacheza tu. Nilidhani mlikuwa mnapigana. Yule
bwana kashikilia kuwa ni mchezo tu".
"Ulikuwa mchezo. Mazoezi ya viungo. Wazungu huita
practice."
"Mpaka mtoane damu?"
Hakujua Joram alivyoisherehekea habari hiyo. Alitupa
maneno mengine mawili matatu, kisha akairudia meza yake. Akaendelea kunywa na
kuvuta. Japo alionekana katika hali ya utulivu, lakini macho yake yalikuwa
makini, yakimtazama kila anayeingia na kutoka. Aliwaona wengi. Na kati yao
alikuwemo yule ambaye alihitaji kumwona.
Alikuwa rafiki au adui yake, Chonde. Aliingia na kuifuata
meza ambayo haikuwa na mtu, akaketi. Mara tu Joram alipomwona akainuka na
kwenda kupiga simu ambayo alizungumza maneno machache sana. Kisha alikirudia
kiti chake na kumwita mhudumu ambaye aliombwa kuleta bia nne. Mhudumu huyo
alipozifikisha chupa hizo Joram alimwelekeza azipeleke kwa Chonde. Kisha
alitulia akimtazama Chonde alivyokuwa akibishana na mtumishi huyo kwa zawadi
hiyo ambayo hakujua ilikotoka hadi alipoelekezwa na kumwona Joram. Akazipokea
na kuanza kunywa.
Lakini baada ya dakika kumi meza ya Joram ilifurika
kwa chupa kumi zilizoletwa na mtumishi yuleyule kwa niaba ya Chonde.
Walitazamana kwa muda. Baada ya muda Chonde alihamia meza ya Joram.
"Za tangu jana?"
"Siyo mbaya."
Wakaendelea kunywa kwa muda. Kila mmoja akimsoma
mwenzake. Kisha Chonde alitokwa na kicheko chembamba. Joram aliungana naye kwa
tabasamu dogo.
"Pole sana."
"Kwa?"
"Yale ya jana."
"Lilikuwa zoezi tu. Usijali."
Kikafuata kimya kingine, kimya ambacho Joram
alikivunja kwa kuanzisha maongezi ambayo Chonde alizungumza kwa uangalifu
akiepuka lolote ambalo Joram alihitaji kufahamu juu yake. Pamoja na Joram
kuzungumza kwa ujanja na hila za kila aina, bado Chonde alimfanya ajione mtoto
sana katika dunia ya upelelezi na mzembe katika elimu ya saikolojia. Ni hapo
alipozidi kuamini kuwa Chonde hakuwa mtu wa kawaida. Na kama alikuwa jasusi
bado hakuwa jasusi la kawaida. Alikuwa zaidi. Jambo hilo liliongeza hasira za
Joram dhidi ya mtu huyo. Amshinde vipi katika mapambano ya mwili na amshinde
tena katika mapambano ya kiakili? Hata hivyo Joram hakujali sana, akijua kuwa
dakika hii ambayo anaipoteza na Chonde, mahala fulani, yuko mtu ambaye
anaifanya kazi ile ambayo yeye alishindwa kuifanya jana, kazi ya kufungua kile
kijaluba cha Chonde na kuona kimehifadhi nini hata kilindwe kwa kiwango kama
kile. Hivyo, akaamua kumruhusu Chonde aendelee kumlaghai na kumdhihaki.
"Mwanamapinduzi aliyekata tamaa," Chonde
alisema. "Aibu ilioje kukata tamaa hali nchi yako iko mashakani? Si
ungejaribu kutoa mchango wako?" Joram hakumjibu.
Kisha kama aliyekumbuka jambo Chonde alisema ghafla,
"Nasikia msichana wako ametekwa nyara!"
“Umesikia wapi?"
"Kwani ulidhani siri?"
Hilo lilimshitua Joram. Alishangaa kuona mtu huyo
alivyo mwepesi wa kupata habari. Baada ya kuisoma barua ile Joram hakuipeleka
polisi wala kuchukua hatua zozote zaidi ya kutabasamu tu. Lililomfanya asifanye
lolote hasa ni kule kuwa kwake na uhakika kuwa barua ile aliielewa zaidi ya
mwandishi wake alivyotaka aielewe. Bila shaka mtu huyo alikuwa amezidokoa
habari hizo kwa polisi. Jambo hilo lilimfanya azidi kumfanya Joram kuamini kuwa
hakuwa mtu mwenye mkono mrefu tu bali alikuwa na masikio mapana.
Yeyote aliyeketi kando akiwatazama watu hawa wawili
wakiongea angeamini kuwa ni kikao cha marafiki wa siku nyingi. Asingeamini kuwa
yalikuwa kama maongezi baina ya Chatu na Mbwa, au baina ya Malaika Gabriel na
Ibilisi.
Yule msichana wa mapokezi alikuwa mmoja kati ya watu
walioamini hivyo. Alikuwa amewatazama kwa muda mrefu na kushuhudia wanavyocheka
na kutabasamu, akayasahau mashaka yote aliyokuwa nayo juu ya urafiki wao na
kuamini kuwa pambano la jana lilikuwa zoezi la viungo. Hivyo, alizama katika
shughuli zake na kuwatupia jicho mara moja moja.
Chonde alikuwa akifunua mdomo kuongea kitu wakati saa
yake ilipotoa mlio ambao haukuwa wa kawaida. Ulikuwa mlio wa sauti nyembamba
sana, ulimfikia Joram kwa mbali sana. Chonde aliitazama saa hiyo kwa utulivu,
kisha alimtazama Joram kwa makini zaidi. Dakika mbili baadae aliendelea kunywa
kwa utulivu. Dakika ya tatu aliinuka na kuaga kuwa anaelekea msalani. Joram
alisubiri dakika tano, kisha akamfuata. Hakumkuta. Akafahamu kuwa mlio katika
saa ya chonde ulikuwa ishara ambayo ilimkumbusha kitu fulani, jambo
lililomfanya Joram kuhofia mtu wake ambaye wakati huu alikuwa katika chumba cha
Chonde. Hivyo, akakiendea kibanda cha simu na kuzungusha namba za simu za
chumba hicho. Haikupokelewa. Toka kwenye simu, Joram alitoka nje ya hoteli na
kukodi gari ambalo lilimpeleka New Afrika. Akajipenyeza kwa hila hadi
ghorofani, mbele ya chumba hicho. Akatega sikio na kusikiliza kwa makini.
Chumba kilikuwa kimya kabisa. Ukimya huo ulimtisha sana. Aliyaamini sana
masikio yake. Na kwa vyovyote alitegemea kuwa na mtu chumbani humo. Akasikiliza
kwa makini zaidi. Bado hakusikia chochote. Akaufungua mlango taratibu na
kuchungulia.
Macho yake yalivutiwa na mtu aliyelala chali juu ya
sakafu utumbo wake ukiwa nje, macho yake yakidhihirisha kuwa roho ya mtu huyu
pia ilikuwa nje. Kabla Joram hajajua kuwa ilimpasa kuingia chumbani humo au la,
sauti nzito aliyoifahamu sana ilimhimiza ikisema, "Usiogope. Karibu
ndani."
Msemaji alikuwa kajificha nyuma ya mlango, bastola
kubwa ikiwa mkononi mwake ikimtazama Joram kwa uchu.
"Ingia na ufunge mlango. Nadhani hutapenda kufia
hapo mlangoni kama paka. Njoo ndani ufe kistaarabu kidogo."
Joram akaingia. Hakujishughulisha kumtazama Chonde
aliyesimama nyuma ya mlango na bastola yake. Badala yake alimtazama marehemu na
kushuhudia alivyouawa kinyama. Tumbo lake lilikuwa limebomoka kwa kitu ambacho
hakikuwa risasi wala kisu. Bila shaka ulikuwa mlipuko wa bomu. Kifo hicho
kilimsikitisha sana Joram. Huzuni ikamshika. Kwa huzuni hiyo alimgeukia Chonde
na kufoka kwa hasira akisema, "Shetani mkubwa. Kwa nini umemwua mtu huyu
asiye na hatia?"
"Ni wewe uliyemwua," Chonde alimjibu Joram.
"Mimi! Nimemwua vipi?"
"Usijifanye hufahamu. Bila shaka ni wewe
uliyemtuma kuifanya kazi ile ambayo mwenyewe ilikushinda. Kazi ya kujua katika
kisanduku hicho mna nini. Nami nikifahamu kuwa pamoja na kukuadhibu, kama
nilivyokuadhibu usiku wa jana usingekata tamaa ndipo niliamua kutega bomu dogo
kando ya kisanduku hicho. Wakati huohuo mtu yeyote anayekigusa saa yangu
inaniashiria. Hivyo tulivyokuwa tukinywa hapo hotelini nilishangaa kuona dalili
za mtu.
“Nikafahamu kuwa mtu asiye na hatia anakufa. Nimemkuta
kisha kata roho.” Akageuka kumtazama marehemu kwa muda. Kisha aliyarejesha
macho katika uso wa Joram na kusema, "Ni wewe uliyestahili kuwa chali,
utumbo nje, badala ya mtu huyu, Joram.”
Joram asingeweza kukanusha. Kifo cha kijana huyo
kilimsikitisha sana. Alikuwa mmoja kati ya vijana wake smart ambao huwatumia
kwa hili na lile, kijana ambaye alikuwa amemsaidia sana katika harakati zake
zilizopita. Hakupata kushidwa hata mara moja isipokuwa leo ambapo ameyapoteza
maisha yake. Joram akajilaumu kumtuma katika kadhia hiyo. Hamu yake ilikuwa ni kumshinda
na kuutawanya ubongo wake sakafuni...
Kama aliyekuwa akiyasoma mawazo yake, vilevile Chonde
aliongeza kwa sauti nzito, "Hata mimi sikufahamu kama wewe ni mtu hatari
sana Joram. Unastahili kufa mara moja."
Maisha yakiwa ukingoni, Joram alijua kuwa alihitaji
kuikusanya akili yake yote ili ajiokoe. Hakujua afanye nini. Walikuwa na
bastola moja tu, na ilikuwa katika mikono ya Chonde. Kuipata bastola hilo
ilikuwa ndoto ya mchana. Chonde alikuwa macho kama kipepeo. Na bado Joram
asingemudu kuitumia mikono yake. Hata hivyo, alitegemea kitu kimoja tu
kimsaidie kutafuta muda wa kuokoa maisha yake. Muda. Muda waweza kufanya
maajabu. Hata asipookoka, si inapendeza endapo ataufaidi uhai wa dakika chache
zaidi.
"Najua ninakufa," alisema. "Nadhani
unafahamu vizuri kuwa nakufa kwa ajili ya tamaa ya kutaka kujua siri
uliyoificha katika kijisanduki hicho. Nifanyie basi wema wa mwisho. Nifungulie
kisanduku hicho nife nikijua mna nini."
Chonde alicheka, "Tatizo lako Joram ni kule
kufikiria kuwa unacheza na mtoto mdogo. Unachojaribu kufanya ni kuvuta muda.
Wakati huohuo unathubutu kuendelea na upelelezi wako ili endapo lolote
litatokea - kitu ambacho siamini - utoroke na kutoa siri hiyo nje. Kwa taarifa
yako siri iliyoko katika kisanduku hicho ni nzito kuliko bara zima la Afrika.
Kwa maneno mengine, ni siri ambayo dunia nzima inapigania kujua. Kwa bahati
mbaya watu tunaoifahamu siri hiyo ni wachache sana. Na tumeshona midomo. Hata
maiti siwezi kuisimulia siri hiyo. Nadhani hilo linakutosha. Sasa jiandae kufa.
Ungependelea risasi ya kichwa au kifua?"
Joram alimtazama usoni na kuliona tabasamu la
kifedhuli katika macho yake, tabasamu ambalo halikuwa na mzaha. Akajaribu
kuicheza tena karata yake ya mwisho. "Jana ulinishinda kwa judo. Vipi
ukiniua kwa mikono? Nadhani ni aibu na dalili za uoga kutumia risasi pasipo na
umuhimu."
Chonde alicheka tena. "Ningependa kukuua kwa
mikono mitupu. Hata hivyo, sina muda wa kutosha. Umebakiwa na nusu dakika ya
kuishi. Utapenda kufa ukiwa umefumba macho au nikuue ukinitazama?"
Sasa mzaha ulikuwa mbali na sauti ya Chonde. Mauaji
yalikuwa wazi katika macho yake. Joram akajua kuwa maisha yake yamefika
ukingoni. Akiwa ameshuhudia vifo vingi vya risasi alitabasamu kimoyomoyo na
kuamini kuwa hatimaye zamu yake imefika. Hata hivyo, bado aliyapenda maisha.
Bado aliipenda dunia. Na alikuwa akiiacha moja kwa moja. Hivyo, badala ya
kuyafumba macho yake aliyafumbua kwa nguvu na kuyakaza usoni. Hiyo pia
aliifanya kuwa karata yake ya mwisho kwani kuua si mchezo, hasa kumwua kiumbe
asiye na uwezo wa kujitetea.
Ilimsaidia. Nusu ya dakika ilipita Chonde kaielekeza
bastola katika kifua cha Joram, kidole chake kikigusa kiwambo cha kufyatulia
risasi, lakini alisita kuifyatua. Mara mlipuko wa bastola ukasikika. Joram
alijirusha kando na kutua chini ambapo aliruka tena hadi upande wa pili wa
kitanda. Risasi mbili tatu zaidi zikasikika, kama zinazopigwa bila shabaha
yoyote. Kisha kimya kikafuata. Kimya hicho kilitoweka kwa mkoromo wa mtu
aliyekuwa akikata roho. Ndipo Joram alipojiinua na kuchungulia. Ikamshangaza
kumuoa Chonde kalala chini, kifudifudi, damu zikimvuja katika tundu kubwa la
risasi katika uso wake. Joram alichupa na kuirukia bastola iliyokuwa mikononi
mwa Chonde. Akajicheka kwa kuona akipokonya bastola kutoka katika mikono ya
marehemu aliyekata roho kitambo. Akaikimbilia suit case ya chonde pamoja na
kile kisanduku. Akavichukua na kuanza kutoka.
Mara mlango ulifunguka ukifuatwa na bastola ambayo
ilichungulia kwa uangalifu. Bastola ikaingia ikifuatiwa na binadamu ambaye
aliufunika uso wake kwa kofia kubwa na miwani. Alikuwa kavaa suruali na koti la
kiume katika hali ambayo ingemfanya mtu yeyote amfikirie kuwa pande la
mwanamume. Lakini Joram alimfahamu mara moja. Akaitelemsha bastola yake ambayo
aliishika na kumkimbilia huku akisema kwa furaha, "Nuru nawezaje
kukushukuru Nuru?"
Walikumbatiana na kubusiana kwa furaha.
Kisha walitengana mara moja na kutazamana.
"Umewezaje kunifahamu mara moja kwa urahisi kiasi hiki? Tangu nimetoweka
watu wanashindwa kunifahamu".
"Nadhani nakufahamu zaidi ya wanawake wote. Zaidi
ya hayo nani mwingine ambaye anaweza kuhatarisha maisha yake kuipenyeza risasi
katika tundu la ufunguo ili kumwua mtu ambaye alikuwa tayari kuniangamiza? Kwa
kweli sijui namna ya kukushukuru Nuru!" Wakakumbatiana tena.
"Nuru! Niliwahi kukwambia kuwa u mzuri? Niliwahi
kukuambia kuwa hawakukosea waliposema kuwa wewe ni binadamu aliyekuja duniani
kwa makosa badala ya kuwa malaika kama ulivyokusudiwa? Nadhani walikosea Nuru.
Wewe ni malaika. Tazama ulivyo mzuri! Tazama ulivyotokea na kuipokonya roho yangu
kutoka katika kinywa cha mauti. Nuru, nawezaje kukushukuru Nuru?"
Hayo yalipita katika kichwa cha Joram wakiwa
wamekumbatiana. Joram alitamani kuyatamka kwa sauti, lakini hakufanya hivyo.
Badala yake alisema, "Nakupenda."
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Nuru kumsikia Joram
akilitamka neno hilo. Mara kwa mara alimtesa kwa kutojua kama kweli alimpenda
au la. Ingawa walifanya mapenzi, mara nyingi, lakini bado Joram hakuwahi
kulitamka neno hilo kwa sauti ambayo ililipa uzito kama huo. Kadhalika, macho
yake hayakufichua mapenzi yake kwa hali yoyote. Hivyo, kwake ilikuwa zaidi ya
habari njema. Hata hivyo, bado alikuwa na la kusema. "Sikuamini
Joram," alimnong'oneza. "Pamoja na kutoweka kwangu nikiwa nimetekwa
nyara hukujishughulisha kunitafuta. Walao kutoa taarifa polisi."
Joram akaangua kicheko. "Usinichekeshe Nuru.
Waweza kuwa ulifanikiwa kuwalaghai watu wote pamoja na polisi, lakini mimi
hukunidanganya. Nilijua kuwa ilikuwa hila uliyoiandaa tu ili unishawishi
kuingia katika vita. Mwandiko wa barua ile pamoja na kuuvurugavuruga, kwa mtu
aliyesomea miandiko kama mimi, nilifahamu kuwa ni wako. Vilevile ile damu
iliyodondoka pale haikuwa na uzito wowote. Nilijua umejikata kidole makusudi.
Na ile vurugu iliyofanyika chumbani haikuwa na umuhimu. Kwa vyovyote, majasusi
khatari kama hawa wasingefanya mchezo usio na umuhimu kama ule. Hivyo, nilikuwa
nikikusubiri nikitegemea utokee na tuendelee na starehe zetu."
"Starehe?" Nuru aliuliza kwa mshangao.
Alishangaa kuona Joram alivyoigundua hila yake kwa urahisi. Ilimshangaza zaidi
alipodai starehe wakati wamesimama kando ya maiti mbili ambazo zilikuwa hata
hazijapoa kwa ajili yao. "Starehe Joram? Nilidhani tumeingia kazini."
Joram akatabasamu. "Sikia Nuru, siyo tabia nzuri
kuzungumza kando ya maiti za binadamu. Pamoja na kwamba bastola zilizotumika
zilikuwa na viwambo vya kupoteza sauti bado mtu yeyote anaweza kutokea na
kutukuta katika hali hii. Nasi hatuna muda wa kuyajibu maswali ya polisi.
Twende zetu mara moja," alimaliza akiichukua mizigo yake na kuanza kutoka.
"Nifuate. Twende kwa utulivu kama tutokao chumbani kwetu."
"Kumbuka tu wanaume wawili," Nuru alisema
akitabasamu.
Waliteremka na kuiacha hoteli bila ya tatizo lolote.
Watu wawili watatu waliokutana nao waliwatazama kikawaida.
Baada ya kuingia mitaani Nuru aliifichua bastola na
kumpatia Joram akisema. "Chukua bastola yako. Samahani kwa kuichukua bila
idhini yako. Nadhani uliihitaji sana. Ningeweza kukupotezea maisha."
Tabasamu likamtoka Joram. "Hata hivyo umeniokoa.
Kama ningeingia nayo pengine Chonde angeniua kwanza na kunisimanga
baadaye," Joram alijibu. "Nimepata nyingine. Hii umeipataje?"
"Nilienda kwako kuichukua".
"Na umewezaje kunusa kuwa niko katika chumba kile
nikisubiri kufa hata ukaja kuniokoa?"
"Ni rafiki yako aliyekuokoa. Hayati Edward
ambaye, kwa bahati mbaya, mshenzi yule amemwua. Unajua nilipotoka hotelini kwa
kisingizio cha kutekwa nyara, nilienda kujificha kwake? Tulijadiliana nae namna
ya kurudisha moyo wako katika msimamo unaotakiwa. Mara ukampigia simu na kumpa
maelekezo ya kwenda kufungua kisanduku hicho. Aliponieleza maelezo yako na
jinsi ulivyoponea chupuchupu mara ya kwanza ndipo nilijua kuwa umerudi kazini.
Nilitaka nije kwako mara moja. Lakini yeye aliniomba nisifanye pupa. Akaniomba
nifuatane nae katika hoteli na kujificha kando nikimlinda. Nilifanya hivyo.
Mara nikaona mtu mwenye dalili za kikafiri akiingia chumbani humo, bastola
mkononi; ingawa ilifichwa sana. Kabla sijafahamu la kufanya nilikuona wewe pia
ukinyatia na kuingia. Ndipo nilipojivuta mlangoni na kuchungulia katika tundu
la ufunguo. Nikamwona Chonde akiwa tayari kukuua. Sikuwa na la kufanya zaidi ya
kumlenga na... na ..."
Mara Nuru aliangua kilio. Akamgeukia Joram na
kumkumbatia kwa nguvu akisema, "Nimeua mtu... Nimeua mtu, Joram..."
"Watu huuawa," Joram alimnong’oneza.
"Hebu jitahidi kuwa msichana shujaa kama ulivyo, Nuru. Usingemwua
angeniua. Watu watakusikia. Twende zetu chumbani."
"Lakini nimeua, Joram... nimeua..."
******
Ulikuwa usiku mfupi sana kwa Joram. Alikuwa na mengi
ya kufanya ambayo hakuweza kuyatekeleza. Ilimchukua muda mrefu kumshawishi Nuru
kwa vinywaji na mahaba ili asahau hofu yake ya kuua mtu. Baada ya usiku wa
manane ndipo Nuru alipoacha kuweweseka na kupitiwa na usingizi mzito. Lakini
alimkumbatia Joram kwa nguvu. Ilimlazimu Joram kutumia hila fulani na kujitoa mikononi
mwake na kumfanya akumbatie mto.
Akinyata kwa utulivu, Joram alikiendea kisanduku cha
marehemu Chonde na kutazama uwezekano wa kukifungua. Isingekuwa kazi rahisi.
Ilihitaji utaalamu wa hali ya juu au risasi ya bastola. Joram hakuwa tayari
kuitumia risasi kwa hofu ya kumwamsha Nuru. Na utaalamu siyo jambo ambalo
lingepatikana kwa dakika moja. Hivyo, alikiweka kando kisanduku hicho na
kuuchukua mfuko wa Chonde ambao haukumchukua muda kuufunua mifuko yake ya siri
ambamo alitoa nyaraka mbalimbali na kuzisoma kwa makini. Yale maandishi wa
kijasusi ni jambo jingine ambalo lilihitaji muda na utulivu mkubwa ili
kueleweka. Hivyo, hakupoteza muda kujaribu kuyasoma. Badala yake alichukua hati
ya kusafiria ya Chonde, kile kijisanduku na nyaraka zote alizoona muhimu. Vitu
vingine alivifungafunga katika mfuko na kuvificha mahala ambapo aliamini kuwa
visingepatikana kwa urahisi.
Baada ya hapo alichukua begi lake na kutoa vitu vyote
vilivyokuwemo. Alichukua kinyago fulani cha hoteli na kukifunga katika mfuko wa
nailoni na kuutumbukiza katika begi lake. Akalinyanyua kupima uzito wake. Kisha
akaliweka mezani, na kuacha balbu ambayo ilikuwa ikitoa nuru nyekundu iendelee
kuwaka. Akalitupa taulo lililokuwa kiunoni mwake na kujilaza kitandani kwa
utulivu akiutoa mto aliokuwa ameukumbatia Nuru na kuichukua nafasi hiyo.
Akainua mikono ya Nuru na kuifanya ituwe kiunoni mwake. Akayafumba macho yake
na kujifanya kulala. Lakini asingeweza kulala alikuwa akiyasubiri mapambano kwa
hamu.
Joram hakujua kuwa alikuwa amepitiwa na usingizi
mzito. Alipoamka alikutana na macho mazuri ya Nuru yakimtazama kwa utulivu.
"Za asubuhi, mpenzi," Nuru alimsalimu Joram.
"Nadhani siyo mbaya."
Nuru alitulia kidogo kabla ya kuongeza, "Nilikuwa
nikisubiri uamke ili tuzungumze mpenzi. Nadhani haya yatakuwa maongezi yetu ya
mwisho".
"Kwa vipi?"
"Unajua jana nimeua mtu? Wakati wowote polisi
watafika hapa na kunitia pingu. Endapo nitanusurika kitanzi siwezi kunusurika
kifungo cha maisha." Akasita tena na kuongeza, "Leo nimeota mpenzi.
Nimeota nikining'inia juu ya kitanzi. Wewe na watu wengine mkiwa kando
mkinicheka. Nilijaribu kukuita unisaidie lakini sauti haikuweza kutoka."
Joram akacheka. "Nani aliyekwambia kuwa
utafungwa? Polisi wangemfahamu mtu aliyemwua bila shaka ungepata medali ya
dhahabu badala ya kukuvika pingu. Licha ya hayo, hawawezi kabisa kufahamu nani
alimwua. Unajua, uliingia hotelini mle ukiwa mwanamume? Ni mimi tu niliyeweza
kukufahamu," Joram akacheka tena. "Lakini yote hayo ya nini? Leo
tunaenda zetu Nairobi."
"Kufanya nini?"
"Kutumia."
Nuru akashikwa na mshangao. "Nilidhani umeingia
kazini Joram."
Joram alitabasamu kabla ya kumjibu akisema. "Kuna
mpelelezi mwenzangu maarufu anayeitwa Willy Gamba, aliwahi kusema kazi na dawa.
Mpelelezi ni binadamu vilevile. Lazima astarehe na kuburudika. Yawezekana
tutaenda Nairobi tukiwa kazini. Sasa, sikia Nuru. Nitafunga mizigo yetu yote na
kukutaka ukanisubiri Uwanja wa ndege. Hapana usiende Terminal II nenda
kanisubiri Terminal I uwanja wa zamani. Nataka twende kwa ndege ya
kukodi."
"Ndege ya kukodi!" Nuru hakustahamili
kuficha mshangao wake. "Kwa kweli, suala zima linanitatanisha. Kwanza,
nadhani hatuna pesa za kutosha kutuweka hotelini kwa siku tatu zaidi."
"Nani aliyesema kuwa hatuna pesa?"
Saa mbili baadaye Joram alikuwa mtaa wa Sokoine
akielekea benki ya City Drive. Mkononi alikuwa na mfuko wake mkubwa ambao
ulionekana mzito. Alipoingia benki alimfuata meneja aliyeongea nae jana ambaye
alimpokea katika hali ya kujuana. Baada ya salamu za kawaida Joram alipewa fomu
alizotakiwa kujaza. Akajaza kwa makini na kuzirejesha kwa meneja ambaye
alizipitia. Kisha alitakiwa kuonyesha mali yake aliyohitaji kuhifadhi kwa
utaratibu wa Self-Custody. Akafungua begi lake na kutoa kinyago.
"Ni hicho tu?" meneja aliuliza.
"Nilidhani una kidani cha almasi," akamjibu kwa sauti ya mzaha.
Moyoni meneja huyu aliamini kabisa kuwa ndani ya
kinyago hicho mlikuwa na kipande cha almasi au Tanzanite. Kwani hakuona sababu
nyingine ambayo ingemfanya Joram ajiingize katika gharama kubwa kwa ajili ya
kinyago cha Mmakonde mmoja.
"Hiki kina thamani kama roho yangu," Joram
alimjibu meneja.
"Ni kumbukumbu ambayo iliachwa na babu mzaa babu
ambayo inalinda ukoo wetu. Niliwahi kudhani kwamba ni utamaduni wa kipuuzi
nikakidharau, lakini yalinipata makubwa. Nusura nipoteze roho. Tangu
nimekithamini na kuwa nacho, mambo yameniendea kama ninavyotaka."
Meneja huyo alielekea kumwamini. Wakainuka na kuelekea
shimoni. Waliwapita wafanyakazi wanaotunza akaunti za watu, ambao
hawakujishughulisha kuwatazama zaidi ya ule mtazamo wa kawaida. Wakateremka
ngazi na kuingia vyumba vya chini. Ni hapo Joram alipomgusa meneja huyo bega na
kumwambia, "Sikia bwana meneja. Sihitaji kuhifadhi kinyago hiki wala kitu
kingine. Nahitaji pesa. Za kigeni."
Sauti yake ikiwa ileile, makini, iliyotulia, ikamfanya
meneja huyo kudhani kuwa huo ulikuwa utani mwingine wa Joram. Hivyo, aligeuka
akitabasamu. Lakini tabasamu lake liliyeyuka ghafla na nafasi yake kumezwa na
hofu iliyochanganyika na mshangao mara alipokutana na bastola kubwa
ikimchungulia kifuani.
"My God," aliropoka kwa hofu.
"Usiogope," Joram alimnongoneza.
"Endapo hutakuwa mbishi hutaumia. Kwanza pesa hizo sio zako. Nifunguliea
nichukue kidogo na kuondoka zangu."
"Sina ufunguo," meneja alijibu. "Zaidi
ya hayo, vitasa hivi hufunguliwa na watu wawili kwa pamoja. Sioni unavyoweza
kuzichukua." Akavuta pumzi kwa nguvu kabla ya kuongeza, "Licha ya
hayo ndugu Joram, nashindwa kuamini kama kweli unadiriki kukifanya kitendo
hicho. Unajua wewe ni mtu mwenye hadhi kubwa hapa nchini na duniani kote. Kwa
nini uichafue hadhi hiyo? Kama unataka pesa hata ungeiomba serikali ungepewa.
Hakuna asiyejua mchango wako katika kuilinda nchi hii."
"Yaelekea huufahamu ubahili wa serikali hii
wewe," Joram alimcheka. "Sasa tusipoteze muda. Mimi ninazo funguo
ambazo zinafungua kila kufuli. Sidhani kama kufuli zenu zitashindikana.
Nitakupa funguo hizo ujaribu mmoja baada ya mwingine. Nitakuwa nyuma yako
nikikutazama. Ukifanya ujinga utapoteza maisha yako.
Juhudi hizo hazikufua dafu. Ndipo alipoamua kufumua
kitasa kwa risasi. Bastola ilikuwa na kiwambo cha kupoteza sauti, na, kwa
hivyo, ulitokea mlio wa kawaida tu.
Dakika iliyofuata walikuwa ndani ya chumba cha fedha
za kigeni, Joram akiwa kamsimamia meneja ambaye aliamriwa kutoa kinyago na
kupakia mabunda ya noti za Dollars, Pounds na nyinginezo. Mfuko uliposhiba,
Joram alimwamru meneja huyo kuondoka. Aliuchukua mfuko na kumtaka atangulie.
"Tutatokea mlango wa uani na kwenda nje kupitia
geti. Bastola itakuwa mfukoni lakini tayari kuvunja mgongo endapo utafanya
ujanja au ujinga wowote. Tembea kama kawaida bila kugeuka nyuma."
Walitoka na kuelekea uwani badala ya ofisini.
Wafanyakazi wawili watatu waliwatazama kwa mshangao lakini tabasamu la Joram
liliufanya mshangao wao utoweke. Tabasamu hilohilo liliwafanya askari wa geti
wasishuku lolote kumwona meneja wao katangulia akitokea mlango ambao huutumika
kwa nadra sana.
Barabarani Joram alimtaka meneja huyo kuendelea na
safari akiifuata barabara ya Samora bila kugeuka nyuma. Meneja huyo alitembea
kwa dakika kadhaa. Aliipita Benki ya Nyumba na kuifikia barabara ya Samora.
Hapo alisimama kungoja amri nyingine. Hakusikia. Akatulia kwa muda akiogopa
kugeuka nyuma. Alipoona macho ya wapita njia yakianza kumtazama kwa maswali
ndipo alipojitahidi kugeuka nyuma. Akajikuta akiwa peke yake. Hakujua Joram
yuko wapi. Kwanza aliduwaa kwa muda. Kisha alirudiwa na fahamu, akainuka na
kuondoka mbio kurudi ofisini. "Tumeibiwa," alimwambia mfanyakazi wa
kwanza aliyekutana nae. Akaingia ofisini kwake na kuvuta king'ora cha ishara.
Dakika chache baadaye polisi waliwasili na kuanza kuuliza maswali yao.
Wakati huo Joram alikwisha badili mavazi yake na kuvaa
yale ya kizee pamoja na ndevu za bandia zilizojumuishwa na miwani kumfanya
aonekane mtu mwingine kabisa. Kadhalika alikwisha badili teksi mbili ambazo
zilimteremsha sehemu mbalimbali. Hii ya tatu alimwambia dereva, "Airport,
tafadhali. Fanya mwendo wa kuruka."
Dereva hakumwangusha.
Wakati polisi walipoanza kuweka vizuizi vya njiani,
yeye alikuwa akimaliza kumlipa bwana fedha nauli ya ndege.
*********
JIJI la Nairobi lilimraki Joram Kiango na Nuru kwa
hewa yake yenye ubaridi ambao ulikuwa kinyume kabisa cha joto waliloliacha Dar
es Salaam. Waliuacha Uwanja wa Kimataifa wa Kenyatta kwa teksi ambayo
iliwafikisha Hilton Hotel.
"Mr. and Mrs. Charles Moris," Joram
alijitambulisha katika kitabu cha wageni.
Mhudumu wa mapokezi aliwatazama kwa muda akivutiwa na
sura na maumbile yao. Kisha aliwapatia chumba kimoja Self-Contained, kama
walivyotaka. Akawakabidhi kijana mmoja ambaye aliwaongoza hadi katika chumba
chao ghorofa ya nane. Baada ya kuwafikisha aliwapa ratiba ya chakula, vinywaji
na maelekezo mengine ambayo masikioni mwa wasikilizaji wake yalikuwa kama wimbo
baada ya kuyasikia mara kwa mara. Walimkubalia yote na kumtupia maswali huku
mara kwa mara wakimuonyesha meno kulijibu tabasamu lake ambalo halikuwa na
mpaka. Kisha Joram alimfukuza kwa kumpa noti ya shilingi mia moja ambayo
ilidakwa kwa heshima zote na kupotelea mfukoni.
"Wakati wowote, ukihitaji chochote usisite
kuniita, mzee. Naitwa James," alieleza akitoka.
"Bila shaka, James".
Mara tu walipobaki peke yao, Nuru alimtupia Joram
jicho lililojaa maswali. Alipoona Joram hatamki lolote aliamua kuzungumza.
"Nadhani una mengi ya kunieleza Joram. Kila nilipojaribu kukuuliza kisa
cha safari yetu tulipokuwa angani hukupenda kunijibu."
"Sidhani kama kweli. Ulikuwa hupendi kuzungumza
mbele ya yule rubani."
"Kwa nini? Kwani kuna siri yoyote?"
"Bila shaka. Ulipokuwa uwanja wa ndege Dar es
Salaam ulikuwa umejivika mavazi ya kizee tofauti na ulivyokuwa asubuhi.
Ulipofika hapa jambo la kwanza ulilofanya ilikuwa kujibadili mavazi na kuwa
kama ulivyo. Tulipofika hapa umelipa kwa fedha za kigeni bila shaka yoyote.
Umezipata wapi? Na..."
"Alaa! Hivi sijakwambia? Kati ya pesa nyingi
tulizopata katika mfuko wa marehemu Chonde nyingi zilikuwa za kigeni,"
Joram alidakia. "Nadhani nilikuonyesha Nuru."
"Ulinionyesha. Na kwa nini umeamua kupanga kwa
jina la bandia?" Nuru aliendelea kusaili. "Na hapo watakapoomba
kuiona hati ya usafiri utawaonyesha nini?"
"Hilo lisikusumbue. Uongo sikuanza jana. Lakini sababu
kubwa iliyonishawishi kuandika jina la bandia ni hofu ya kusumbuliwa na
waandishi wa habari. Unawajua walivyo, Nuru. Mara nyingi hawana kitu cha
kuandika. Hivyo, wanapopata kijambo watakikuza ili kijae ukurasa. Umaarufu
wangu nchini Tanzania ni jambo ambalo waandishi wa Nairobi wanaweza kuliondolea
uvivu kwa haki kabisa." Akasita na kucheka kidogo. Halafu akaendelea,
"Hapana Nuru. "Tumekuja kustarehe. Tunahitaji kustarehe. Nairobi ni
mwanzo tu wa starehe zetu. Toka hapa, tutakwenda zetu London, Paris, Hong Kong,
New York na kokote ambako roho itatuita. Lazima tufurahi. Binadamu huishi mara
moja tu. Hana budi kuitumia nafasi hiyo ili akifa awe amefaidi maisha."
0 Comments