TUTARUDI NA ROHO ZETU? (09)


 ILIPOISHIA.........

Watu hao ambao walikuwa wakitafutwa kwa udi na uvumba, alfajiri iliwakuta wakiwa wamesimama mbele ya hoteli moja ndogo katika mtaa uliojaa watu waliokuwa wakijadiliana. Macho yao yaliwatazama raia hao wa makaburu waliojaa wasiwasi kwa dhihaka. Kadhalika, waliwakebehi askari na poli ambao walikuwa wakipita huku na huko katika mtaa na vichochoro huku wakiwapita bila ya kuwatupia macho. Isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote kuwashuku kwa urahisi. Pamoja na kukesha, pamoja na kuchoka kwa kazi ya kwenda hapa na pale huku wakilazimika kuua na kuua tena, bado walijitahidi kuwa katika hali ya kawaida kama raia yeyote wa kawaida katia nchi hiyo. Hali ambao ilitokana na mavazi waliyovaa pamoja na rangi yao.

Yeyote aliyewaona aliamini kuwa alikuwa akiwaona vijana wengine wa kikaburu. Hayo yalikuwa matokeo ya moja ya shughuli nyingi ambazo Joram alifanya kwa gharama kubwa sana aliposafiri hapa na pale katika miji mbalimbali. Alimpata mtaalamu ambaye aliwatengenezea ngozi za bandia zilizovaliwa usoni, mikononi na kufunika vichwa vyao kwa nywele za kizungu. Vitu hivyo ni miongoni mwa mali zake ambazo alizisafirisha kwa hila kwa kumtumia yule Mmarekani Moole.

SASA SONGA NAYO...........

Kwa ujumla Joram aliona kuwa mambo yote yalikuwa yakienda kama yalivyopangwa, ingawa kiasi yalianza ghafla kuliko alivyotegemea. Alishtuka sana jana alipoambiwa na yule kiongozi wa BOSS kwamba leo saa nne wangeilipua Dar es Salaam na miji mbalimbali ya nchi za Kiafrika kwa ile silaha yao iliyoko angani. Hivyo, hakuwa na simile tena moyoni. Ndipo alipolazimika kufanya mapenzi ya hali ya juu na Nuru akiwa na hakika kuwa anatazamwa na ule mtambo wao ambao alikwisha uona. Alifanya hivyo ili kuwapumbaza watazamaji hao. Baada ya hapo ndipo alipofanya hila kukorofisha mtambo huo. Katika kipindi hicho cha kutoonekana aliondoka na kupenyapenya kwa hila katika viochochoro hadi nyumbani kwa Moole ambako alibisha mlango na kufunguliwa na Moole mwenyewe. Alipoomba mzigo wake Moole alikanusha kabisa kwamba hakuwa amechukua mzigo wa mtu kama huyo. Lakini ngumi mbili tatu zilimfanya amwongoze ghalani ambako Joram alimvamia na kumfunga mikono na miguu, kisha akaufungua na kuchukua vile vitu muhimu tu. Akarudi haraka hadi chumbani kwake ambako, akisaidiwa na Nuru alipekuapekua na kupata ramani walizoziandaa, pesa na vitu vingine. Ni wakati Joram alipomaliza kujivisha ngozi hizo zilizomfanya aonekane kama alivyo sasa, alipoingia yule kachero wa kwanza. Hila aliyoitumia Nuru ya kujifanya kuwa alikuwa akipambana na mzungu aliyetaka kumnajisi ilimsaidia sana. Ndipo kachero huyo alipopata kile alichostahili kupata. Nao akafanya haraka kumsaidia Nuru kuvaa “Uzungu” wake na alipokamilika walivichukua vilivyokuwa muhimu na kuingia mitaani.

Wakiwa wameikariri ramani hiyo kikamilifu, kazi waliyoifanya mitaani humo ilikuwa kufuata yale majengo waliyokusudia na kutega vile vigololi vilivyopatikana kwa Chonde na kuvitegesha katika kipindi cha saa tatu kamili. Walifanya kazi hiyo kwa ukamilifu kuliko walivyotegemea. Watu wachache ambao walilazimika kupoteza maisha ni wale walioshuku jambo au kujaribu kuwazuia kufanya kazi yao. Wakiwa hawajui kuwa wanapambana na nani watu hao walikufa kwa utulivu kabisa, isipokuwa yule ambaye kifo kilimtetemesha hata akaamua kuruka dirishani kutoka ghorofa ya nne akiwa na kisu kifuani.

Sasa kazi ya kutega vigololi ikiwa imekwisha, Joram alimtazama Nuru na kumnong’oneza, “Awamu iliyobaki ni yangu peke yangu. Ni lazima niingie katika mtambo wao na kuulipua. Nikiweza kuulipua kabla ya madhara tuliyoandaa katika jiji hili kutokea litakuwa jambo jema sana. Nikishindwa, mioto itakapoanza nenda pale ambapo nimekuonyesha katika ramani ukanisubiri.”

“Hatuwezi kwenda wote?”

 “Haiwezekani. Tumelijadili hilo mara nyingi sana.” Wakakubaliana.

Kisha Joram akajiingiza miongoni mwa watu waliokuwa wakipita katika mitaa hiyo, akielekea ilikomwelekeza ramani yake. Mwendo wake ulikuwa wa haraka na uhakika, ingawa alifahamu kikamilifu ulinzi mkali uliozunguka mtambo huo. Matumaini ya kurudi yalikuwa ndoto isiyo na hakika. Hakujali. Asingejali kufa, endapo tu kifo hicho kingetokea baada ya kufanikiwa kutega mabomu yake katika mtambo huo. Aliamini kuwa Nuru asingeshindwa kurudi Tanzania katika msukosuko mkubwa utakaoutokea mji huu, saa mbili na nusu baadaye.

Nuru alimwacha Joram na kuondoka kwa hatua chache. Mara tu alipoamini kuwa asingegeuka tena kumtazama, alianza kumfuata. Hakujua kuwa yeye pia alifuatwa na watu wanne wenye silaha kali mkononi na mioyo yenye hofu na hasira dhidi yake.

MKOBA wake wenye silaha zake zote ukiwa umetulia mkononi, kwa utulivu na uhakika kama mzigo wowote ambao haukuchukua chochote cha haja, Joram alipiga hatua moja baada ya nyingine katika mitaa ya mji mkuu wa Afrika Kusini. Alipishana na wengi akiandamana na wengi wenye misafara yao.

Kitu fulani katika damu yake kilimnong’oneza kuwa anafuatwa. Hilo halikumshangaza. Tangu alipoachana na Nuru alifahamu fika kuwa angepinga ushauri wake wa kumsubiri pale alipomwelekeza hadi atakapoimaliza awamu hii ya mwisho ambayo ilikuwa ya hatari mno. Akiwa ameshangazwa na ushujaa wa msichana huyu, jinsi alivyokuwa tayari kuihatarisha roho yake kwa hiari, aliamini kabisa kuwa asingekubali kuikosa fursa hii ya mwisho, fursa ambayo endapo ingefanikiwa isingefutika katika kurasa za matukio muhimu ya kihistoria duniani.

Hivyo, hakujishughulisha kugeuka nyuma, kwa hofu ya kuwafanya makachero, ambao aliamini wamezagaa kote mitaani wakimtafuta, kumshuku. Badala yake aliendelea na safari yake huku akitafuta nafasi na wasaa ambao ungemwezesha kumtia Nuru chenga ya mwili. Hakuumaliza mtaa huo kabla fursa hiyo haijajitokeza. Katika kona ya mtaa huo Joram alikuta mahala palipokuwa na ajali ya magari matatu yaliyogongana.

Watu wengi walikuwa wamejazana kuitazama ajali hiyo. Kati yao, Joram aliweza kuona nyuso za watu wenye dalili ya ukachero na uaskari. Hakuwajali. Badala yake alijitia mmoja kati ya raia waliokuwa wakiitazama miili ya madereva wawili ambao hawakuwa na dalili ya uhai.

Aliitumia fursa hiyo kutoa kofia mfukoni na kuivaa kichwani, pamoja na kuyafunika macho yake kwa miwani ya jua. Kisha akajipenyeza katika kundi hilo na kutokea tayari akiwa amemchanganya Nuru. Hivyo, akaendelea na safari yake, mluzi mdomoni, tabasamu usoni na hadhari moyoni.

Baada ya mitaa kadhaa aliumaliza mji. Kwa mbali, aliliona jengo lenye mtambo aliokuwa akiuhitaji. Ili kuthibitisha alitumia hila kuitazama ramani yake. Hakuwa amekosea. Akaendelea na safari yake akianza kujikumbusha kwa mara nyingine hila ambazo aliziandaa ili zimwezeshe kufanikisha jukumu lililokuwa mbele yake. Hakuwa amekosea.

Akaendelea na safari yake akianza kujikumbusha kwa mara nyingine hila ambazo aliziandaa ili zimwezeshe kufanikisha jukumu lililokuwa mbele yake. Moyoni alijua kabisa kuwa alikuwa akikaribia mbele ya domo la mauti lililo wazi. Kuingia ulikuwa wajibu wake, lakini kutoka kinywani humo akiwa hai ni jambo ambalo hakuwa na hakika nalo.

Hakuogopa. Lakini kutokuogopa hakukumfanya astahimili kujikuta akitokwa na sala ndefu kimoyomoyo, jambo ambalo hakumbuki kwa mara ya mwisho alilifanya lini.

********

“Bado yuko mbele yetu mzee…” Taarifa ilimfikia Von Iron ambaye alitulia katika ofisi yake, mara kwa mara akitazama saa yake ya mkononi. “… Tufanyeje mzee? Tumuue?” sauti iliendelea.

“Nimesema mwacheni,” Von alinguruma katika walkie talkie iliyokuwa mbele yake. “Mfuateni hadi mtakapopata nafasi nzuri mumkamate. Tunamtaka hai.”

“Anaelekea kuwa anaweza kuleta madhara, mzee. Anaweza kuwa na silaha…” sauti iliendelea.

“Unataka kuniambia kuwa wanaume wanne mnashindwa kumkamata malaya mmoja tu wa Kiafrika?”

“Sivyo, mzee. Lakini…”

“Lakini nini? Mnachotakiwa kufanya ni kumleta hapa akiwa hai, ili atueleze wapi alikotorokea Joram Kiango. Mkishindwa kufanya hivyo nadhani hamtashangaa kwa lolote litakalowapateni.” Alimaliza na kufunga redio hiyo.

Taarifa ya kuonekana kwa Nuru ilimfikia nusu saa iliyopita. Fununu iliyosaidia kupatikana kwake ililetwa na mtu aliyefia hospitali baada ya kuruka dirishani kwa maumivu ya kisu. Kabla ya kukata roho mtu huyo alifaulu kutamka kuwa aliuawa na msichana wa kizungu mwenye lafudhi ya Kiafrika. Wakagundua kuwa mafanikio yote ya Joram yalitokana na hila ya kujifanya mzungu.

Ndipo wakuelekeza upelelezi kwa namna nyingine. Na haukupita muda kabla hajatiliwa mashaka msichana huyu ambaye alikuwa akitembea mitaani kwa namna ambayo si ya kawaida kwa wasichana, asubuhi kama hiyo. Mtu alimsogelea. Akamsalimu. Majibu aliyopata yaliutia kasoro uzungu wake kutokana na lafudhi. Mwingine alimkaribia.

Akajitia kukosea na kuugonga mkoba wake, kisha aliinama mbiombio kumsaidia kuuokota. Alishangazwa na wepesi wa msichana huyo katika kuuokota mkoba huo. Alimtazama vizuri zaidi. Akaona dalili ya Uzungu bandia katika uso na mwili wake. Ndipo akaandamwa, bila ya yeye kufahamu, dakika yoyote akiwa tayari kupigwa risasi, endapo Iron angeafiki…

Iron hakuwa tayari kuafikiana na makachero hao waliojaa hasira na uchu wa kumuua Nuru. Hakuafiki kwa kuwa yeye pia alijawa na uchu moyoni, uchu wa kumpata Nuru akiwa hai, uchu wa kuonja kile ambacho aliambulia kukishuhudia kwa macho tu. Ndiyo, kufa, Nuru alikuwa hana budi. Lakini angeweza kufa baadaye. Hakuiona sababu yoyote ya kufanya haraka.

“Bosi tumeamua kumnasa…” taarifa ziliendelea kumfikia.

“Mkamateni.”

Mara zikasikika purukushaniu katika chombo hicho. Zilifuatiwa na milio ya risasi tatu. Moyo wa Iron ulidunda kwa hofu. Asingevumilia endapo msafara wa risasi hizo ungeishia katika mwili wa Nuru kabla…

“Bosi amemjeruhi mtu wetu… turuhusu tummalize…”

“Nasema mleteni akiwa hai,” Iron alinguruma.

*******

Mara chombo cha mawasiliano kikazimwa. Dakika chache baadaye mlango wa ofisi ya Iron ulifunguka na kumruhusu msichana ambaye alikuwa akisukumwa kwa mitutu ya bastola nne kuingia chumbani humo huku akipepesuka. Alikuwa hai. Lakini jeraha la kisu katika mkono wake wa kulia, kuchubuka shavuni, na uvimbe usoni, vilidhihirisha kuwa aliupigania uhai wake kwa gharama kubwa.

“Ameua watu wawili,” kiongozi wa msafara huo alieleza.

“Atajuta…” lilikuwa jibu pekee la Iron.

“Amegoma katakata kuelekeza alikojificha mwenzake.”

“Ataeleza.”

Makachero hao walishangazwa kiasi na tabia hiyo mpya ya kiongozi wao. Hakuwa Von Iron waliyemfahamu. Von Iron waliyemfahamu angekuwa wa kwanza kutamka kwa ukali “ua.” Na endapo kifo kisingetokea mapema Von Iron waliyemfahamu angeshuhudia ukatili wa hali ya juu ukitendeka katika mwili wa msichana huyo jeuri aliyetisha, hasa jinsi ngozi yake ya bandia iliyobanduka hapa na pale kwa purukushani na kufanya mabaka ya ngozi yake asilia yajitokeze kwa namna ya kuchekesha na kutisha kiasi.

“Sikieni,” Von aliwaamuru. “Huyu niachieni mimi. Nitajua la kumfanya. Fanyeni hivi, endeleeni kumtafuta Joram Kiango. Mkimpata namtaka vilevile. Hai au maiti. Sawa?”

“Sawa, bosi,” waliafiki wakitoka mmojammoja, baada ya kutazamana tena kwa mshangao.

Walipobaki peke yao Von Iron alikiacha kiti chake na kumsogelea Nuru. Akamkazia macho yake makali. Mara alilazimika kuyainamisha macho hayo mara moja baada ya kuona kitu ambacho hakupata kukiona katika macho ya msichana yeyote, kitu kisichoelezeka kwa ukamilifu, kitu kama nuru ya aina yake ambacho kilifunua mapazia fulani na kuacha barabara ndefu inayoelekea kusikojulikana; kilichomfanya Joram ayaepuke macho hayo ni zile hisia za kutatanisha ambazo zilimjia ghafla zikimfanya ajihisi kama anayeifuata barabara hiyo akielekea huko ambako hakujulikana, katika dunia nyingine inayotatanisha.

“Una habari kuwa maisha yako yamo mikononi mwangu?” Von Iron aliuliza.

Hakupata jibu, jambo ambalo lilimfanya ainue tena macho na kumtazama Nuru.

Ile nuru ya kutisha aliyoiona awali katika macho hayo haikuwepo tena. Badala yake alikutana na macho yaleyale aliyoyategemea, macho aliyotamani kuyaona, macho ya msichana, yenye dalili zote za usichana. Mara akawakumbuka marehemu wazazi wake. Akakumbuka kuwa ni kitu fulani katika maumbo ya msichana mweusi kama huyu ambacho kiliwafanya waondoke duniani kwa aibu na uchungu, kitu ambacho Von alikuwa akikitamani ili akione au kukionja. Leo ilikuwa fursa ya kipekee. Atamtumia msichana huyu kumfunulia siri hiyo, kisha angemwua.

“Una habari kuwa maisha yako yamo mikononi mwangu?” alilirudia swali lake.

Bado Nuru hakumjibu. Aliendelelea kusimama paleplae alipokuwa, uchovu ukimsumbua, maumivu yakimtesa. Moyoni hasira kali ilikuwa ikichemka dhidi ya watu hawa. Hakuwa na shaka kuwa maisha yake yalikuwa ukingoni. Lakini si hilo lililomtia hasira. Hasa alisikitika kwa kule kuona kuwa amekamatwa kabla ya kazi ya mwisho kukamilika. Japo alikuwa na hakika kuwa Joram alikuwa hajakamatwa, lakini aliamini kuwa ingekuwa haki yake kushirikiana na Joram bega kwa bega katika awamu ya mwisho kama walivyofanya katika ile ya awali. Kiasi, vilevile, alikuwa akijiuliza kama hakuwa amefanya makosa kwenda kinyume cha matakwa ya Joram na kumfuata kwa siri badala ya kumsubiri kama alivyoamriwa. Alijuwa wazi kuwa ni kitendo hicho ambacho kilimtia mashakani.

Hata hivyo, hakuwa na hofu kubwa sana juu ya maisha yake. Hakuamini kuwa kifo kilikuwa karibu kiasi hicho. Mipango waliyoiandaa ilimtia hakika kuwa ingetokea fursa nzuri ambayo ingempa mwanya wa kutoroka hadi nchi jirani za mstari wa mbele. Imani hiyo ilijengeka katika moyo wake mara alipojikuta amezungukwa na askari wenye silaha, lakini wakiwa hawana dalili ya kuzitumia silaha hizo dhidi yake. Hata baada ya kutoa bastola yake na kuwaua wawili kati yao walifyatua silaha zao kwa dhamira ya kumtisha tu; akajua kuwa walimtaka hai ili wamlazimishe kutoa siri fulani. Hivyo, hata alipozidiwa nguvu, baada ya kuvamiwa na kupigwa sana, hakuwa na shaka sana.

Na hasa huyu mtu mnene anayeonekana kama kiongozi wao. Huyu ambaye tamaa ya kimwili ilikuwa wazi katika macho yake. Kosa analofanya huyu la kumtamani lingeweza kabisa kusaidia kuyaokoa maisha yake na ya Joram Kiango. Alichohitaji ni muda kidogo.

Suala hili la kupendwa au kuhitajiwa kimapenzi halikumshangaza. Kwa kweli, alilitegemea. Joram alikuwa amemfafanulia hilo pia walipokuwa wakijiandaa kuingia nchini humu. Alimweleza kwa lugha ya kishairi akisema “Katika silaha zote za mwanamke uzuri unazitangulia.” Akamweleza kinagaubaga nini la kufanya. Hata walipokuwa wakifanya mapenzi kitandani, kabla ya Joram kutumia hila ya kuharibu kile chombo chao cha kutazamia alimnong’oneza, “Tutafanya kila kitu. Najuwa wanatutazama, usione haya. Nataka tuwatie homa ili endapo watatukamata, watamani kuyashuhudia waliyoyaona kwa vitendo. Nafasi ambayo natumaini hutashindwa kuitumia.”

Haya, sasa nafasi hiyo imetokea… Nuru alijiambia kimoyomoyo. Akayainua macho yake, akayalegeza kidogo, akiruhusu tabasamu dogo. “Najua kuwa ninakufa…” alimjibu Iron kwa sauti ndogo ambayo masikioni mwa mwanaume ilitosha kuanzisha kongamano fulani baina ya mwili na damu.

Kufa huna budi! Iron alisema rohoni… utakufa kifo kibaya. Lakini itakuwa baada!... kwa mdomo alisema, “Nimesema maisha yako yamo mikononi mwangu. Vitendo vyenu vilikuwa vuya kinyama mno. Pamoja na kupokelewa vizuri katika nchi hii na kuahidiwa kuishi kwa amani na starehe, bado mmediriki kufanya mambo yasiyoeleweka. Mnapita kuua watu wasio na hatia bila sababu yoyote. Naamini huo ni ushauri wa huyu mwendawazimu uliyefuatana naye. Unafahamu alikokimbilia?”

“Sifahamu…”

“Amekutoroka,” Iron alidakia. “Amekutoroka. Bila shaka hivi sasa anajaribu kuitoroka nchi. Hafiki mbali. Dakika yoyote ataletwa hapa akiwa hai au maiti,” alimaliza akimkazia macho Nuru. Macho yake yalikumbuka alichohitaji. Akazisahau hasira zake dhidi ya Joram na kumnong’oneza Nuru kwa sauti ambayo kwake ilijaa upendo. “Suala lako ni tofauti bi mdogo. Una nafasi nzuri ya kusamehewa madhambi hayo iwapo tu… iwapo…”

Mara Iron alijikuta hajui lipi zaidi amwambie Nuru. Hakuwa hodari wa kutongoza. Ingawa alisoma riwaya nyingi za mapenzi, lakini ilikuwa vigumu sana kila alipotamani kuyaweka aliyoyasoma katika vitendo. Sababu moja kati ya nyingi zilizomfanya hadi leo awe hana mke ni hiyo ya kutojua kuwakabili wanawake wote aliowahitaji walikuwa kama wanaomdhihaki kwa kusubiri aseme nini. Wale ambao hakuwataka ndio waliojileta kwake kwa urahisi. Alipolewa hakubabaika kuwalaki. Lakini leo, kichwani akiwa hana hata tone moja la pombe, hakuona vipi ampate Nuru. Akaduwaa akimtazama.

Nuru aliuhisi unyonge huo. Akaamua kusubiri.

Nusu dakika ilipotea kabla ya Iron kujua aseme nini. Kisha alikumbuka kuwa alikuwa na akiba nzuri ya vinywaji vikali. Akafungua kabati na kutoa chupa moja ya John Walker ambayo aliimimina katika glasi. Alimkaribisha Nuru ambaye alikataa. Akaimimina tumboni mwake. Glasi ya pili ilimchangamsha. Akarudisha vifaa hivyo katika kabati na kumsogelea Nuru na kumgusa bega huku akinong’ona kwa sauti ambayo kichwani mwake alihisi imejaa mahaba. “Wewe ni msichana mzuri sana wa Kiafrika. Sijapata kumwona mwingine wa aina yako.” Mkono wake ukagusa pale ambapo ngozi ya bandia ya Uzungu aliyoivaa Nuru ilikuwa imebandukabanduka kwa purukushani. Akaishika na kuibandua. Gundi nyepesi iliyotumiwa kuiambatanisha ngozi hiyo ya nailoni na mwili iliacha mabaka meupe. Lakini nyuma ya mabaka hayo ulijitokeza uso mzuri, uso asilia wa Nuru. “Wewe ni mzuri kama ulivyo. Huhitaji kabisa ngozi hii,” Iron alisema akizidi kuzibandua ngozi sehemu za mapajani.

Sasa aliyesimama mbele yake hakuwa tena yule msichana wa Kizungu. Alikuwa msichana wa Kiafrika, msichana mzuri, ambaye kwa muda, uzuri wake ulimpumbaza kaburu Iron. Kisha tamaa ikamzidi nguvu, mikono yake ikapoteza utulivu na kuanza ziara kutambaa katika mwili wa Nuru. Mara ulimi wake ukaanza kudai njia katika kinywa cha Nuru, huku akitweta kwa nguvu na kunong’ona maneno ambayo Nuru hakuyaelewa. Hakutofautiana na sokwe mweupe aliyeonjeshwa asali. Kila kitendo cha Von kilizidisha hasira katika moyo wa Nuru. Mikono hiyo ilipoyafikia matiti yake na kuyachezea, akahisi kama aliyeguswa na kinyaa ulimi ulipokuwa ukibishana na meno yake ukitafuta mwanya wa kuingia mdomoni mwake, aliona kichefuchefu. Ambacho alitamani kufanya ni kutumia fursa hiyo kuachia pigo ambalo lingeondoa uhai kisha kutafuta fursa ya kutoroka. Hata hivyo, hakuthubutu kufanya hivyo kwa kuchelea kuharibu mambo. Hakukoma kuitazama saa kubwa iliyokuwa ukutani. Kila dakika iliyopita alikuwa akisheherekea kimoyomoyo. Sasa ilikuwa imebaki kama saa moja tu kabla ya mitego waliyoitega kufyatuka. Wakati huo asingekosa mwanya wa kutoroka. Kabla ya hapo alihitaji kuubembeleza muda kwa bei yoyote, isingemgharimu chochote kuendelea kuliruhusu jitu nene liendelee kujipumbaza katika mwili wake. Mara moja mbili akaguna na kutetemeka kwa namna ya kumfanya aonekane kama aliyeshikwa na ashiki.

Kitendo hicho kilichochea wazimu wa Iron. Mara akapambua mavazi ya Nuru. Mikono yake iliyokuwa ikitetetemeka iligombana na vifungo vya mavazi huku akizidi kunong’ona hili na lile. “Sikiliza…” Nuru alimweleza akiushika mkono wake na kuutoa mapajani mwake huku akimfinyafinya. “Hapa ni ofisini. Mtu yeyote anaweza kuingia…”

“Hii ni ofisi yangu,” Von alikoroma. “Hamna anayeweza kuingia bila ruhusa yangu.”

“Sio vizuri.”

“Tafadhali…” kisha Von alijilaumu kwa kutamka neno hilo. Vipi amtafadhalishe mtu mweusi? Zaidi, mtu ambaye roho yake iko katika mikono yake. Akaupeleka mkono wake wa pili katikati ya mapaja ya Nuru kwa nguvu kidogo. Nuru aliyabana mapaja yake. Ni hapo Von alipokumbuka kuwa isingekuwa kazi ndogo kumtenda msichana huyu bila hiari. Hakuwa amezisahau zile picha za sinema ambazo huonyesha jasho linavyowatoka watu wanaojaribu kunajisi. Wala asingesahau yaliyosemwa katika kile kitabu cha mapenzi alichowahi kusoma, “… hicho ni kitu pekee ambacho mwanamke ana mamlaka nacho… kitu pekee anachoweza kujivunia… rasilimali yake pekee…” hivyo, akajikuta akilazimika kutumia njia nyingine. “Una habari kuwa maisha yako yamo mikononi mwangu? Dakika yoyote nitakayosema ufe utakuwa marehemu. Najaribu kukuokoa kwa kuwa sioni kama unastahili kufa mapema kiasi hiki,” alimweleza Nuru.

“Nitajuaje kama hunidanganyi? Nitajuaje kama baada ya kumaliza shida zako hutaniua?” Nuru alisema akimlegezea macho.

“Nakuhakikishia kuwa utakwenda zako kwa amani na furaha kokote unakotaka kwenda.” Von alipoona hajaaminika kikamilifu alimwacha Nuru kwa muda na kuliendea kabati ambalo alilifungua na kutoa bahasha kubwa. Ndani ya bahasha hiyo mlikuwa na pesa nyingi za nchi mbalimbali. “Hizi ni pesa zenu. Ni miongoni mwa vitu vyenu mlivyonyang’anywa mlipofika hapa. Sasa hivi nakukabidhi pesa hizi ukae nazo ili utakapoondoka zako ukaishi popote unapotaka.” Alimpa Nuru na kuziweka katika mfuko wake. Alikuwa akicheka kimoyomoyo akifahamu kuwa mara baada ya kuimaliza hamu yake na kumwua Nuru angezirejesha fedha hizo katika himaya yake. “Sasa tunaweza kuendelea,” alisema akianza upya kuchezea mwili wa Nuru.

Nuru hakumzuia mara moja. Alikuwa hajafahamu atumie hila ipi kumchelewesha tena. Safari hiyo kilichomwokoa Nuru ni king’ora kilichotoa mlio wa aina ya paka aliyekabwa koo katika moja ya mitambo ya Von. Sauti hiyo ilimfanya Von aruke hadi kwenye simu ambako aliichukua na kusikiliza kwa makini. Sauti nyembamba ilisema kwa wasiwasi, “Bosi, inaelekea kuna jambo la hatari katika mtambo maalumu. King’ora cha hadhari kimekuwa kikilia kwa muda mrefu. Simu za walinzi wetu huko hazipokelewi.”

“Impossible,” Von alifoka. “Unataka kuniambia kuwa maafa yanayotokea mjini yanaweza kuhamia huko nje ya mji?”

“Inaelekea, mzee. Kwa sababu huyu mtu anayeitwa Joram haelezeki. Aweza kuwa huko sasa hivi.”

“Impossible,” alifoka tena. “Na kama kweli kaenda huko, basi kajipeleka mwenyewe kaburini.” Von alisita kidogo. Kisha aliongeza, “Sikia. Andaa helikopta yangu na dereva. Nataka kufika huko mara moja. Nataka kushuhudia kwa macho yangu mwenyewe mtu huyo anayejiita Joram Kiango anavyosulubiwa.

***

Huko angani Nuru aliziona vizuri kabisa maiti nne za askari wa Makaburu zilizovalia magwanda na silaha zao mikononi. Zilikuwa zimelala sakafuni mbele ya lango kubwa la chuma ambalo lilizunguka ua wa seng’enge uliozunguka jumba kubwa. Helikopta ililizunguka jengo hilo mara tatu, Von akitazama kwa darubini huku na kule. Aliporidhika alimwamuru rubani kutua kando ya ua huo katika kichaka kilichoutenga mtambo huo na mji.

Kutoka mjini hadi hapa, ilikuwa safari ya dakika mbili tatu tu. Kabla ya kuanza safari hiyo Von alitupiana maneno makali na msaidizi wake ambaye alishangazwa na uamuzi wa Von kumpeleka Nuru huko. Alimwambia, “Sikubali kabisa. Nadhani ni wewe mwenyewe uliyeweka sharia ya kupigwa risasi mtu yeyote atakayekaribia mtambo ule, awe raia wa nchi au mgeni. Vipi aende huyu ambaye tunamhisi kuwa ni mwenzi wake ambaye amefika huko kufanya mashambulizi?”

“Huyu ni mateka wangu,” Von alimjibu. “Bado nina mengi ya kumsaili. Zaidi ya hayo, kama kweli Joram yuko huko tutamtumia huyu kumfanya Joram asithubutu kuendelea na chochote anachoota kichwani mwake.”

“Bado sikubali,” msaidizi huyo alieleza. “Nimeandaa kikosi cha askari wanne ambao ungefuatana nao huko. Kadhalika, nilikuwa nikisubiri amri yako ili nitumie askari wengine hamsini kwa gari. Inaelekea yote niliyofanya ni bure.”

“Ni bure kabisa,” Von alimjibu. “Unajua kabisa kuwa mtambo ule unalindwa katika hali isiyo na shaka kabisa. Hata kama atafanikiwa kuingia ndani hawezi kabisa kufanya madhara yoyote. Baada ya juhudi zake zote ataambulia kufa tu. Hivyo, nakushauri urudi na hao askari wako uliowaandaa. Nitakwenda mimi, huyu mateka na dereva tu. Sawa?”

Msaidizi huyo alimtazama Von kwa hasira ya mshangao. Alizithamini sana hekima zake katika masuala yote ya kiusalama katika nchi hii miaka yote aliyokuwa naye. Lakini vitendo vyake saa chache zilizopita vilimchanganya kabisa. Vilikuwa vitendo ambavyo havikubaliki. Yeye, kama mtu wa pili katika usalama wa utawala huu, hakuona kama alistahili kumtii Von hata kwa hilo. Hivyo, alimtupia jicho la hasira na kumwambia, “Kwa mara ya kwanza nitafanya kinyume cha matakwa yako.”

“Na kwa mara ya kwanza nakuambia kuwa… kuwa… hufai kufanya kazi chini yangu. Baada ya suala hili nitaangalia suala lako,” Von alisema akimsukumiza Nuru katika helikopta na kumwamuru rubani kuondoka.

Hata hivyo, rohoni alikuwa na mashaka kwa uamuzi wake huu. Alijua kabisa kuwa alikuwa akifanya kosa kubwa kufuatana na Nuru huko aendako. Hata hivyo, alifahamu fika kuwa hii ilikuwa nafasi yake pekee ya kufanya naye mapenzi na baadaye kumwua. Kimojawapo cha vyumba kadhaa katika jengo la mtambo huu kilikuwa chumba maalumu cha faraja kwa ajili yake na wakubwa wachache sana. Chumba hicho kilikuwa na mitambo ya televisheni, ambayo ilitumia nguvu ya setilaiti yao hiyo iliyoko angani kuitazama miji mbalimbali ya Afrika kinaganaga. Vilevile kulikuwa na chombo maalumu ambacho kinaweza kutazama shughuli zote zinazofanyika katika chumba hicho. Mara kwa mara Von hujifungia humo na kutazama utendaji kazi wahandisi bila ya wao kuwa na habari. Mhandisi mmoja aliwahi kupoteza kazi na maisha yake baada ya kushukiwa na Von kuwa alikuwa na dhamira mbaya kwa mtambo huu. Hivyo, kifo chake machoni mwa watu wengi kilionekana kama ajali tu iliyosababishwa na dereva mlevi kugonga mtu anayetembea kando ya barabara katika mitaa ya Johanesburg. Leo Von alitegemea kukitumia chumba hicho kujistarehesha na mwili wa Nuru kabla ya kutulia na kuanza kuangalia kwa furaha watu wanavyoteketea kwa moto katika miji ya Dar es Salaam, Lagos, Lusaka, Harare na kwingineko.

Furaha iliyokuwa ikichemka katika fikra za Von iliingia nyongo mara baada ya helikopta yake kupita juu ya jengo hilo na kushuhudia walinzi wake walivyolala ovyo wakiwa maiti. Hivyo, akamtupia Nuru jicho la chuki. Tamaa aliyokuwanayo dhidi yake ilianza kuyeyuka na nafasi yake kuchukuliwa na hasira kali. Alitamani ammalize papo hapo na kuyasahau yote aliyokuwa akiyawaza juu yake. Hata hivyo, wazo jingine lilimjia akilini. Nuru alionekana katili sana ambaye haogopi kifo kama wanawake wengine anaowafahamu. Hata hivyo, anaweza kufa baada ya kutaabika sana. Hakuna mateso ambayo yatamtaabisha zaidi ya kushuhudia kifo cha mpenzi wake, Joram Kiango. Akiwa na hakika kabisa kuwa Joram alikuwa maala fulani katika jengo hilo akifa au kusubiri kifo, Von alitoa bastola yake na kuigongagonga katika kisogo cha Nuru. “Twende,” alimwamuru, baada ya kumtaka rubani asubiri katika helikopta.

Nuru alitelemka na kufuata maelekezo ya Von. Waliipita miili ya marehemu waliolala ovyo, damu ikivuja kutoka katika majeraha ya risasi miilini mwao.

Von alimshangaa Joram, peke yake, aliwezaje kuwaangamiza askari wengi kiasi hicho bila wao kufanya lolote. Lakini haikumshangaza Nuru hata kidogo. Wala Nuru hakuhitaji kusimuliwa. Akiwa mtu anayemfahamu Joram na hila zake nyingi alijua kuwa alitumia njia moja au nyingine kuwafikia askari hao waliojiamini kwa silaha zao aina ya machine gun. Baada ya hapo alitoa hati zake za bandia kuwaonyesha askari hao, hati ambazo zilifungwa kinamna kiasi cha kuhifadhi hewa ya sumu ambayo, bila shaka, iliwafanya askari kulewa ghafla na hivyo, kuwaua mmoja baada ya mwingine haikuwa kazi ngumu.

Kilichomshangaza Nuru ni kutofahamu Joram alikuwa akifanya nini muda wote huo katika eneo la hatari kama hilo. Alikadiria kuwa dakika tano zingetosha kabisa kuuteketeza mtambo huo na kutoweka. Na kwa mujibu wa ramani yao ndani ya kiwanda hicho hamkuwa na ulinzi wowote zaidi. Vipi asitokee na kummaliza mtu huyu mnene ili waondoke zao?

Von hakumpa nafasi ya kuwaza zaidi. Alikuwa akimsumbua mbele kwa mtutu wa bastola yake harakaharaka. Nuru hakuwa mzito wa kuelewa kuwa Von alikuwa akimtangulia kwa dhamira ya kumfanya ngao endapo lolote lingetukia kinyume na mategemeo yake.

Baada ya kukagua vyumba mbalimbali wakafika katika chumba cha Von. Ukiondoa makochi na kabati lililojengwa ukutani chumba hicho hakikutofautiana na maabara au studio ya aina yake machoni mwa Nuru. Mashine na mitambo mingi ilikuwa imepangwa kwa tafsiri fulani, kuta zikiwa screen zilizopangwa katika hali ya kupokea habari mbalimbali. Von aliisogelea mashine moja ambayo machoni mwa Nuru ilikuwa kama kompyuta na kubonyeza swichi ainaaina. Kioo katika ukuta mmoja kilipata uhai na kuanza kuonyesha mambo ya ajabuajabu. Baada ya hali kutulia Nuru aliona kuwa walikuwa wakitazama chumba baada ya chumba katika jengo hilo. Kilitokea chumba ambacho kilikuwa na mitambo mingi ya kutisha. Chumbani humo Nuru aliwaona wahandisi watatu waliokuwa makini wakichapa kazi ya kuongoza mitambo bila dalili yoyote kuwa mambo yanakwenda mrama. Hilo lilimfurahisha sana Von. Akaangua kicheko kwa furaha. Ni yeye aliyependekeza kuwa kwa usalama wa mitambo ishara za hatari zisiwafikie wahandisi hao, wasije wakapata hofu na kusababisha setilaiti iliyoko angani kukosa uongozi wa ardhini, jambo ambalo lingeweza kusababisha maafa na hasara isiyokadirika. Kwa jinsi jengo hilo lilivyoandaliwa Von alikuwa na hakika kabisa kuwa ingemhitaji binadamu mwenye moyo wa malaika kuwafikia wahandisi hao na kuuharibu mtambo huo. Joram hakuwa na moyo huo. Ni hilo lililomtia nguvu. Sasa ameamini kuwa hakukosea. Kwa muda, aliwatazama wahandisi hao wanavyoshughulikia. Wakijua kuwa leo ilikuwa siku ya kazi kubwa walifanya kila kitu kwa juhudi na umakini wa hali ya juu. Kisha Von alibonyeza sehemu nyingine. Chumba hicho kikahama na vyumba vingine kuanza kupita katika kioo.

“Nataka tumwone mpenzi wako anavyokufa au alipofia,” alimweleza, tabasamu la kifedhuli likiyasindikiza maneno yake. “Keti tafadhali. Keti ili uone kwa starehe.”

KIOO kilionyesha vyumba mbalimbali ambavyo vilijitokeza na kupita. Kila chumba kilikuwa na vitu mbalimbali vilivyoyavuta macho ya Nuru. Lakini ilielekea kuwa havikuwa vyumba Von alivyovihitaji. Aliuendesha mtambo huo harakaharaka kwa kubonyeza kidude hiki na kile kama karani anayepiga chapa. Mara kilitokea chumba ambacho Von alikuwa akikitafuta. Katika chumba hicho, ambacho kilionekana kidogo, walikuwemo watu wawili waliokuwa wakipigana. Mmoja hakuwa mtu bali jitu. Lilikuwa pande la mwanamume, refu, nene, jeusi lenye magumi manene na macho ya kutisha. Lilikuwa likipigana kwa maguvu yote katika hali ambayo ilionyesha kuwa lilikusudia kuua kwa mikono. Jitu hili halikuwa na dalili yoyote ya uchovu wala maumivu yoyote. Kinyume kabisa cha mtu wa pili ambaye lilikuwa likipambana naye. Huyu alikuwa kijana wa kizungu, mwenye dalili zote za ushujaa na ufundi wa kupigana ngumi na karate. Lakini ufundi wake haukuwa na dalili yoyote ya kuonyesha kulishinda jitu hili kwani tayari kijana huyo alikuwa akivuja damu hapa na pale katika majeraha ya kutisha, huku akiwa na dalili za uchovu mkubwa.

ITAENDELEA..............


Post a Comment

0 Comments