ILIPOISHIA............
Hayo yalisemwa baada ya watu kuwatazama Joram na Nuru wakitoka katika ndege iliyowaleta, huku wakiwa wametanguliwa na rubani ambaye walikuwa wamemshikia bastola. Nje ya ndege Joram aliitupa chini bastola yake na kuweka mikono yake juu. Ndipo Polisi wa makaburu ambao walikuwa wameuzingira uwanja wakiwasubiri, wakajitokeza na kuwakimbilia.
Wakawavamia na kuwakagua
harakaharaka. Walipoona kuwa hawana silaha nyingine wakawaongoza kuliendea gari
lililokuwa likisubiri. Muda wote huo kamera za televisheni na zile za wapiga
picha wa magazeti ziliwaelekea Joram na Nuru kwa ukamilifu. Kama kuna chochote
kilichowashangaza watazamaji ni jinsi sura za vijana hawa zilivyoonekana
tulivu, nzuri, zisizo na dalili zozote za ugangwe kama walivyotegemea.
Msafara wa gari uliishia katika jumba moja kubwa lenye
ghorofa kadhaa. Humo, badala ya lifti waliyoingia kuwapandisha juu
iliwateremsha chini ambako walijikuta katika chumba kilichoelekea kuwa maalumu
kwa kuhoji mateka. Askari waliokuwa nao waliamuru kusubiri, kisha wakatoka na
kuufunga mlango nyuma yao. Baada ya muda waliletewa chakula na vinywaji. Wakala
na kunywa.
SASA SONGA NAYO....................
Baada ya muda, kama walivyotegemea, walianza
kutembelewa na maafisa wa upelelezi, ambao waliuliza maswali kemkem. Maswali
yote waliyajibu kwa ukamilifu kama walivyojiandaa; kwamba walikuwa wameishiwa
na hila za kuwaepuka INTERPOL wakaona hawana njia nyingine zaidi ya kukimbilia
huku ambako wangehitaji hifadhi.
Baada ya maswali yalifuata mawaidha na badala ya
mawaidha ikawa kashfa. "Wewe kama Joram Kiango ambaye nchi yako na Afrika
nzima ilikutegemea huoni aibu kufanya ulivyofanya na kuja huku?" aliulizwa
"...Utajisikiaje utakapolazimika kufuata matakwa
yote ya ubaguzi na kulazimika kushuhudia Waafrika wanavyonyanyaswa?"
"...Unaweza kukiri hadharani kuwa viongozi wote
wa Afrika ni wadanganyifu na hawajui watendalo?"
"...Ukipewa bastola ili umuue mpigania uhuru
yeyote atakayematwa, utafanyaje?"
"...Huyu msichana na uzuri wake wote ni malaya?
Mbona anakubali kuandamana na mwizi?"
Yalisemwa mengi zaidi ya hayo. Yako ambayo Joram
alijibu kwa namna ambavyo alijua walimtegemea kujibu. Mengine hakuyajibu,
akijua kuwa walimtegemea kutojibu. Mengine ilimlazimu kuinama kwa haya akiwa na
hakika kwamba walitarajia aone aibu. Baadhi ya maswali aliyakwepa kijanja
akijua ni mitego iliyokusudiwa kumnasa.
Kutoka hapo walipelekwa katika chumba kilichokuwa na
mitambo mingi ambayo eti ingeonyesha kama walikuwa wakisema ukweli au la.
Waliwekwa katika mitambo hiyo na kuanza kuulizwa tena maswali. Yote hayo Joram
alikwishamfafanulia Nuru kabla hawajaondoka Paris kuja Kinshasa, Zaire, ambako
waliiteka nyara ndege ile ya kukodi. Alimweleza kuwa ambacho mtambo kama huo
unaweza kuonyesha ni dalili za moyo kudunda na damu kuchemka mara unapoulizwa
swali ambalo litakushtua au unapobuni uongo. Hivyo, endapo utazungumza kwa
kujiamini haitaonekana dalili yoyote.
Ndivyo ilivyotukia. Saa chache baadaye walichukukuliwa
na gari kutoka katika chumba hicho na kupelekwa katikati ya mji ambako
waliingizwa katika nyumba moja kubwa na kuelekezwa katika chumba kilichokuwa na
vitanda viwili. Humo walikuta mizigo yao yote. Ingawa mizigo yao ilikuwa kama
ilivyokuwa, lakini Joram hakusita kugundua kuwa tayari ilikuwa imekaguliwa kwa
ukamilifu. Hilo alilithibitisha baada ya kufungua na kukuta kila kitu kimo
isipokuwa furushi la pesa zilizokuwa zimesalia. Hilo pia alilitegemea. Hivyo,
hakubabaika. Akamwendea Nuru na kumvuta mkono akimwelekeza kitandani ambako
alimketisha ili ampumzike kidogo.
"Pole,” alimwambia.
"Kwa?"
"Usumbufu."
"Mbona bado sijasumbuka. Naamini huu ni mwanzo
tu, kuna mengi yanayokuja na nitakuwa tayari kuyakabili yote..."
"Shii," Joram alimnyamazisha. “Usijisikie
huru kiasi hicho," alinong'ona. "Bado tuko chini ya ulinzi mkali.
Yawezekana wanatutazama na kutusikiliza. Kiswahili si lugha ngumu kiasi hicho.
Endelea kujihadhari."
Moyoni Joram alikuwa na sherehe kubwa. Alikuwa
akishangilia mafanikio ya msafara huo ambao ulienda kama alivyokusudia kuelekea
kuzaa matunda. Kufika Afrika Kusini na kupata mapokezi yenye hadhi kwa kiwango
hiki ilikuwa jambo pekee la pili ambalo alilihitaji sana. Jambo la awali ambalo
alihakikisha limefanikiwa kabla hajabandua mguu wakekuiacha dunia huru na
kujitosa jehanamu kiasi hiki ilikuwa kulisafirisha sanduku lake ambalo lilikuwa
na kila kitu alichohitaji katika jukumu lililokuwa mbele yake. Kati ya vitu
vilivyokuwemo ni pamoja na pesa za matumizi muhimu, silaha aina aina, madawa ya
kila aina, ramani mbalimbali, ngozi na sura za bandia ambazo zingemfanya
aonekane mtu mweupe, na zaidi ya yote ni vile vijigololi maalumu ambavyo
alivipata kutoka kwa hayati Chonde.
Ilikuwa imemgharimu uongo mkubwa na pesa kuweza
kulifikisha sanduku lile katika nchi hii. Alikuwa ametumia hila za kumwendea
mfanyabiashara wa Kimarekani ambaye alikuwa akisafirisha mizigo yake moja kwa
moja kutoka Ufaransa. Baada ya kujijenga kwake kwa urafiki bandia alimhadaa kuwa
amepata oda ya kuuza madawa ya kulevya nchini Afrika Kusini. Mmarekani huyo
alikataa kabisa kujihusisha kwa hali yoyote katika biashara ya aina hiyo. Joram
alikazimika kumpigia magoti kwa maneno huku akimpa pesa nyingi na kumwahidi
sehemu kubwa ya faida. Ndipo sanduku hilo liliposafiri pamoja na mizigo mingine
muhimu ya Joram. Na aliarifiwa kuwa sanduku hilo limefika salama. Ilimpendeza
sana Joram kuona kati ya watu wengi waliokuja kiwanjani kushuhudia wateka nyara
hao wakitelemka kutoka ndani ya ndege, mmoja wao alikuwa Mmarekani huyo
aliyeitwa Moore. Ilimpendeza zaidi kuwa Moore hakuweza kufahamu kuwa mteka
nyara huyo ndiye yule aliyekuwa rafiki yake siku tatu zilizopita nchini
Ufaransa. Joram akiwa amekariri ramani ya nyumba ya Moore kama anavyovifahamu viganja
vyake vya mkono, alikuwa akiisubiri kwa kiu kibwa fursa ya kuweka mikononi
mwake mizigo yake.
Kabla ya kuoga kama alivyohitaji kufanya, Joram
alijitia shughuli na kufanya kama anayepanga vitu chumbani kwake vizuri.
Alichokuwa akifanya hasa ni kitu au vitu fulani na haukupita muda kabla ya
kukiona alichokuwa akitafuta. Kipande kidogo sana cha kioo kilichokuwa
kimejitokeza sakafuni katika pembe moja ya chumba kama kilichosahauriwa na
waashi kwa bahati mbaya. Joram alijua kuwa nyuma yake kipande hicho kulikuwa na
nyaya ambazo zilisafiri hadi kwenye mtambo ambao ulikuwa na jukumu la
kupeperusha kila wanachoongea au hata kuwaona. Baada ya kuona hayo Joram
alilidhika, akijua kuwa alikuwa hana haraka ya kuwa msiri. Alihitaji faragha
kwa usiku mmoja tu, na katika usiku huo alijua ambacho angefanya kuufanya
mtambo huo ushindwe kuwajibika kwa dakika kadhaa.
Wakaoga.
Wakalala.
Jasho jembamba lilikuwa likiwatoka maofisa wanne wa
Boss ambao walikuwa katika chumba fulani wakiwashuhudia Joram na Nuru
walipokuwa wakifanya mapenzi katika chumba chao. Maofisa hao walikuwa wamekaa
katika chumba hicho kwa muda mrefu, dhamira yao kuu ikiwa kupata hakika kama
kweli Joram alikuwa hana hila nyingine iliyomleta Afrika Kusini zaidi ya
ukimbizi. Taarifa za maofisa wote waliotumwa kuwahoji na ambao walikagua mizigo
yao haikuonyesha hila wala ila yoyote. Hata hivyo upinzani uliokuwepo uliishia
kuamuliwa kuwa wapewe chumba hiki na kuachiwa uhuru kiasi fulani ili waendelee
kuchunguzwa. Chumba hiki kilikuwa maalumu na siri kubwa isipokuwa kwa maofisa
wachache wa ngazi za juu. Ndipo jukumu la kuwatazama Joram na Nuru
likawaangukia kaburu Von Iron na wenzake.
Ndipo walipolazimika kutokwa na jasho. Kwani walikuwa
wakitazama kwa namna moja ilikuwa kama picha ya kupendeza sana, kwa maaana nyingine
picha ya kuchukiza, inayotesa na kuadhibu.
Ilikuwa picha ya kupendeza wakati walipokuwa
wakiwatazama Joram na mpenzi wake Nuru walipokuwa wakitazamana kwa mapenzi
pindi wakati wakijiandaa kulala. Ikaanza kuchukiza walipoanza kuvua mavazi yao
na kuketi kama walivyozaliwa huku wakibusiana. Na ilianza kutesa walipojibwaga
kitandani na kufanya mapenzi kiroho mbaya bila kujali au kujua kama
wanatazamwa, kana kwamba walikuwa wakiwaonyesha watazamani kwa makusudi.
Von Iron aliuzima mtambo huo na kulifuta jasho
lililokuwa katika paji lake la uso. Hakujiamini kuwatazama wenzake machoni,
akihofu wasije wakasoma kitu alichokuwa akikisoma akilini. "Tukutane
kesho..." Von aliamuru akianza kutoka nje. Bila kuinua macho aliweza
kuhisi kuwa wenzake walikuwa wakimhurumia zaidi ya walivyokuwa wakijihurumia
wao. Alijua vilevile kuwa wenzake hao walijua kama alivyojua yeye kuwa baada ya
kuagana nao angerudi katika chumba hicho.
Alirudi.
Akiwa peke yake aliwatazama kwa makini na uhuru zaidi,
akisherehekea kila hatua iliyofuata katika mapenzi yaliyokuwa yakiendelea
mtindo mmoja juu ya kitanda. Tangu alipokuwa amewaona Nuru na Joram katika
televisheni hajua kuwa wangeweza kuwa wazuri kiasi hiki. Kadhalika hakutegemea
kuwa Mwafrika aliyevua nguo angeweza kuwa kiumbe mzuri kama hawa, aliwategemea
kuwa viumbe wa kutisha sana kama mizimu. Kumbe sivyo.
Aliendelea kuwatazama. Alijipinda na kujinyoosha kwa
maumivu na tamaa kubwa huku mkono wake mmoja akiubembeleza uume wake, mkono
wake wa pili ukiwa umelea kichwa kwa wivu wa masikitiko. Starehe au mateso yake
yalikoma Joram alipozima taa.
Von alijifariji kwa kuizima mitambo hiyo na kubonyeza
ile ambayo ilimfanya akague ulinzi na usalama wa ule mtambo wa nyuklia
unaoendesha Satilaiti maalumu iliyoko angani ikisubiri kufanya kazi ambayo
haitafutika katika kurasa za historia ya dunia. Aliuona ulinzi ulivyokuwa
makini. Askari wanne wenye machine guns walikuwa wakipita kwa zamu kulikagua
jengo hilo. Ndani mafunzi wenye silaha walikuwa machio wakikagua mwenendo wa
mtambo huo kwa umakini na uangalifu mkubwa. Von aliweza kuona katika screen
kubwa iliyokuwa mbele ya wanasayansi hao jinsi setileiti hiyo ilivyokuwa
ikielea huku na huko katika bahari ya Hindi kando ya pwani ya Afrika Mashariki.
Alitabasamu kidogo alipojikumbusha utaalamu wa hali ya juu uliotumika katika
kuunda chombo hicho hata kisiweze kuonekana kwa macho ya kawaida.
Kisha alibonyeza mahali fulani kuondoa mtambo huo
machoni kwake. Badala yake alibonyeza mahali ambapo palimwezesha kuona gereza
la ardhini ambamo kulikuwa na mateka au wafungwa ambao walitakiwa kuteswa hadi
kufa. Humo kulikuwa na kila aina ya mateso. Haikuwepo njia yoyote ya kuweza
kutoka isipokuwa kwa funguo maalumu ambazo alidhihifadhi yeye mwenyewe. Von
aliwatazama wafungwa au mateka hao waliokuwa wakikaribia kufa. Baadhi yao
walikuwa weupe, Mmarekani mmoja ambaye alikuwa mpumbavu kiasi cha kuamua
kuwasaidia wapigania haki wa Afrika Kusini, pia walikuwepo Warusi wawili ambao
pia tabia zao hazikuwa tofauti na mzungu huyo pamoja na watu weusi watatu. Ni
hawa watu weusi ambao walimfanya Von aangue kicheko kwa sauti. Alijiuliza
walikuwa wamepatwa na nini weusi hawa hata wakathubutu kujileta wenyewe huku
kama wapumbavu. Mtu atajipeleka jehanamu na kutegemea atatoka salama?
Zimesikika habari nyingi za watu ambao waliwahi kufa
na baada ya siku kadhaa kufufuka. Watu hao hudai kuwa walipokuwa wafu wamefika
peponi na kuwaona malaika. Haijawa kutokea hata mtu mmoja ambaye aliwahi kwenda
jehanamu na akarudi duniani. Hawa weusi aliwaona kama watu walipenda sana kufa
vifo vya kikatili. Jambo la kusikitisha kwao ni kwamba BOSS iliarifiwa tangu
walipoondoka Naijeria na Tanzania na kuja Botswana. Iliarifiwa pia walipoanza
mbibu za kuvuka mpaka. Hivyo hila zao za mmoja kujifanya wendawazimu asiyejua
analofanya na mwingine kujitia mkimbizi anayeishi kambi ya wapigania uhuru
hazikuwa na mafanikio yoyote. Von hakupenda kuwaona ana kwa ana. Aliamua
wafungiwe katika chumba cha mauti wasubiri kifo. Hawa walikuwa wawili tu kati
ya wanane ambao walikuwa wamekamatwa siku mbili zilizopita. Wawili walikuwa
wameuawa kwa mateso wakati wakihojiwa. Mmoja alikuwa amejiua mwenyewe kwa sumu
baada ya kumvamia askari aliyekuwa akimhoji na kumjeruhi vibaya kwa kisu kabla
hajameza vidonge ambavyo vilimuua mwenyewe.
Wapelelezi hawa walikuwa ni matokeo ya juhudi za
kuthibitisha uwezekano wa kuwepo kwa mtambo maalumu unaoziadhibu nchi za
Kiafrika. Von alifahamu kuwa bado wangekuja wengi zaidi, weupe kwa weusi,
lakini kamwe wasingefika popote pa haja. Na kamwe wasingefika popote kwani
zilikuwa zimesalia siku mbili tu kabla ya Afrika huru kuipigia magoti Afrika
Kusini na kusubiri vilio na maombolezo yasiyo na mfano. Von alicheka tena,
safari hii kwa kujipongeza akijua kuwa sifa ndogo kuwa na wadhifa kama aliokuwa
nao sasa. Roho za watu wengi kuwa mikononi mwako zikisubiri tamko lako kabla ya
kuteketezwa!
Kisha Von aliufunga mtambo huo na kurudi nyumbani
kwake. Akiwa kapera ambaye hakujua lini angeoa alijikuta akikosa usingizi
alijikuta akimfikiria Nuru na kumwonea Joram wivu. Bila kufahamu anachokifanya
Von alijikuta akiapa kwa jina la Mungu kuwa asingekufa kabla hajamuonja.
"Mara moja tu..." alijiambia. "Nione wana nini wanawake
weusi..."
Kesho yake aliamuru Joram na Nuru waletwe katika ofisi
yake. Akiwa amezungukwa na wasaidizi wake Von alijitahidi kuwatazama Joram na Nuru
kwa namna tofauti kabisa na ile iliyokuwa ikipita katika akili yake.
"Sina haja ya kuwahoji chochote", Von
aliwaambia kwa sauti nzito. "Kwa kiasi mlichohojiwa naamini mmeonyesha
kuwa mmechoshwa na upuuzi wa hawa viongozi wanaojiita wanamapinduzi katika nchi
zenu. Sivyo?"
"Kwa maana hiyo mngependa kuishi huku daima.
Msimamo wenu ni wa kishujaa. Nawapenda watu shujaa. Ni hilo ambalo limenisukuma
kuwaacha hai pamoja na kuwapa heshima ya kuwaita hapa ili niwape habari
njema".
Joram akiwa amesimama mbele yake, akiwa kamshika Nuru
mkono, hakuwa na haja ya kuambiwa huyu ni nani katika nchi hii. Alimfahamu mara
moja kuwa alikuwa mkuu wa shirika la kijasusi la utawala huu. Kwa maana
nyingine alikuwa adui yake namba moja. Mtu ambaye asingeondoka bila kumpa adhabu
ya risasi ya kichwa kwa hatia ya kusababisha maafa kwa Waafrika wengi wasio na
hatia. Hata hivyo Joram hakuonyesha dalili yoyote katika macho yake alipouliza
kwa upole, "Habari njema ipi? Tumeruhusiwa kupewa uhuru zaidi ya huu
tulionao? Tunajiona kama ndio tuko kifungoni".
"Mko huru kuliko mnavyostahili", Von
alimjibu Joram. "Habari njema niliyotaka kuwapeni ni juu ya uhalibifu
ambao utazitokea nchi za Kiafrika kesho saa nne mchana endapo hawatawatuma
viongozi wao hapa leo kuweka saini mikataba ya kuwa watiifu kwa utawala huu na
kutothubutu kuwasaidia wendawazimu wanaodai uhuru wa Namibia na haki hapa
Afrika Kusini. Kama hawatafanya hivyo hadi saa tatu na nusu za mchana. Nyie
mtapewa heshima ya kushuhudia moja kwa moja Ikulu zinavyoungua, majengo
yanavyoteketea na watu kupoteza maisha. Mtabahatika kushuhudia jambo la
kupendeza. Jambo la kihistoria".
Macho yake yaliwatazama Joram na Nuru kwa umakini. Nao
wakifahamu kuwa kuna kitu kilitakiwa kuonekana katika macho yao, Joram
aliruhusu tabasamu kidogo huku Nuru akifuta machozi.
"Ni habari njema", Joram alisema polepole
baadaye akauliza. "Habari njema..., tunaweza kuruhusiwa kurudi chumbani
kwetu?".
Binadamu hajapata kuwa na adui mwingine, mkubwa na
mkatili katika maisha yake zaidi ya kifo. Ni kifo pekee ambacho kimeishinda
akili ya binadamu. Hakukosea yule mwanamuziki aliyeimba "kifo hakina
huruma, kifo ni kiboko yao". Hutokea binadamu akawa na shughuli zote, siku
nenda rudi bila kukipa kifo wazo lolote hadi kinapotokea bila kutegemewa. Ni
hiyo sababu pekee inalomfanya mwanadamu asitokwe na jasho la hofu siku zote za
maisha yake kwa kuogopa kifo. Kwa vile hutokea bila ya kutegemewa.
Hivyo hakuna kifo kibaya kama kifo cha kusubiri siku
na saa. Hasa kifo cha kinyama na cha kikatili kama hiki ambacho kilikuwa
kikitegemewa na watu kadha wa kadha katika nchi kadha wa kadha za Kiafrika. Leo
ilikuwa imewadia siku ile. Siku ambayo Afrika ya Kusini ilikuwa imetoa kuwa
ingekuwa ya mwisho kabla ya kuachia pigo la mwisho ambalo lingeiteketeza miji
yote ya nchi zilizoko mstari wa mbele.
Pamoja na ukweli kwamba tukio hili lilikuwa limeamriwa
kuwa siri kubwa sana miongoni mwa wahusika, kama yale mengine ambayo huishia
katika masikio ya wachache na hutoweka bila ya raia wa kawaida kuyapata, lakini
hili kwa njia moja ama nyingine lilikuwa limevuja na kusambaa mitaani. Jambo
ambalo lilisababisha mashaka na hofu kubwa mitaani. Wananchi waumini wa dini
walitoroka makazini na kukimbilia kwenye makanisa na misikiti ili kutubu dhambi
zao zote na kumbembeleza Muumba awanasuwe awanasuwe katika janga hili. Wale
ambao hawakumwamini Mungu walitulia katika vikundi vikundi wakizungumza kwa
utulivu. Wachache sana waliamua kuyamalizia maisha yao huku wakinywa pombe
katika baa ambazo hazikufunguliwa milango.
Viongozi wa Chama na Serikali walikuwa katika vikao
vya dharura wakijaribu kujadiliana hili na lile. Lolote la haja halikupatikana,
japokuwa yalitokea mapendekezo mengi. Jambo ambalo kila mmoja alitamani kutamka
ingawa ulimi ulishindwa kutamka hadharani kwa aibu, ni ambalo lingewahakikishia
wananchi uhai na usalama wao. Lakini maadamu ungekuwa uhai usio na uhuru, na
usalama usio na uhakika na hakuna aliyethubutu kupendekeza hivyo. Iliyonaki
ilikuwa kupeana moyo tu kuwa haiweze kutokea, na endapo itatokea cha kufanya ni
kujaribu kuepuka majengo ambayo yanaweza kuelekea kuyavuta macho ya muuaji.
Ilielezwa pia kuwa kote nchini wananchi walikuwa wakichimba mahandaki kwa ajili
ya kujificha.
Ikulu, Rais na baraza lake la mawaziri walikuwa katika
kikao cha muda mrefu. Kikao ambacho kilichukua siku nzima, hata usiku ukaanza
kukaribia. Inangawa kilikuwa kikao cha siri sana, lakini ilikuwa dhahiri kuwa
chochote ambacho kilikuwa kikijadiliwa ndani hakikupata ufumbuzi ya tatizo.
Mmoja alikuwa amependekeza kwa mara nyingine kuwa nafasi hiyo itumike kuivamia
Afrika Kusini kijeshi, "Ili tukomeshe kabisa suala hili la kutishiwa na
kuonewa mara kwa mara. Tutumie majeshi yetu yote ya nchi za mstari wa mbele
kuingia nchini humo na kuanzisha mapambano ili kuunda utawala halali. Najua,
adui ana jeshi imara na silaha kali sana. Lakini wingi witu wetu utasaidia
tutashinda..."Mapendekezo hayo yalijadiliwa lakini hayakuonekana kama
yangekuwa jibu la kuziokoa nchi za Afrika na kumaliza tatizo ambalo lilikuwa
mbele likisubiri saa chache ili litokee. mwingine akatoa wazo. "Si rahisi
kutumia masaa manane yaliyobaki kukusanya majeshi na kuyaongoza katika nchi
nyingine na kuanzisha vita. Zaidi yote, hatari au mkasa ambao uliokuwa
ukisubiriwa ulikuwa ukitokea angani, hivyo uvamizi huo usingesaidia au kuzuia
maafa hayo...". Baraza la mawaziri liliendelea kujadiliana kwa utulivu
katika ukumbi huo wa Ikulu. Jengo hilo likiwa miongoni katika majengo kadhaa
yaliyokuwa katika orodha ya kulipuliwa ilikuwa kana kwamba Rais na mawaziri
wake walikuwa wameamua kikisubiri kifo hicho kwa pamoja; kufa kiofisa...
Binadamu aliyekuwa na hali mbaya kuliko wote nyumbani
nchini Tanzania aliitwa Inspekta Mkwaju Kombora. Yeye alikuwa akitaabika kimwili
na kiakili. Juhudi zake zote, pamoja na wenzake wa kutoka nchi mbalimbali,
zilikuwa kama upuuzi. Upelelezi ulikuwa haukuzaa matunda yoyote yale. Na hasa
upelelezi huo ulikuwa kama umewafanya wazidi kujipalia mkaa wa moto; kwani
ilikuwa dhahiri kuwa kila jambo linaloafikiwa hapa wakati huo huo utawala wa
makaburu unakuwa na taarifa nalo. Hayo yalithibitika alipoarifiwa kuwa
wapelelezi wote waliotumwa kuingia Afrika Kusini walikuwa mikononi mwa
makaburu. Ilikuwa kama waliopelekwa kufa makusudi kabisa. Jambo ambalo
lilimfanya ashuku mara moja kwamba miongoni mwao alikuwemo chui aliyejivika
ngozi ya kondoo.
Hivyo Insipekta Kombora aliugeuza upelelezi wake
kutoka mstari wa mbele na kuanza kuchunguza mstari wa nyuma. Na haukupita muda
kabla dalili hazijajitokeza kuwa huyu mgeni aliyedhaniwa kuwa msamaria mwema,
ambaye alileta fununu nyingi kutoka Afrika Kusini angehitaji kuchunguzwa zaidi.
Uchunguzi ukaanza katika vikosi vyote vya wapigania uhuru duniani, katika vyuo
na hospitali ambazo alidai amepitia na hata Afrika Kusini. Taarifa zilizidi
kuongeza haja ya kutazamwa kwa makini. Na haukupita muda kabla kabla ya watu
waliokabidhiwa jukumu la kumwangalia hawajatoa taarifa kuwa alikuwa mtu wa
BOSS. Habari hiyo ilimuumiza sana Kombora. Alitoa amri kuwa mtu huyo aliyejiita
Clay achunguzwe kwa makini sana, kwani kwa vyovyote leo ilikuwa siku ya mwisho
iliyotolewa na utawala huo haramu na lazima angekuwa na jambo la kuarifu kwa
mabwana zake.
Baada ya hayo Insipekta Kombora aliendelea na shughuli
katika ofisi yake. Alipokea na kujibu simu na walkie talkie nyingi ambazo
hakuona kama zilikuwa zikimsaidia chochote. Aliwasiliana na maofisa wenzake
katika nchi za Zambia, Zimbabwe, Angola, Msumbiji, Naijeria na kwingineko
kujaribu kuona wamefikia wapi. Hakuna alichopata zaidi zaidi ya yale
aliyotegemea. Kwamba wananchi walikuwa wakitaabika na kulalamika mitaani katika
hali ya hofu kubwa. Kwamba hata makazini hawakuwa wamekwenda.
Ofisi ilikuwa haikaliki. Kila Kombora alipojaribu
kutulia juu ya kiti, kiti hakikuelekea kuafikiana naye. Kila alipoinuka ili
atoke, hakujua angeelekea wapi. Unawezaje kutulia na huku unahesabu saa
kusubiri kifo au maafa ya kusikitisha ambayo ni aibu kwako, kwa taifa lako na
bara lako zima? Aliendelea kutaabika kimwili na kimawazo, akipokea na
kusikiliza habari kutoka sehemu mbalimbali. Mara zilimfikia habari za Joram na
Nuru kuwa walikuwa wameingia Afrika Kusini na kuomba hifadhi ya kisiasa. Kwa
kombora zilikuwa habari za kushangaza sana. Habari za kusikitisha. Habari zinazotia
aibu. Joram Afrika kusini! Hata hivyo, alikwishachoka kushangazwa na habari za
kijana huyu anayeitwa Joram. Mambo yote aliyokuwa akiyafanya, ambayo
yaliwafikia watu wa habari, Kombora aliyasikia au kuyaona katika vyombo vya
habari. Angeweza kumsifu Joram kwa mbwembwe zake ambazo ziliwafanya polisi wote
wa miji mbalimbali na nchi zilizoendelea washindwe kumtia mikononi. Lakini kila
alipokumbuka kuwa mbio hizo za Joram zilikuwa za kukimbiza akiba pekee za pesa
ya kigeni alizoibia nchi yake alijisikia vibaya. Hayo yakifuatwa na tishio
lililokuwa likizidi kusogea, vilimfanya ajilazimishe kuliondoa jina hilo
akilini mwake.
“… Inspekta Kombora anaongea. Namba ngapi hiyo?”
alijibu sauti katika walkie talkie iliyokuwa mkononi mwake. Alipotajiwa namba alijikuta
akisikiliza kwa makini zaidi. Ilitoka kwa kiongozi wa makachero ambao walikuwa
wakifuatilia nyendo za Clay.
“… Inaelekea kama tutamkamata red handed, mzee. Sasa
hivi anaunganisha mitambo yake ya mawasiliano…”
“Nisubiri. Nakuja mara moja.”
Dakika mbili tatu baadaye, Kombora alikuwa miongoni
mwa polisi wanne waliokuwa katika chumba fulani katika hoteli ya Kilimanjaro.
Chumba hiki kilikuwa cha nne kutoka chumba cha Clay. Hata hivyo, kutokana na
mitambo waliyoitega kitaalamu, japo hawakuwa wakimwona, waliweza kumsikia
anavyoongea katika chombo fulani cha kijasusi.
“Sikiliza mzee… sikia…” askari mmoja alimwambia
Kombora huku akitweta.
“…Ndiyo. Ndiyo… nimefanikiwa kupanda katika majumba ya
kutosha. Moja Ikulu.. hapa Kilimanjaro moja… jengo la IPS moja… Kitegauchumi…
Muhimbili… Benki Kuu ya muda… Tipper… kiwanda cha Urafiki na sehemu mbalimbali
muhimu. Tunachosubiri ni saa moja tu. Ikifika, kwa jinsi nilivyotega inaelekea
jiji zima litalipuka. Mimi nitaondoka hapa wakati wowote…”
“Unasikia mzee?... Unasikia?”
Kombora hakusubiri kumsikiliza afisa huyo. Aliwaamuru
kumfuata kukiendea chumba cha Clay. Kinyume cha mategemeo yao waliukuta mlango
ukiwa wazi. Naye alikuwa kaketi kwa utulivu juu ya kochi, gazeti mkononi. Yeyote
ambaye angeingia bila ya kufahamu kinachotokea angemdhania kuwa alikuwa akisoma
gazeti.
ITAENDELEA....................
0 Comments