Mwandishi: Ben R. Mtobwa
"Bila shaka. Ulipokuwa uwanja wa ndege Dar es Salaam ulikuwa umejivika mavazi ya kizee tofauti na ulivyokuwa asubuhi. Ulipofika hapa jambo la kwanza ulilofanya ilikuwa kujibadili mavazi na kuwa kama ulivyo. Tulipofika hapa umelipa kwa fedha za kigeni bila shaka yoyote. Umezipata wapi? Na..."
"Alaa! Hivi sijakwambia? Kati ya pesa nyingi tulizopata katika mfuko wa marehemu Chonde nyingi zilikuwa za kigeni," Joram alidakia. "Nadhani nilikuonyesha Nuru."
"Ulinionyesha. Na kwa nini umeamua kupanga kwa jina la bandia?" Nuru aliendelea kusaili. "Na hapo watakapoomba kuiona hati ya usafiri utawaonyesha nini?"
"Hilo lisikusumbue. Uongo sikuanza jana. Lakini sababu kubwa iliyonishawishi kuandika jina la bandia ni hofu ya kusumbuliwa na waandishi wa habari. Unawajua walivyo, Nuru. Mara nyingi hawana kitu cha kuandika. Hivyo, wanapopata kijambo watakikuza ili kijae ukurasa. Umaarufu wangu nchini Tanzania ni jambo ambalo waandishi wa Nairobi wanaweza kuliondolea uvivu kwa haki kabisa." Akasita na kucheka kidogo. Halafu akaendelea, "Hapana Nuru. "Tumekuja kustarehe. Tunahitaji kustarehe. Nairobi ni mwanzo tu wa starehe zetu. Toka hapa, tutakwenda zetu London, Paris, Hong Kong, New York na kokote ambako roho itatuita. Lazima tufurahi. Binadamu huishi mara moja tu. Hana budi kuitumia nafasi hiyo ili akifa awe amefaidi maisha."
SASA SONGA NAYO....................
Joram aliongea kwa sauti imara, ingawa Nuru alihisi na
kuamini kuwa hakuwa mkweli. Hata hivyo, kwa kadri alivyomfahamu alihisi kuwa
Joram alikuwa na jambo, jambo ambalo lilikuwa halijakamilika kichwani mwake na
hakuona haja la kuliongelea. La sivyo, ingewezekanaje Joram ashambuliwe na mtu,
Nuru amuokoe kwa kumwua mtu huyo, waache maiti chumbani na kukodi ndege hadi
huku, wapange kwenda zao bila sababu yoyote maalumu? Hiyo si itakuwa hadithi?
Bila shaka kuna jambo.
Nuru alilingoja jambo hilo kwa hamu. Baada ya kuwa na
Joram kwa muda mrefu, baada ya kukinaishwa na starehe, na baada ya risasi
aliyoifyatua kuondoa roho ya mtu, roho ya Nuru ilikuwa juujuu ikitegemea jambo,
jambo jipya. Jambo ambalo litampa haki na wadhifa halisi wa kuwa na Joram
Kiango kama alivyokuwa hayati Neema Idd. Alikuwa ameamua kuichukua nafasi ya
Neema, katika mwili na akili ya Joram si kuichukua kwa kunywa pombe na kucheza
muziki. Ni kuichukua kikazi. Na ni kazi hiyo ambayo aliisubiri kwa hamu.
Nuru alipomtazama tena Joram alimwona kazama katika
mawazo mengi. Akamwacha na kuingia bafuni ambako alioga kwa utulivu. Alipotoka
bafuni hakumuona Joram. Badala yake alipata kipande cha karatasi Joram akimtaka
radhi kuwa amelazimika kwenda maktaba mara moja.
Upweke ulimfanya aamue kwenda chumba cha maongezi
ambako alijipatia bia mbili huku akiitazama televisheni. Aliangalia vipindi
kadhaa vya burudani na taarifa za habari. Hakukuwa na mapya zaidi ya yale
ambayo yameondokea kuwa ya kawaida masikioni na machoni mwa binadamu. Macho
yalipokinai televisheni, aligeukia chupa ambayo ilikuwa mbele yake.
Mara akatanabahi ameketi na mtu ambaye alikuwa
akizungumza. "Nasema, samahani naweza kuketi nawe?"
"Bila samahani?"
Mtu huyo aliketi na kuanza kumwaga vinywaji na
maongezi. Maongezi yake yaligeuka kumtaka Nuru. Alisema mengi, akidai kwa viapo
kuwa hakupata kumuona msichana aliyeumbika kama Nuru, kwamba alikuwa tayari
kufa ili ampate. Mara mikono yake ikakosa utii. Ikaanza kutambaa juu ya mapaja
ya Nuru. Ni hilo lililomwondoa hapo na kumrudisha chumbani kwao.
***
Joram alikuwa hajarudi. Saa kadhaa tayari zilikuwa
zimepita. Alipotahamaki, usiku ulikuwa umeingia. Alikula peke yake chumbani
humo akiogopa kwenda chumba cha maakuli ambako kulikuwa na wanaume ambao
hawakuzoea kukubali kuwa mwanamke angeweza kuwa pale peke yake. Uchovu
ulimfanya ajilaze kitandani. Hakujua usingizi ulivyomchukua. Alipoamka alijikuta
yuko mikononi mwa Joram.
"Samahani mpenzi," Joram alimnong’oneza.
Hakujishughulisha kumjibu kwa maneno. Badala yake
alilijibu busu la Joram kwa vitendo. Kisha usingizi ulimchukua tena. Alipoamka
aliupeleka mkono kumkumbatia Joram. Akajikuta akigusa godoro tupu. Joram hakuwa
kitandani. Alipofumbua macho alimwona kainama mezani akisoma kwa makini.
Akanyoosha mkono na kuichukua saa yake ndogo ya mkono kuitazama. Ilikuwa saa
kumi na nusu za alfajiri. Hakuona sababu ya kumsumbua Joram. Akajifunika na kujaribu
kulala. Usingizi haukuafikiana nae. Baada ya kuoga na kufungua kinywa asubuhi
hiyo Joram alimwomba Nuru kuwa angerudi tena maktaba. "Leo nitamaliza
shughuli zangu. Baada ya hapo tutakuwa pamoja katika kila la heri na
shari," alimweleza. Kisha akampatia kitita cha noti
akimwambia."Unajua tutakuwa na msafara mrefu? Nataka uende huko ukiwa
katika hali halisi ya kuvutia kila macho ya mwanamume. Kwa hiyo, tafadhali leo
pitapita madukani ununue kila vazi ambalo litakustahili. Usijali bei. Kumbuka
pesa tunayo."
Nuru alizipokea na kumuuliza, "Na wewe huhitaji
nguo mpya?"
"Nahitaji. Hata hivyo, sina haraka. Wanaume huwa
hawatazamwitazamwi kama wanawake."
"Najua unahitaji muda wa kuwa peke yako,"
Nuru alimwambia. "Endelea baba, siwezi kukuzuia."
Mara tu Nuru alipoondokaJoram aliingia kazini.
Alifungua begi lake na kutoa nyaraka za Chonde ambazo alitumia kila njia,
kuzielewa. Akatoa kitabu ambacho alikipata kwa taabu sana kinachoeleza mbinu
mbalimbali za kusoma maandishi ya mafumbo.
Akaketi na kuanza kutumia kitabu hicho kuyasoma tena
maandishi ya Chonde. Haikuwa kazi ndogo. Ilihitaji muda mrefu na utulivu
mkubwa. Alichofanikiwa ni kupata mwongozo ambao ulieleza namna ya kukifungua
kile kisanduku. Akakifungua bila tabu yoyote.
Ndani mlikuwa na vijigololi kumi na viwili. Joram
alikiinua kimoja na kukitazama kwa makini. Katikati ya kigololi aliona vidude
vilivyokuwa vikichezacheza mfano wa saa za electronic. Alikitazama kigololi kwa
makini akijaribu kutafuta umuhimu wake, hakuupata. Chini ya vigololi hivyo
Joram alipata ramani ambayo alipoikunjua alikuta kuwa ni ya Jiji la Dar es
Salaam. Ramani hiyo ilionyesha majengo maarufu kama Ikulu, vituo vya kijeshi,
mabenki, na kadhalika. Vitu vyote hivyo vilikuwa vimewekewa namba za kirumi
kuanzia moja na kuendelea. Namba ya jengo la benki kuu iliyoungua ilikuwa
imewekewa alama ya x kwa wino mwekundu.
Mara baada ya kuona hayo Joram alipatwa na wasiwasi.
Alihisi kuwa, kwa namna moja ama nyingine, Chonde alihusika na moto
ulioteketeza Benki Kuu. Hofu yake kubwa ilikuwa zile hisia kuwa alama
zilizofuata ambazo zilikuwa hazijawekwa x kwa wino mwekundu zilikuwa katika
orodha zikisubiri, jambo ambalo lingeleta maafa na madhara makubwa kwa nchi na
wananchi. Zaidi, ingekuwa ushindi mkubwa kwa maadui wa taifa. Hivyo, kwa mara
nyingine, alifanya sherehe moyoni kushangilia kifo cha Chonde.
Kisha alifunga sanduku hilo kikamilifu na kuirudia
meza ambayo aliinamia na kuanza kujifunza tena mbinu za kuyasoma maandishi hayo
kwa makini zaidi.
Alikuwa hajatulia vizuri mlango ulipofunguka ghafla na
Nuru kuingia huku macho yake yakiwa mekundu kwa mchanganyiko wa hasira na
mshangao. Alisimama akitweta na kumtazama Joram kwa namna ya mtu ambaye hakujua
la kusema.
"Usiniambie kuwa kuna mtu aliyekuvamia kwa nia ya
kukunajisi mchana wote huu," Joram alimwambia kwa dhamira ya kumfariji.
"Acha mzaha Joram. Sikutegemea kama ungekuwa mtu
wa kufanya kitendo kama kile."
Joram aliinua uso wake kumtazama.
"Kufanya nini?"
"Kuiba".
"Kuiba?"
Nuru akamkazia jicho la hasira. "Usijifanye
hufahamu. Dunia nzima sasa inafahamu. Kwa kweli, sikutegemea kabisa.
Imenishangaza kukuona katika televisheni ukitangazwa kama mtu hatari ambaye
ameweza kuiba fedha za kigeni ambazo nchi yake inazitegemea kama dawa."
Akasita akamtazama kwa chuki ambayo ilichanganyika na mshangao, "Kwanini
ulifanya hivyo, Joram?"
***
"Bado siamini kama amefanya hivyo," mtu
mmoja alikuwa akifoka pia, akiwa kaketi katika kundi la watu wenye hasira na
mshangao kama yeye. Mabega yao yalikuwa yakimeremeta kwa nyota ambazo zilipamba
magwanda yao kudhihirisha madaraka yao.
"Amefanya, lakini siamini kama Joram ni mtu wa
kutenda kitendo cha aibu kama hiki. Jambo la kusikitisha zaidi ni jinsi habari
hiii ilivyovuja kiasi cha kuyafikia masikio ya adui zetu. Leo nimesikia habari
hizo na Afrika Kusini," Kombora aliendelea kulalamika.
"Ujerumani pia imetangaza afande," mtu mmoja
aliongeza.
"BBC vilevile," mwingine aliongeza.
"Unaona, basi? Unaona habari mbaya zinavyosafiri
upesiupesi? Pamoja na kwamba Joram ametuasi kimsimamo tulikuwa na haki ya
kumsetiri kwasababu ya vitendo vyake vya nyuma. Sasa nadhani hatuna tunachoweza
kufanya. Maji yamekwishakumwagika, hayazoleki. Lililopo ni kutafuta uwezekano
wa kumpata na kurudisha pesa zote, hasa za kigeni."
"Hilo ndio tatizo mzee," msaidizi wake mmoja
alijibu. "Taarifa za mwisho zinathibitisha kuwa hayupo kabisa hapa nchini.
Kuna dalili kuwa ametorokea nchi jirani kwa ndege ya kukodi."
"Lazima, lazima apatikane," Kombora
alisisitiza. "Pesa alizochukua ni nyingi sana na zinahitajika sana. Hana
haki ya kuzifuja kwa starehe zake binafsi. Wasiliana na nchi jirani zote.
Wasiliana na Interpol. Waarifu kuwa tunamhitaji Joram kwa hali na mali. Maadamu
siri imekwishafichuka, hakuna haja ya siri tena."
Baada ya majadiliano marefu jalada hilo lilifunikwa na
kuletwa jingine ambalo lilikuwa “zito” Zaidi. Lilihusu mkasa au maafa
yaliyotukia taifa pamoja na lile tishio la maisha na majumba muhimu. Walipima
juhudi zao zote wakilinganisha habari mbalimbali. Haikuwepo dalili yoyote ya
kujenga matumaini.
Kisha wakavirudia vifo vya watu wawili katika chumba
kimoja cha hoteli hapa Jijini. Dalili zilionyesha kuwa marehemu walikuwa watu
wasiofahamiana kabisa. Pekuapekua yao katika chumba hicho haikuwapatia kitu
chochote zaidi ya mavazi ambayo yalionyesha kuwa yameshonwa nchi za nje.
Nyaraka walizohitaji, ambazo zingeweza kuwasaidia, hawakuzipata. Ilielekea vifo
hivi vingeingia katika yale majalada ambayo kesi zake hazikuwahi kutatuliwa.
Hivyo, baada ya kuzitazama tena picha za marehemu wote, zilirudishwa katika
majalada na kufungiwa.
Kikao kikaendelea.
*****
"Kwanini umefanya hivyo, Joram?" Nuru
aliendelea kufoka. Joram, ambaye alionekana kimawazo yuko maili kadha wa kadha
nje ya chumba hicho, alimtazama Nuru kwa muda. Kisha ikawa kama amemkumbuka.
Tabasamu dogo likamtoka, likifuatwa na sauti nzito, "Ilikuwa lazima
nifanye vile, iko siku utaelewa Nuru."
"Nitaelewa!" Nuru alifoka, "Nitaelewa
nini, mwanamume mwenye heshima zake na hadhi yake duniani anapothubutu kuingia
benki na kuiba pesa ambazo nchi na watu wake wote wanazitegemea? Siwezi kuelewa
kabisa, Joram. Ambacho naweza kuelewa ni wewe kuondoka sasa hivi na kwenda zako
ofisi ya Ubalozi wetu ukaombe radhi na kurudisha kila senti. Tafadhali fanya
hivyo, Joram."
Hilo lilisababisha kicheko kwa Joram. "Nina haki
ya kula pesa za Tanzania kama wengi wao wanavyozila, Nuru. Huoni watu wenye
mishahara ya shilingi elfu mbili wanavyojenga majumba ya mamilioni? Unadhani
wanazipata wapi bila ya wizi? Tofauti yangu na wao ni kwamba mimi nimeiba
kimachomacho, wao wanaiba kisirisiri. Mwizi ni mwizi tu." Akasita kidogo
kabla ya kuendelea, "Acha tuzitumie Nuru. Acha tuzifaidi. Hii ni nafasi
pekee katika maisha yetu ambayo hatujaisahau. Jisikie starehe..."
"Siamini kama maneno hayo yanatamkwa na Joram
Kiango. Kwanini umebadilika kiasi hicho Joram?"
Kabla Nuru hajapata jibu mlango uligongwa na kufunguka
taratibu. James aliingia. Uso wake ulionyesha kuwa alikuwa na habari ambayo si
nzuri sana. Baada ya kubadilishana salamu za kawaida aliwataka radhi na
kumchukua Joram chemba.
"Kaka, samahani. Unajua pamoja na kujiita kwako
Charles Morris, ni watu wachache sana ambao waliamini? Sura yako si ngeni
kabisa hapa Kenya. Umetokea mara nyingi katika magazeti na televishani. Wewe ni
yule mpelelezi mashuhuri Joram Kiango. Sivyo, kaka?"
Joram alipochelewa kumjibu, James aliendelea,
"Ziko habari mbaya zilizotokea katika vyombo vya habari. Inasemekana
umetoroka kwenu ukiwa umechukua fedha nyingi za kigeni. Kwa jinsi
ninavyokufahamu nashindwa kuamini kama ni kweli. Lakini hilo si muhimu sana kwa
sasa. Nilichofuata ni kukufahamisha kwamba sasa hivi wapelelezi wa hoteli hii
wamekaa kikao wakilijadili suala lako. Waweza kutiwa msukosuko mkubwa. Kwa
hiyo, nakushauri utafute mbinu yoyote ambayo itakufanya uokoe maisha yako. Nina
ndugu yangu anayeishi Nyeri. Anaweza kukuficha kwa muda."
Joram alicheka na kumshukuru James. "Usijali
rafiki yangu. Nitajua la kufanya. Kwa sasa niache nijipumzishe kidogo na
kufikiria la kufanya." Baada ya hayo aliutia mkono wake mfukoni na kuutoa
ukiwa umeshikilia noti kumi za mia mia ambazo zilidakwa na James kabla
hazijamfikia. "Kajipatie bia mbili," alimwambia akigeuka na kurudi
chumbani.
"Unaona Joram? Twende zetu ofisi ya
Ubalozi," Nuru alimdaka juujuu kwa maneno hayo.
"Kufanya nini?" Joram alizungumza kwa upole
kama kawaida yake. "Tutakwenda zetu tunakotaka. Sasa hivi uwe binti
mtulivu na ufanye kama nitakavyokuambia, tafadhali. Baada ya dakika chache
tutakuwa zetu angani tukielekea katika mji mwingine wenye starehe kuliko
huu."
"Haiwezekani, Joram. Lazima ukaombe radhi na
kurudisha pesa za watu," Nuru aliendelea kukanusha.
"Alikuwa ameishi na Joram kwa muda mrefu. Lakini
alikuwa hajapata kumuona Joram anavyokasirika. Leo hii aliziona hasira zake.
Aliiona nuru kali na tena baridi, ikijitokeza katika sauti yake ndogo, nzito,
aliposema taratibu, "Haya. Nenda zako ofisi za Ubalozi. Chukua na pesa
zetu uwapelekee."
******
Dakika mbili tatu baadae mzee mmoja wa kiume, mwenye
mvi nyingi na ndevu za kutosha alionekana akitoka katika hoteli hiyo. Alikuwa
kafatana na kijana wa kiume mwenye sura nzuri ambaye alikifunika kichwa chake kwa
kofia pana na macho kwa miwani ya jua. Mikononi mwao walikuwa na mifuko yao.
Wafanyakazi waliowatazama wakiondoka hawakuweza kukumbuka wageni hawa waliingia
lini na iwapo walikuwa katika vyumba vipi. Waliwasindikiza kwa macho hadi
walipotoka nje na kukodi teksi.
Kati ya wafanyakazi walioshuhudia wakiondoka ni James
Kamau. Hata ndoto haikumjia kuwa alikuwa akiwatazama Joram Kiango na Nuru
wakiondoka.
***SURA
YA SITA***
SAA chache walikuwa angani tena, katika Ndege ya
Shirika la Ndege la Uingereza, wakielekea London kupitia Cairo, Misri.
Sasa habari za "Wizi wa Joram" zikiwa
zimetapakaa duniani kote, zikienezwa na kila chombo cha habari, haikuwa kazi
ndogo kwao kuipata fursa hii ya kuiacha nchi ya Kenya. Polisi mitaani na katika
vituo vyote vya usafiri walikuwa macho wakimtazama kila mtu ambaye alielekea
kufanana na Joram. Passport na vitambulisho vyao vilitazamwa kwa makini zaidi,
huku maswali mengi yakiulizwa. Hata hivyo, Joram na Nuru walifaulu kupenya
vizingiti vyote huku wakicheka kimoyomoyo, kwani askari hao hawakuwatazama
kabisa kwa jinsi walivyojibadili kimavazi na kitabia, kinyume kabisa cha
matarajio ya askari.
Nuru aliuficha uzuri wake kwa kuiondoa ile hali ya
uvulana aliotoka nayo hotelini na kujivika nywele zilionekana nusu zingemezwa
na mvi. Mavazi yake pia yalikuwa yale ambayo vijana wasingependa kuyatupia
macho zaidi ya mara mbili. Jambo ambalo lilifanya wawe sawa na huyu mzee
mkongwe aliyekuwa akitembea kidhaifu, mfuko mgongoni na mkwaju mkononi. Hali
zao pia zilikuwa za wakazi halisi wa Nairobi. Hati zao za halali pamoja na
picha zao zilifichwa vilivyo katika mifuko ya siri iliyokuwemo katika mfuko
waliorithi toka kwa hayati Chonde.
Ndani ya ndege Joram alitulia akinywa bia aliyoletewa
kwa utulivu, huku mara chache akimtupia Nuru maongezi mafupi mafupi. Baada ya
muda ambao haukuwa mrefu alipitiwa na usingizi. Aliamka ndege ilipokuwa ikitua
katika Uwanja wa Ndege wa Cairo. Misukosuko ya abiria wanaoshuka na kuingia
ilipopungua walizungumza na Nuru maongezi machache ambayo dhamira yake kubwa ilikuwa
kuwafanya watazamike kama watu wa kawaida wasio na dosari yoyote machoni mwa
wasafiri wengine.
Safari ilipoanza tena Joram alikiweka kiti chake
katika hali ya kulala akimwacha Nuru akipekua kitabu chake kutafuta alipokuwa
ameishia. Ikiwa safari ndefu, ya kuvuka bahari kubwa kama hii ya Atlantic,
Joram alikusudia kutumia vyema kufidia usingizi ambao hakuupata kiukamilifu
alipokuwa Nairobi. Na ndivyo ilivyomtukia. Hakupata nafasi ya kuyafumbua macho
yake kuyatazama maji mengi yaliyotapakaa kote. Alipoamshwa na Nuru na kutazama
dirishani, alishangaa kuona wakizunguka juu ya Jiji la London wakisubiri kutua.
"Imekuwa safari fupi kuliko nilivyotegemea,"
alisema.
"Hata! Ilikuwa safari ndefu sana kama
ilivyo," lilikuwa jibu la Nuru.
Taratibu, ndege ikashuka na kutua bila msukosuko
wowote katika uwanja mashuhuri wa Heathrow. Pilikapilika za abiria kuchukua
mizigo na kutaka kutoka mapema zikaanza. Joram na Nuru, wakiwa miongoni mwa
abiria walioshuka mwisho, walichukua mizigo yao na kupita katika ofisi za
forodha na abiria wengine waliokuwa wakisubiri usafiri.
Dereva mmoja, msichana, wa shirika la usafiri la Avis
and Hertz, aliwafuata na kuwashawishi kuingia katika gari lake. Akawapeleka
mjini katika Hoteli maarufu duniani ya Wilson Place ambapo walijipatia chumba maridadi.
Mapokezi yakiwa ya kistaarabu, huduma za kistaarabu, na wahudumu waliosomea
ustaarabu, yote yaliwafanya waone kama wako nyumbani badala ya ugenini, jambo
ambalo liliwafanya wasijali chochote juu ya malipo makubwa yanayodaiwa na
hoteli hiyo.
Kuna mzungu mmoja, mshairi, au mpenzi tu wa taifa lake
ambaye aliwahi kusema: "When a man is tired of London, he is tired of life
for there is all that life can afford," kwamba binaadamu anayekinaishwa na
Jiji la London basi amekinaishwa na maisha kwa ujumla kwani London inacho kila
kitu ambacho maisha ya binaadamu yanahitaji. Joram na Nuru wasingemwona mtu
huyo kuwa mwongo sana. Pamoja na kwamba wote hawakuwa wageni sana wa jiji hili,
macho yao yaliendelea kuvutwa na vitu mbalimbali siku yao ya pili walipoamua kuzunguka
jijini. Walikodi gari lililowatembeza kila mahali kufuata matakwa yao. Kwanza,
walipenda kuona mto ule maarufu unaougawa mji wa London, Thames. Waliyatazama
maji yake yanayopita kwa utulivu pamoja na madaraja yake murua. Kisha
walizunguka katika miji ya Kingstone, Bromley, Croyon na kwingineko, wakiona
mambo tofautitofauti katika mitaa mashuhuri kama Oxford, Kingsway, Dean na
Sheftebury. Usiku ulipoingia walikwenda katika jumba la Her Majesty kutazama
michezo ya kuigiza.
"Kesho tutakwenda kutembea Epping Forest,"
Joram alimnong'oneza Nuru walipokuwa wakirudi hotelini kwao.
"Ningependa kuingia Richmond Park," Nuru
alimjibu.
"Nilipokuja kozi hapa miaka minne iliyopita
nilidhamiria kuingia lakini sijui ilikuwaje nikashindwa, safari hii
nisingependa kushindwa tena."
"Huwezi kushindwa. Tuna muda na pesa. Tutafanya
kila kitu ambacho roho itatutuma kufanya. Nafasi kama hii hutokea mara chache
sana katika miaka ya maisha yote ya binaadamu."
Chumbani kwao walivua uzee na kuurudia ujana wao.
Wakatazamana na kucheka kidogo. Kisha walikumbatiana na kuongozana kitandani.
Muda mfupi baadaye Nuru alikuwa akikoroma taratibu, huku Joram akinyata
kukiacha kitanda. Aliiendea mizigo yao na kuikagua kwa makini.
Kila kitu kilikuwemo kama kilivyokuwa kimehifadhiwa.
Akatoa kile kisanduku chenye vigololi na kuvitazama kwa makini. Kisha
alivirudisha na kuchukua vitabu vyake ambavyo alikuwa akivisoma au kufanya
majaribio ya maandishi na mahesabu kwa umakini na utulivu. Mara kwa mara
alichana karatasi hii na kujaribu ile, mara akiacha kuandika na kuanza kusoma
kwa umakini, kisha akianza tena kuandika.
"Siwezi kukusaidia mpenzi?"
Sauti ilimzindua Joram kutoka katika lindi hilo la
shughuli iliyokuwa mbele yake. Aligeuka na kumtazama Nuru ambaye alitulia nyuma
yake, uchi kama alivyozaliwa, macho yake yakitazama mahesabu katika karatasi za
Joram.
"Samahani kwa kukuvuruga. Nimekuwa nyuma yako kwa
zaidi ya saa nzima sasa. Nadhani hata hujui kuwa kumepambazuka."
Ndipo Joram alipotupa macho nje. Hakuamini. Nuru ya
jua lililochomoza kitambo ilikuwa ikipenya dirishani kwa uangalifu.
"Samahani Nuru. Usingizi ulinipaa ndipo nikaja mezani kupoteza muda,"
alisema akianza kufunika karatasi zake.
"Kupoteza muda?" Nuru alimwuliza.
"Nimekutazama kwa muda mrefu sana. Hata kuna nyakati ambazo ulikuwa ukisema
peke yako. Najua una jambo ambalo linakusumbua, jambo ambalo umeamua kuliweka
siri rohoni mwako. Hutaki kunishirikisha. Huniamini hata kidogo! Sijui nifanye
nini ili uniamini Joram!"
"Ndiyo. Afanye nini ili amwamini?" Joram
alijiuliza. Msichana huyo ambaye ameacha kila kitu hata kazi na nchi yake ili
awe pamoja naye! Msichana ambaye kuwa nae kumemsaidia sana katika kujifariji na
msiba wa Neema na aibu aliyoipata kwa kushindwa kumuua Proper! Msichana ambaye
majuzi tu aliyaokoa maisha yake kwa kumwua mtu ambaye angemwangamiza bila
huruma! Zaidi ni msichana mzuri wa sura na tabia, msichana ambaye ni ndoto ya
kila mwanaume!
“Sikia Joram, huwezi kukadiria kiasi gani nakuamini na
kukutegemea. Sifai kuambiwa lolote. Kwako mimi ni mwanamke tu ninayefaa kwa mapenzi
ya kimwili. Siwezi kuwa Neema ambaye alikuwa mwenzi wako kikazi ambaye kimwili
hukuwahi kumgusa.”
“Sivyo Nuru.”
“Wala sifahi lolote hata kukusaidia katika hesabu za
fizikia unazopiga au kusoma maandishi hayo na kuyalinganisha na hayo ya
kijasusi kama unavyofanya. Sifai hata kwenda maktaba kukusaidia kupekua walao
kitabu unachokihitaji.”
“Nuru!” Joram alifoka kwa sauti ambayo masikioni mwa
mtu asiyemfahamu ingekuwa ya kawaida tu. “Nilidhani wewe ni mtu pekee unayeweza
kunielewa. Nilidhani unaifahamu tabia na msimamo wangu. Sina tabia ya
kuyachukua matatizo yangu na kuyabwaga mikononi mwa binadamu mwingine.
Sijazowea kuchukua fumbo ambalo limenishinda kufumbua na kumwomba mtu mwingine
anisaidie. Wala tabia hiyo siwezi kuianza leo. Hivyo, ninapokuambia sina la
kukuambia maana yake sina la kukuambia. Nadhani umenielewa.”
"Nadhani nimekuelewa. Hata zile pesa
ulizozipokonya City Drive, ambazo tunachezea sasa naamini ni fumbo jingine
ambalo hukupenda kulifumbua. Sivyo mpenzi?"
Joram akatabasam, "Yaelekea mimi na wewe tutakuwa
na safari ndefu kimaisha."
Wakashikana mikono na kurudi kitandani.
*******
Baada ya kuzitawala na kuzinyonya sana nchi zetu
nyingi za Kiafrika, na baada ya 'kutoa' uhuru shingo upande, Uingereza
iliendelea kujifanya baba na mama wa makoloni yake ya awali. Falsafa hii ndiyo
chanzo cha vijimsaada kadha wa kadha. Eti pia Uingereza ndiyo mtaalamu wa
habari zinazohusu nchi zilizokuwa chini ya himaya yake. Na habari ambazo hupata
nafasi katika vyombo vya habari mara nyingi huwa ni zile ambazo si nzuri sana
kwa masikio ya wasikilizaji, yaani habari za aibu, kushindwa, rushwa udikteta,
uzembe na kadhalika. Uteuzi huu wa habari hizo mbovu na kuacha zile njema ni
ushahidi mwingine ambao huonyesha kuwa Uingereza ingependa kuendelea kuitawala
Afrika hadi siku ya mwisho ya dunia.
Habari za wizi wa fedha za kigeni katika Tanzania
zilikuwa tamu mno katika magazeti, redio na televisheni zote za Uingereza.
Zilipambwa kwa wino na rangi mbalimbali na uongo ainaaina hata zikawa kubwa
kuliko zilivyostahili kuwa. Hiyo ilitokana hasa na mwizi wa pesa hizo
alivyokuwa mtu maarufu duniani. "Ndivyo walivyo waafrika..."
liliandika gazeti moja."Kati yao hakuna mwaminifu..." Gazeti jingine
lilipendekeza kuwa Tanzania isipate msaada wowote wa kimataifa bila ya pesa
hizo kurudishwa. "Tunaamini kilichofanyika ni njama tu baina ya Joram na
viongozi wa serikali yake," Televishen moja ilitangaza.
Habari hizo
zilianza kuwa za kawaida machoni na masikioni mwa Joram na Nuru. Hawakuzijali
wala kuzishughulikia. Hata hivyo, kuna gazeti hili ambalo liliwashtua zaidi.
Mwandishi wake alikuwa amesafiri hadi Dar es Salaam ambako alifanya utafiti
wake binafsi, akihonga hapa na kuiba habari pale hata akawa ameunganisha
taarifa ambayo ilidai kuwa Joram alikuwa ametorokea Nairobi kwa ndege ya
kukodi. Mwandishi huyo alisafiri hadi Nairobi ambako utafiti wake ulimfikisha
katika chumba alichokuwa Joram na Nuru kwa majina bandia. "Kwa kila hali
sasa hivi Joram yuko London," lilieleza gazeti hilo. "Dunia haiwezi
kupumbazwa na hila zake za kujibadili sura na umbile. Kwa hali ilivyo, atakuwa
akiishi katika hoteli kubwa kwa jina la bandia.”
"Imekuwa tabia ya kawaida," gazeti hilo
liliendelea kueleza. "Kila wanapofanya madhambi yao huko kwao hukimbilia
huku. London imejaa watu weusi ambao wanaishi wanavyotaka baada ya kufanya
maovu - au mema ambayo yalionekana maovu - huko makwao. Wako wachoyo, wahujumu,
wazembe, wanafiki na kadhalika. Wengi wameziacha nchi zao zikiwa masikini zaidi
huku roho za watu zikiteketea katika vita na mauaji yasiyo na mwisho. Uingereza
tunawakaribisha na kuishi nao kama binadamu wenzetu. Miongoni mwa watu hawa
sasa yumo Joram Kiango, mtu aliyejifanya na akaaminika kuwa ana roho ya kipekee
yenye upendo na ushujaa kama ngao kwa jamii yake. Kumbe alikuwa fisi katika
ngozi ya kondoo. Huyu, Uingereza haiwezi kumstahamili. Lazima apatikane,
ahukumiwe na kupokonywa kila senti aliyobaki nayo.”
Nuru alimaliza kuisoma habari hii huku akitetemeka
kidogo. Lakini ilimshangaza alipoinua uso na kukutana na ule wa Joram ambao
ulikuwa ukichekelea. Hilo lilimshangaza. Akiwa mtu ambaye ameishi na Joram kwa
kipindi cha kutosha, alikuwa na hakika kuwa amemfahamu Joram vya kutosha.
Asingelaghaika kama watu wengine kung'amua wakati gani anacheka kwa hasira na
wakati upi anajifanya kuchukia hali amefurahi. Tabasamu hili, ambalo lilikuwa
likiendelea kuchanua katika uso wa Joram, halikuwa tabasamu batili, bali
tabasamu halisi, tabasamu ambalo huutembelea uso huu kwa nadra sana. Hivyo,
ilimshangaza sana Nuru. Alimtegemea Joram kujisingizia kucheka huku rohoni
akibabaika na kukata tamaa. Si kushangilia kama aliyepata tuzo au ushindi
mkubwa baada ya shindano gumu.
"Sijakuelewa Joram, sidhani kama hii ni habari
njema," alimwambia.
"Wala sidhani kama una haki ya kutegemea habari
njema tangu ulipokubali kuandamana na mwizi mkubwa kama huyu," Joram
alimjibu taratibu. Alipoona uso wa Nuru bado una maswali na dalili za
kutoridhika, aliongeza, "Kinachonichekesha ni huyu Mwingereza
anavyojifanya ana uchungu na nchi yetu kuliko sisi wenyewe. Utafiti aliofanya
hautokani na moyo wake wa kuwajibika bali ni nguvu alizonazo kiuchumi, uwezo
ambao ameuiba toka katika makoloni miaka nenda rudi." Alikohoa kidogo
kabla ya kuongeza, “Hawawezi kunitisha kabisa. Nitaishi hapa nikistarehe katika
jiji hili kubwa ambalo linapendeza kwa madini yaliyoibwa toka makwetu,
yaliyochimbwa kwa jasho la babu zetu. Nitaondoka hapa tu tutakapokuwa tayari
kuondoka. Sivyo, dada Nuru?"
"Nilichosema ni jinsi unavyoifurahia habari hii badala ya kuionea aibu. Sikutegemea. Au nakosea. Pengine hili ni fumbo jingine?" Joram hakumjibu.
ITAENDELEA...................
0 Comments