ILIPOISHIA...............................
“Nataka tumwone mpenzi wako anavyokufa au alipofia,” alimweleza, tabasamu la kifedhuli likiyasindikiza maneno yake. “Keti tafadhali. Keti ili uone kwa starehe.”
KIOO kilionyesha vyumba mbalimbali ambavyo vilijitokeza na kupita. Kila chumba kilikuwa na vitu mbalimbali vilivyoyavuta macho ya Nuru. Lakini ilielekea kuwa havikuwa vyumba Von alivyovihitaji. Aliuendesha mtambo huo harakaharaka kwa kubonyeza kidude hiki na kile kama karani anayepiga chapa. Mara kilitokea chumba ambacho Von alikuwa akikitafuta. Katika chumba hicho, ambacho kilionekana kidogo, walikuwemo watu wawili waliokuwa wakipigana. Mmoja hakuwa mtu bali jitu. Lilikuwa pande la mwanamume, refu, nene, jeusi lenye magumi manene na macho ya kutisha. Lilikuwa likipigana kwa maguvu yote katika hali ambayo ilionyesha kuwa lilikusudia kuua kwa mikono. Jitu hili halikuwa na dalili yoyote ya uchovu wala maumivu yoyote. Kinyume kabisa cha mtu wa pili ambaye lilikuwa likipambana naye. Huyu alikuwa kijana wa kizungu, mwenye dalili zote za ushujaa na ufundi wa kupigana ngumi na karate. Lakini ufundi wake haukuwa na dalili yoyote ya kuonyesha kulishinda jitu hili kwani tayari kijana huyo alikuwa akivuja damu hapa na pale katika majeraha ya kutisha, huku akiwa na dalili za uchovu mkubwa.
SASA SONGA NAZO....................
“Unaona?” Von alisema akicheka. “Mpenzi wako yuko
mashakani. Wakati wowote ataaga dunia. Hajatokea binadamu aliyewahi kumshinda
Toto na kukivuka chumba kile akiwa hai.”
“Kwanza Nuru hakuelewa. Kisha akaelewa. Kijana wa
kizungu aliyekuwa akipambana na jitu hilo la kutisha hakuwa mwingine zaidi ya
Joram Kiango, akiwa bado katika hali ya Uzungu bandia. Moyo ulimdunda Nuru kwa
hasira kuona akiwa ameketi hapa, juu ya kiti cha starehe, hali Joram anateseka
peke yake. Akamgeukia Von kutazama uwezekano wa kumwua na kwenda kumsaidia
Joram Kiango. Alikutana na macho makali ya Von ambayo yalimtazama katika hali
ya kuyasoma mawazo yake kinaganaga. Bastola yake ilikuwa imara mkononi,
ikimwelekea Nuru kifuani. Nuru hakuwa na la kufanya zaidi ya kuyarejesha macho
yake katika screen na kulitazama pambano hilo lilivyokuwa likiendelea. Kichwani
alikuwa akijiuliza kwa mshangao ni jitu la aina gani hili, kubwa kupindukia,
jeusi kupindukia lenya nguvu kupindukia ambalo, badala ya kutumia maguvu hayo
kupambana na utawala dhalimu wa makaburu bado, linawatetea kiasi hiki?
Alijilazimisha kutulia na kuendelea kulitazama pambano
hilo la kutisha. Joram alibadili mbinu mbalimbali, akikwepa kiufundi karibu
kila konde lililotupwa na jitu hilo, pamoja na kulipachika makonde mazito.
Lakini haikusaidia. Joram hakuweza kupita chumba hicho kukiendea chumba cha
pili ambako angeifikia mitambo aliyokusudia kuilipua. Kwa muda, Nuru alimwona
Joram kama mtu aliyekata tamaa, akifikiria kuitumia bastola yake ambayo bila
shaka ingewaweka tayari wahandisi aliokuwa akiwanyatia au kurudi alikotoka.
Hapana, alimwona vizuri zaidi. Joram alikuwa akiwaza kwa makini huku
akilitazama jitu hilo ambalo lilitulia kimya, likimsubiri kwa utulivu kama
ambalo halikuwa na uhusiano wowote na matukio yote yaliyokuwa yakitendeka.
Baada ya kulitazama sana jitu hilo Joram alifuta jasho na damu iliyojaa usoni
mwake na kutamka maneno fulani ambayo hayakuwafikia Nuru na Von. Alitamka neno
jingine.
Jitu hilo lilitulia kama lililosikia lugha yoyote ya
dunia. Joram alipolisogelea hatua moja lilikaa tayari kwa mapambano. Aliposogea
hatua ya pili lilirusha ngumi nyingi mfululizo. Joram akarudi nyuma na kuangua
kicheko. Kicheko chake kilipokelewa na Von Iron ambaye alikuwa akilitazama
pambano hilo kwa furaha. “Naanza kumheshimu mpenzi wako. Tayari amegundua kuwa
hapigani na binadamu wa kawaida.”
Nuru alijikuta akijiuma mdomo kwa hasira. Kwa nini
muda wote huo alikuwa hajagundua hilo? Joram alikuwa hapambani na binadamu.
Alikuwa akipambana na jitu lililoundwa kwa mkono wa binadamu katika umbo la
binadamu, yaani robot. Aliwahi kusikia kuwa matajiri wengi wamekwishaanza tabia
ya kuyaweka madude haya kama walinzi wao badala ya binadamu wa kawaida ambaye
hutokea siku akakukimbia au kukugeuka.
“Sasa tuone atafanya nini,” Von alikuwa akisema.
Nuru aliyafuata macho yake kumtazama Joram ambaye
alionekana akiacha kujisumbua kupambana na jitu hilo na kuchungulia kwa makini,
alifunua hiki na kile. Pilikapilika zake hizo zilimwezesha kufunua mahala
ambapo kulikuwa na waya ainaaina hadi alipoona jitu hilo likijiweka sawa kama
askari katika gwaride. Kisha lilianguka kifudifudi. Nuru alishangilia
kimoyomoyo. Kwa mshangao alimwona Von akishangilia vilevile. “Ana akili.
Amegundua kuwa dude hilo linaendeshwa kwa nguvu ya sumaku ya umeme ambayo
mitambo yake iko pale alipofunua. Ana akili…” Von alisema katika hali hiyo ya
kushangilia. Alizidi kucheka. Nuru alizidi kushangaa kwa kutomwelewa hadi
alipoongeza, “Ana akili ndiyo. Lakini zitamsaidia nini? Kwa kweli, jitu lile
lina huruma sana. Muda wote huu lilikuwa likimrudisha kwa makonde ili asiende
kujiua mwenyewe. Sasa mtazame. Ona mpenzi wako anavyojiua… Ona…”
Roho ikiwa juu Nuru, hakuwa na la kufanya zaidi ya
kutazama. Alimwona Joram akitazama saa yake na kuanza mwendo wa haraka
kukiendea chumba alichokuwa akikihitaji. Mwendo wake ulikuwa wa hadhari na
uhakika, macho yakiwa wazi, mikono tayari kwa lolote ambalo lingetukia. Mara
aliufikia mlango wa mwisho, uliomtenga na lengo lake. Alinyoosha mkono na
kugusa kitasa. Papo hapo ardhi miguuni mwake ilifunuka na Joram kudidimia
ghafla. Juhudi zake za kushika kando hazikuzaa matunda yoyote. Ardhi
ilijifunika kama ilivyokuwa na Joram kupotea kama ndoto iliyofikia ukingoni.
“Tayari…” Von alichekelea.
Nuru alijikuta yuko wima mbele ya Von akinyoosha
mikono kumpiga huku akifoka, “Yuko wapi Joram? Sema yko wapi?”
Pigo la kitako cha bastola ambalo lilitua barabara
kichwani mwake lilimpoteza fahamu. Fahamu zilipomrudia alikuwa amelazwa chali
juu ya kochi alilolikalia awali. Alikuwa uchi kama alivyozaliwa, mavazi yake
yaliyochakaa yakiwa yametupwa kando. Von alikuwa kaketi palepale alipokuwa,
sigara mdomoni. Macho yake yalimtazama Nuru kwa namna ya mtu aliyekuwa ameikata
kiu yake ya muda mrefu. Nuru alimtazama kisha akajitazama na kuona
alivyochafuka. Hakustahimili. Aliinuka na kumwendea Von kwa nia ya pambano
jingine. Lakini hakumfikia. Hatua mbili alizozipiga zilimfanya ashindwe
kuendelea na badala yake kuanguka sakafuni. Hata hivyo, mdomo haukuwa na
udhaifu kiasi hicho.
“Wewe ni mshenzi kuliko washenzi wote niliopata
kuwaona,” alifoka. “Mwanaume hayawani… Haya unasubiri nini? Niue kama
ulivyomwua Joram. Niue…”
Von alitabasamu kifedhuli. Kitendo cha mapenzi ambacho
kilimchukua dakika moja, Nuru akiwa hana fahamu, kiliupa moyo wake faraja
kubwa. Hakutegemea. Mara akawa ameelewa kisa cha baba yake kupoteza maisha kwa
ajili ya msichana mweusi. Hata hivyo, baada ya kuionja ladha aliyohitaji sana
alianza kuiona athari ya kumwacha kiumbe huyo aendelee kuwa hai. Mapambano
aliyoyaona baina ya Joram na robot yalikuwa yanatosha kabisa kumwonyesha watu
hawa walivyo wapiganaji wasiokata tamaa. Joram amekwisha, lakini huyu japo ni
mwanamke yungali hai, na anaweza kufanya lolote. Kifo cha haraka alichokidai
kilikuwa halali yake kabisa.
Hata hivyo, angehitaji kumwona akifa kwa mateso zaidi.
Angependa kuona tena anavyotaabika kushuhudia mji wao mashuhuri wa Dar es
Salaam unavyoteketea. Angependa kuuona uso wake ukijaa hofu na majonzi kama
ulivyofanya wakati Joram alipokuwa akiadhibiwa na robot Toto, na hasa pale
alipodidimia ardhini.
“Ungependa kufa sasa hivi au baadaye kidogo?” aliuliza
bila mzaha wowote katika sauti yake. “Saa moja na dakika chache baadaye kioo,
ambacho kilikuwa kikionyesha mchezo wa ngumi baina ya mpenzi wake na Toto,
kitaonyesha mchezo wa kupendeza zaidi. Jiji lenu la Dar es Salaam na miji
mbalimbali ya Tanzania na nchi nyinginezo, litapata sura mpya, sura ya
kupendeza. Natumaini ungependa kuliona hilo pia kabla hujafa ili upate habari
ambayo utamsimulia Joram huko kuzimu alikotangulia.”
Nuru, nguvu na fahamu zikizidi kumrejea, aliufurahia
uamuzi wa Von. Aliyakumbuka maneno fulani ya Joram, kati ya mengi aliyokuwa
akimpa, aliposema: katika mambo haya, kila dakika ambayo inaweza kukuweka hai
zaidi inunue kwa bei yoyote. Aliamua kuafikiana na Von. Wazo hilo hasa lilimjia
baada ya kukumbuka kuwa, kama walichofanya ni kitu chenye uhakika, dakika
chache kuanzia sasa jiji la Johanesburg litakuwa mashakani na Von atakuwa
akisema mengine. Nafasi kama hiyo itakapowadia asingeshindwa kuitumia.
Hivyo, alijifanya mnyonge zaidi. Akajiweka kitini hapo
katika hali iliyotosha kumsumbua mwanamume yeyote. Von alikwisha timiza Fula
yake ya kimwili kwa Nuru. Hata hivyo, Nuru alijua fika kwamba, kutokana na
tabia ya roho ya Fula ya mwanaume; dakika chache baadaye angerudiwa na Fula ileile
kwa kiwango kikubwa zaidi.
“Wewe ni mshenzi…” alimchokoza tena ili atazamwe
wakati huohuo akiyalegeza macho yake na kuzidi kujiweka juu ya kochi kinamna
fulani.
*********
Kitu hiki ambacho asili kiliwekwa baina ya mwanaume na
mwanamke, kitu ambacho hakielezekai kikamilifu kwa maneno, kilitimiza wajibu
wake. Nuru alibaini kuwa Von na ukatili wake, pamoja na kuamini kwake kuwa
ametosheka na kukinai, alianza upya kutaabika. Macho yake hayakuweza tena
kutulia, mikono yake ilikuwa haikai pamoja. Alihangaika, akienda hapa na pale
na kushika hiki na kile. Tahamaki akawa ameketi kochi moja na Nuru, mkono wake
mmoja ukikosa kochi na kuangukia juu ya paja nono la Nuru. “Wewe ni mtu mbaya
sana,” Nuru alisema, sauti ikiwa laini, huku akijitia kusogea kando kidogo.
“Sikiliza…”
Nuru alijitia kumsikiliza. Alichofanya hasa ilikuwa
kuupima uwezekano wa kumzidi Von maarifa aikwapue bastola yake ambayo ilikuwa
imara kama hirizi katika mkono wake wa pili.
Von hakuwa mgeni kwa silaha hii ambayo ilikuwa
ikitumiwa na Nuru. Alifahamu fika kuwa msichana huyu alikuwa akitumia mbinu ili
ayaokoe maisha yake. Lakini kufahamu huko hakukukata shauku yake ya kutamani
tena. Alitamani tena, kwa mara ya mwisho. Nuru angefanya nini? Kama kuna kisu
basi Nuru alikuwa ameshika makali yake yeye akiwa ameshikilia mpini. Hata
hivyo, alijua kuwa anacheza mchezo hatari, anacheza na nyoka. Haikuwa busara
kuchezea roho kando ya shimo la mauti lililowazi kiasi hicho. Ni hilo ambalo
lilimfanya aendelee kuishikilia bastola kama roho yake.
Wakati huo Von alikwishaibonyeza mitambo yake ambayo
alisema ingemwezesha kuiona setilaiti hiyo ikishuka taratibu toka angani na
kuiendea anga ya Tanzania ambapo ingesubiri muda uliopangwa kabla ya kuanza
kuachia dhoruba za hewa ambayo ingezusha moto wa kutisha. Katika kioo hicho
waliweza kuyaona mawingu mazitomazito yakipita katika kioo. Kisha dude la ajabu
likajitokeza. Lilikuwa kubwa, jeusi lenye muundo wa ndege aina ya kunguru.
Lilikuwa likisafiri kwa mwendo mkali sana kama linaloifuata televisheni hiyo.
Von aliinuka ghafla huku ameshikwa na mshangao.
Aliiendea meza iliyokuwa na chombo chenye vidude vingi alivyokuwa akivibonyeza
na kuvikagua kwa makini. Alibonyezabonyeza na kutazama tena katika kioo.
Alikuwa kama ambaye hakuyaamini macho yake kuliona dude hilo likizidi kusogea.
Mara jiji la johanesburg likajitokeza katika kioo hicho, majumba fulanifulani
makubwa yakitoa nuru nyekundu kama gari linaloonyesha linaelekea upande upi.
Nuru hiyo ilipokelewa au kujibiwa na dalili hiyo ya moto kutoka katika domo la
chombo hicho ambacho sasa kilikuwa kikielea juu ya mji.
Nuru aliyaelewa majumba yote hayo ambayo yalionyesha
alama za moto. Ni yale ambayo yeye na Joram walifanikisha kutega vile vigololi
walivyovipata kutoka kwa hayati Chonde. Akaitazama saa yake. Ilikuwa ikikaribia
muda uleule ambao Joram alikuwa ameviandaa vidude vile kufanya kazi. Alitamani
apige ukulele wa furaha. Tangu walipoanza harakati hizo hakuwa na hakika kama
walikuwa wakifanya kitu chenye uhakika. Wala hakumwona Joram kuwa na hakika
hiyo, pamoja na kufunua majitabu mengi ambayo yalikaribiua kumtia wazimu. Kumbe
alijua anachokifanya! Ndoto yake imetukia kuwa kweli.
Wakati Nuru akifanya sherehe hiyo moyoni, Von alikuwa
akitaabika kichwani. Hakuelewa kinachotokea. Dalili zilizojitokeza zilikuwa za
kutisha kabisa, zisizokubalika. Ilionyesha kuwa wakati wowote mji wa
Johanesburg ungekuwa ukiwaka moto, Johannesburg badala ya Dar es Salaam,
aliwaza kwa hasira. Haikuwepo njia nyingine ya kufanya zaidi ya kuamuru
setilaiti hiyo iharibiwe na kuanguka. Si kitu ikiangukia mji na kuua watu
kadhaa. Heri nusu shari kuliko shari kamili. Ni hilo alilokusudia kufanya, kuinua
simu na kuwapa wahandisi amri hiyo.
Hilo pia hakuweza kulifanya. Alijikuta akitazamwa na
bastola yake mwenyewe, ambayo alihisahau kando alipokuwa akihangaika na
mitambo. Bastola ilikuwa imara mikononi mwa Nuru, macho yake yasiyo na mzaha
yakitangaza shari. “Pokea chako, mwuaji mkubwa,” Nuru alinong’ona akifyatua
bastola.
Kwanza Von hakusikia maumivu. Alihisi kitu kikipenya
kifuani na kuupapasa moyo wake. Kisha alisikia moyo ukiwaka moto. Akahisi kifo.
Alipiga ukelele wa nguvu akichupa kumwendea Nuru mikono yake ikiwa wazi, tayari
kumkaba koo. Lakini Nuru alimwepuka kwa urahisi na kumwongezea risasi nyingine
ambayo ilimfumua fuvu la kichwa chake. Akadondoka chini na kulala kwa utulivu
kama nguruwe aliyechunwa kwa maji ya moto.
Nuru aliyatazama matokeo ya kazi yake harakaharaka.
Akaibusu bastola hiyo. Kisha akafanya haraka kujivika mavazi yake. Baada ya
hapo alikimbilia kabati la Von ambalo alilifunua na kuanza kupekuapekua
harakaharaka. Alipata alichokitaka. Ilikuwa ramani ya jengo hilo, ikiwa tofauti
na ile waliyoitumia awali. Aliisoma himahima, kwa makini, kisha akaiweka
mfukoni na kuuendea ukuta ambao ulikuwa na funguo nyingi. Akazichukua na
kuziweka katika mfuko wake. Kisha, bastola ikimtangulia, alitoka chumbani humo
mbio kama miguu yake ilivyoweza kumruhusu.
*********
Kuanguka umbali wa zaidi ya mita ishirini kutoka
angani hadi juu ya sakafu ngumu sio mchezo. Bila ya uhodari wake wa karate na
sarakasi, kama Joram asingefikia kichwa basi angefikia mgongo na
kuvunjikavunjika. Lakini alijitahidi kusahau uchovu na maumivu makali
aliyokuwanayo, akaikusanya akili yake pamoja na kubingirika. Hata hivyo, fahamu
zilimtoka kwa dakika kadhaa.
Uhai ulipomrudia alifungua macho yake kwa taabu na
kutazama pande zote. Aligutuka kujikuta akiwa amelala katikati ya mizoga mingi
ya binadamu, baadhi ikiwa mifupamifupa, baadhi ikiwa imevimbiana, mingine ikiwa
imeoza kabisa. Mara akapatwa na harufu kali ya kutisha, harufu ambayo
iliambatana na mainzi mengi manene ya kutisha, ambayo yalikuwa yakirukaruka
katika hali ya kushangilia mawindo haya rahisi. Licha ya mainzi hayo Joram
aliwaona panya wakubwa mithili ya paka waliokuwa wakifanya karamu katika miili
ya binadamu hao. Panya mmoja alikuwa akipita kumzunguka Joram huku akimtazama
kwa namna ambayo ilionyesha kuwa alitamani kuanza kumla akiwa hai bado.
Moyo ulimdunda Joram. Ingawa hakujua au kupata kuhisi
hofu katika moyo wake lakini kitu fulani kilimpanda moyoni na kumtia hasira na
kichefuchefu. Alihisi kama aliyeruka jivu na kukanyaga moto. Kama kufa kwa nini
afe kifo kibaya kama hiki? Afe huku anaona? Huku analiwa na panya? Kwa nini
asingeruhusu lile dude limwue?
Kisha alijikaza kiume na kujikongoja kusimama wima.
Ilikuwa baada ya kujikumbusha ule usemi wake wa mara kwa mara kuwa “Binadamu
hufa kwa uzee, hufa kwa ajali, hufa kwa maradhi. Lakini kuna binadamu ambao
hufa kwa uvivu vilevile, hasa katika shughuli hizi za upelelezi.” Wazo hilo
lilimtuma aanze kutembeatembea humo akitafuta mwanya ambao ungeweza kumtoa nje
ya kaburi hilo.
Alizitazama kuta na kugundua kuwa zilijengwa kwa chuma
cha pua, zikiwa kama chumba kirefu chenye upana wa mita kumi kwa ishirini.
Akatazama juu, akiangalia uwezekano wa kupanda hadi huko alikoangukia. Ilikuwa
ndoto nyingine. Ukuta ulikuwa laini mithili ya kioo ambacho kingemshinda hata
paka.
Afanye nini? Aketi kukisubiri kifo? Alijiuliza.
Hapana, lazima ajitahidi kutafuta mwanya. Lazima kuna mahala pengine penye
mlango unaotumiwa kuwaleta watu hawa kusubiri kifo. Akaendelea kutembea
akiiruka mizoga na wakati mwingine kulazimika kukanyaga mifupa. Mainzi na panya
vilimwongezea msukosuko kwa kukimbia hapa na pale, bila ya shaka kwa mshangao
wa kuona mlo wao ukitembea ovyoovyo kwenda huko na huku.
Joram alichunguza kila ukuta kwa makini. Hatimaye,
aliufikia ukuta uliokuwa na mlango wa chuma uliofungwa kwa nje. Alijaribu
kuutingisha mlango huo bila ya mafanikio. Ulikuwa mlango imara kama ukuta huo.
Akautia mkono wake mfukoni na kuitoa bastola yake ambayo aliilenga mlangoni na
kuifyatua. Risasi iliugonga na kuanguka ardhini kama gololi. Hata bomu lisingeubomoa
mlango huo, jambo lililomfanya Joram aduwae kwa mara nyingine akifikiri la
kufanya.
Mara macho yake yakavutwa na maiti moja iliyokuwa
ikitikisika. Akaisogelea na kuitazama kwa makini. Naam, ilikuwa na uhai mdogo
mwilini mwake. Miguu yake ilikuwa imekatwa na Joram aliona vilevile kuwa jicho
lake moja lilikuwa limeng’olewa. Huyu alikuwa mtu mweupe, kinyume cha wengi
ambao walikuwa weusi. Bila ya shaka alikuwa Mrusi.
“Pole,” Joram alimwambia.
“Wewe ni nani?” mtu huyo aliuliza kwa udhaifu.
“Itakusaidia nini kunifahamu?” Joram alimjibu.
“Unakaribia kufa.”
Mtu huyo alicheka kidogo kabla ya kujikongoja kusema
polepole, “Kweli. Haiwezi kunisaidia chochote. Hata hivyo, naona wewe utakufa
kabla yangu. Mwenzio hii siku ya kumi na nne bado naishi.”
Joram hakuona kama kuna umuhimu wowote wa kuendelea
kumsikiliza mtu huyo aliyekaribia kukata roho. Lakini hakukuwa na jambo muhimu
la kufanya na akaendelea kumsikiliza. Haikuchukua muda kabla hajafahamu kuwa
Mrusi huyo alikuwa mmoja kati ya watu wengi waliokuwa wakiuawa kinyama baada ya
kushukiwa kuwa walikuwa wakifanya upelelezi dhidi ya utawala wa makaburu.
Pango hili lilichimbwa maalumu kwa ajili ya
kuwaangamiza watu hao kwa siri baada ya mateso mengi. Wengi waliachwa na kufa
kwa majeraha waliyoyapata, lakini adhabu kubwa iliyowaangamiza ilikuwa njaa.
“Usishanagae,” aliambiwa. “Ni njia pekee ya
kutuwezesha kuishi.” Alipomwona Joram akizidi kushangaa aliongeza, “Au unaogopa
kula maiti? Sikia, unaweza kunila nikiwa hai. Sina dalili ya kupona. Na
ninavyokuona unaonyesha kuwa tuko pamoja katika kupambana na utawala huo
haramu. Unaweza kunila ukaishi kwa wiki moja zaidi, pengine mwujiza utatokea
nawe ukapona na kuendelea na pambano. Usiogope wala usinishukuru. Wala sitaki
kujua wewe ni nani. Haitanisaidia.”
Joram aliona kama angerukwa na akili endapo
angeendelea kuketi hapo akimsikiliza mtu huyo ambaye ilikuwa dhahiri kuwa uhai
mdogo aliobakiwa nao ulikuwa mdomoni mwake tu. Akaondoka hapo taratibu na
kuurudia mlango huo ambao alitulia tena akiutazama kwa makini.
Bado hakujua angeweza kufanya nini kuufungua.
Ingehitaji mwujiza. Harufu ya maiti hizo, kelele za panya na mainzi yaliyokuwa
yakishangilia bahati zao, vilizidi kumsumbua. Joram alijua kuwa harufu na
usumbufu huo vingemwua kabla hajasikia njaa.
Aliutazama tena mlango kwa uchungu na hasira.
Akatamani apige magoti na kumwomba Mungu ili afanye mwujiza mlango ufunguke.
Hilo hakufanya. Ingekuwa unafiki kwani hakuwa amemwomba Mungu walao kwa
kumshukuru kwa miaka mingi sasa. Vipi amkumbuke wakati wa shida? Na vipi
ategemee mwujiza mkubwa kiasi hicho wakati enzi ya miujiza ilikwishapita? Hii
ilikuwa enzi nyingine, enzi ya kutumia akili na nguvu.
Bado hakuona kama alikuwa na lolote ambalo angeweza
kulifanya kujitoa katika gereza hilo kwani kwa kila hali alijiona kama
aliyefikia mwisho wa msafara wake kimaisha. Kwa mara ya kwanza alilaani bahati
yake.
Si kwa hofu wala uchungu aliyoipata katika gereza hilo
ambalo halikutofautiana na kuzikwa hai. Hasa alijilaumu kwa kuikosa fursa ya
kujionea kwa macho yake mwenyewe utawala wa makaburu na raia wake
watakavyotaabika pindi mitego aliyoitega itakapofyatuka na silaha ambayo
waliiandaa kuwateketeza watu wasio na hatia itakapowageukia. Joram, kama
alivyo, hakuna ambacho kingemsisimua zaidi ya hilo. Aone macho ya mshangao
yanavyowatoka wakubwa wa utawala na machozi yaliyochanganyika na kamasi
yanavyowatiririka juu ya mashavu yao meupe. Aone majumba yao makubwa
waliyoyajenga kwa jasho la wanyonge yakiteketea na kubomoka kama milima ya
barafu. Na hatimaye, aone setilaiti yao ikianguka katikati ya mji wao baada ya
mitambo inayoiweka angani kulipuliwa. Ndiyo.
Ni hayo tu aliyoyahitaji Joram. Ni hayo ambayo
yalimfanya ayahatarishe maisha yake kwa muda wote huu na hata kumwaga damu
isiyo na hatia, ili, afanikishe dhamira yake. Hayo, kuyashuhudia kwa macho yake
kungempendeza zaidi ya pesa na kumsisimua zaidi ya starehe. Kwa nini amekuwa
hana bahati hiyo? Alijiuliza.
Kisha alimkumbuka Nuru. Kiasi hofu ikamrudia
alipojiuliza kama atafanikiwa kunusurika katika mapambano haya. Alikuwa amempa
maelekezo yote muhimu na kusisitiza wakati gani aanze safari ya kutoroka zake
endapo asingemwona.
Bila shaka hakuna hatakayehangaika kumtafuta msichana
mmoja ambaye hana tofauti na wasichana wengine wakati mamia ya watu yakiungua,
maelfu yakikimbia kwa fujo na mamilioni yakiwa yamepigwa na butwaa, wakati
majumba na viwanda vitakuwa vikiteketea kwa moto mkali ambao mfano wake
haujapata kutokea katika historia ya nchi hii na dunia kwa ujumla, wakati
chombo kisichoonekana kwa macho ya nguvu ya kawaida kitakuwa kikielea angani;
na baadaye kuanguka; nguvu yake inayokifanya kielee angani na za madini
inayokifanya kutoonekana zikiwa zimekwisha.
Hapana, Joram hakuona kama Nuru angeshindwa kuitumia
fursa hiyo. Bila shaka baada ya kumchanganya kwa hila alipokuwa akimfuata,
atayafuata maelezo yote.
Joram asingejisamehe endapo lolote lingemtukia
msichana yule na kumpotezea maisha. Licha ya kwamba uzuri wa Nuru haukustahili
kuharibiwa kwa mkono wa Kaburu yeyote katili, ushujaa wake ulikuwa nguzo ambayo
Joram aliitegemea sana. Yote aliyoyatenda, hekima na juhudi za Nuru
zilimsaidia. Mungu msaidie arudi salama, alimwombea.
0 Comments