Joram aliduwaa huku akimtazama msichana huyo. Hakuwa
na shaka kuwa msichana huyo ni shujaa. Lakini hakujua kuwa ni shujaa kiasi
hicho. Ndiyo, alimtegemea sana katika msafara wake. Lakini hakukusudia
kumwingiza katika mkasa ambao ilikuwa dhahiri kuwa pamoja na ugumu wa
maandalizi yake ya muda mrefu hadi sasa matekeo yake yalikuwa gizani. Yeye
alikuwa tayari kwenda, tayari kufanya kazi inayompeleka; uwezekano wa kurudi
haukumsumbua. Kufa kusingemtisha sana mradi atakuwa ameifanya kazi yake. Kifo
chake ni jambo moja, kusababisha kifo cha mtoto wa watu, mzuri kama Nuru, ni
jambo jingine.
"Sikia Nuru. Labda huelewi... Nakusudia kwenda
toka hapa sio nchi ya kawaida. Ni nchi ambayo kuna watu wenye kiu kubwa ya damu
ya mtu mweusi na njaa kubwa ya roho zetu. Na ninahitaji kujipeleka moja kwa
moja mikononi mwao. Kwa ufupi nategemea kwenda Afrika Kusini...".
"Tutakwenda pamoja".
...Na ninachokwenda kufanya ni hujuma. Wakinigundua
watanitafuna mbichi".
"Watatutafuna pamoja".
Joram akaduwaa. "Labda nikufunulie kila kitu
kilivyo Nuru", Joram akamwambia. ""Nisubiri", alisema
akiliendea begi lake lililokuwa limefurika kwa vitabu aina aina pamoja na
encyclopedia ambazo Joram alikuwa akizitumia kwa muda mrefu kujaribu kuyasoma
yake maandishi ya kijasusi ambayo aliyapata katika mfuko wa hayati Chonde. Humo
alitoa karatasi ndefu, iliyoandikwa kwa mashine, ikiwa tafsiri ya maandishi
hayo. Alimkabidhi Nuru na kumwabia asome haraka haraka.
MPANGO KABAMBE WA
KUIFANYA AFRIKA ITUPIGIE MAGOTI
Taarifa hii ni siri kubwa miongoni mwa watu wachache
sana, wa ngazi za juu katika serikali yetu. Ni taarifa ya mafanikio ya jaribio
lililofanyika muda mrefu, kwa gharama kubwa, baina ya wana sayansi wetu na
waliotoka katika nchi marafiki duniani; juu ya uwezekano wa kufanya nguvu za
nukria zitusaidie katika kuwaweka Waafrika, na ikiwezekana dunia nzima katika
kwato zetu.
Itakumbukwa kuwa kifungu kikubwa cha pesa kilitengwa
ili kufanyia majaribio haya. Kwa siri kubwa sana mtambo madhubuti ulijengwa na
setilaiti kutupwa angani. Mbili kati ya setilaiti hizo zilidondoka katika
nbahari ya Hindi kabla ya kuonyesha matokeao. Lakini setilaiti ya tatu
imetimiza majibu. Majaribio yamefanywa na kuleta matokeo ya kuridhisha kabisa.
Mtu wetu alitumwa Lagos na kutega gololi maalumu ambazo baada ya kufyatuliwa
zimeifanya setilaiti hiyo iliyoundwa kwa madini yanayoifanya isionekane kwa
macho iweze kuingia katika anga la nchi hiyo na kuachia bomba la moto mkali
ambao uliteketeza uwanja na watu kadhaa. Jaribio la pili lilifanywa huko Harare
ambako maghala yaliteketea. Jaribio la tatu na la mwisho linakusudiwa kufanywa
Tanzania, katika jengo la Benki Kuu inayojengwa. Hatuna shaka kuwa jaribio hilo
litafanikiwa.
Baada ya jaribio hilo ndipo tutaanzisha mpango wa
kuzifanya nchi zote zinazojiita za mstari wa mbele, kutupigia magoti. Mtu wetu
anayekwenda Tanzania ni mtu wa kutegemewa, aliyeishi huko miaka mingi. Atapewa
pesa nyingi zitakazomwezesha kwenda mahala popote duniani, na kumnunua mtu
yeyote. Huyu atakuwa na jukumu la kusubiri amri yetu ili aachie vipigo vingine
ambavyo vitaifanya Afrika itokwe na machozi huku dunia ikilalamika...
Nuru aliinua kichwa ghafla kumtazama Joram. Tayari uso
wake ulikuwa umelowa jasho la hofu na mshangao. "Joram" Nuru alifoka,
"Mungu wangu. Huoni kama hii ni habari ya kutisha kuliko zote? Tunawezaje
kustarehe hivi huku nchi yetu ikiwa mashakani?".
"Imenichukua siku nyingi kuigundua. Waliyaficha
maandishi hayo kwa hila ambazo zingemtoa jasho mtu yeyote mwenye akili timamu.
Hata hivyo ugunduzi huu hautatusaidia chochote. Kama ulivyosoma setilaiti hiyo
iko angani na haionekani kwa macho. Inaendeshwa na mtambo ambao uko katika
himaya yao, bila shaka ukilindwa kwa hali na mali. Hakuna njia nyingine zaidi
ya kuubomoa mtambo huo".
"Je. Tukitoa siri hii kwa dunia?", Nuru
alimuuliza Joram.
"Haisaidii. Umoja wa Mataifa utalalamika na
kuilaani Afrika Kusini. Pengine watawekewa vikwazo vya kiuchumi. Unadhani hayo
yatawafanya watuhurumie?". Mara ngapi wamelaaniwa? Mara ngapi wamewekewa
vikwazo? Hapana Nuru. Lazima nifike Afrika Kusini. Dawa ya moto ni moto".
Nuru alitulia kwa muda akiitafakari taarifa hii kwa
makini. Mara aliinuka na kumwendea Joram. Akamkumbatia na kumnong'oneza
masikioni. "Samahani sana mpenzi. Nilikuelewa vibaya sana ulipoiba pesa
benki. Vilevile nilishangaa unavyozitumia pesa hizo vibaya kwenda huku na kule
ukuwa hujali matusi ya waandishi wa habari. Sasa nimekuelewa. Nimeelewa kwanini
ulifanya vile. Ulikuwa ukijiandaa kwenda Afrika Kusini. Ulichofanya ilikuwa
kuilaghai dunia ili uonekane mhalifu na mkimbizi asiyeweza kuishi popote
isipokuwa Afrika Kusini. "Sivyo mpenzi?". Joram alipochelewa kujibu
Nuru aliongeza, "Mpenzi. Wewe ni shujaa kuliko mashujaa wengine niliopata
kuwasikia. Tutakwenda pamoja Afrika Kusini...".
"Tatizo siyo kwenda Nuru. Tatizo ni kurudi.
Unaoneje, tutarudi na zoho zetu?".
Wakati Joram na Nuru walipokuwa wakizungumza hayo,
Kombora alikuwa Ikulu mbele ya Rais akitokwa na jasho jembamba. Alifika
ofisini, akiwa hoi kwa ukosefu wa usingizi wa siku kadhaa. Mara alipopata simu
ambayo ilimtaka kwenda Ikulu mara moja, alilitia gari lake moto na kufunga
safari hiyo ya dharura hadi Ikulu ambako alielekezwa katika chumba cha faragha.
Humo aliwakuta Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Ulinzi na Katibu Mkuu katika Wizara
ya Ulinzi. Aliwasalimu kishujaa, ingawa tayari moyo ulikuwa ukimdunda kwa kujua
kuwa hakuwa tayari kuyajibu maswali yao.
"Nini hiki? Rais alimwuliza akimsogezea kijibarua
ambacho kiliandikwa kwa mkono.
Kombora alikipokea na kukitazama. Hakuwa na haja ya
kukisoma kwani ilikuwa moja kati ya zile barua ambazo zilikuwa zikiwafikia
wakubwa wa nchi za mstari wa mbele mara kuwatisha ili waache msimamo wao dhidi
ya Afrika Kusini.
"Isome," Rais alihimiza.
Kombora akakisoma. Mara alielewa sababu ya
kusisitiziwa aisome. Ilisema: "ONYO LA MWISHO." Ikarudia kutaja
sehemu muhimu ambazo aliyeandika barua hiyo alikusudia kuzichoma, sehemu ambazo
ni pamoja na Ikulu. Baada ya kuikodolea macho, Kombora aliyarudisha katika uso
wa Rais. "Nimeisoma mzee."
"Barua hiyo imekutwa katika ofisi yangu,"
Rais alieleza. "Ni dhahiri kuwa aliyeileta anao uwezo na nafasi ya kufanya
lolote katika nchi na ofisi hii. Kwanini mmempa haki hiyo?"
Kombora hakujibu. Hakujua ajibu nini. Yeye na vijana
wake wote walikuwa taabani katika mapambano haya. Majasusi wengi ya Afrika
Kusini yalishikwa, lakini halikutokea lolote ambalo lingeweza kusaidia
kukomesha vitisho vya ainaaina. Mengi yalikuwa majasusi wa kawaida, ambayo ama
hawakuwa na lolote la haja au yalitumwa kwa ajili ya masuala yasiyo na uzito
mkubwa. Wapelelezi wake ambao walikuwa nje pia walivitesa vichwa vyao bila ya
kupata matunda ya kuridhisha. Nusura Kombora apate hasira kwa lawama hizo
ambazo hakuona kama zinamstahili. Alitamani ainuke, atangaze kujiuzulu. Lakini
hayo hakuyafanya kwa kukumbuka kuwa hasira si dawa. Na licha ya hayo aliona
wazi kuwa lawama zilimstahili. Kufanya kazi ni kupata matokeo ya kazi hiyo.
Kazi isiyo na matokeo haiwezi kuitwa kazi.
"Sina haja ya kukulaumu," Rais aliendelea.
"Nauona ugumu wa jukumu mlilonalo. Nilichokuitia ili kukukumbusha kwa mara
nyingine ni kuwa hata kwa bei ya roho zetu hatuwezi kukubali kufuata masharti
ya utawala huu dhalimu. Lazima tupambane nao. Na huu ni wakati pekee wa
kuonyesha moyo wetu. Uoga hauwezi kutufanya tukubali kuwa mateka wa utawala
haramu kama huu. Lazima tushinde," akasita kidogo akimtazama Kombora kwa
makini. "Inspekta," aliongeza kwa sauti ya amri kidogo. "Huu ni
wakati wako. Kuna wakati wa njaa; wakulima hutakiwa kuiokoa nchi; wakati wa
uhaba wa fedha za kigeni wafanyakazi viwandani huombwa kujitoa mhanga; wakati
wa vita jeshi hulazimika kulinda nchi. Huu ni wakati wako, Inspekta. Nchi
inakuhitaji na kukutegemea. Gavana wa Benki amepewa amri ya kukupa kifungu
chochote cha pesa unazohitaji, Mkuu wa jeshi ameambiwa akuruhusu kutumia kikosi
chochote na Bunge limependekeza uruhusiwe kufanya lolote. Kazi kwako,"
Rais alimaliza akainuka na kutoka.
Kombora alipumbazuka kidogo juu ya kiti hicho. Jasho
jembamba lilikuwa likimtoka. Mara akajilaani kwa kusita kuleta barua ya
kujiuzulu kwake. Hakujua angefanya nini zaidi. Aliwatazama viongozi ambao
walikuwa wametulia, wakimtazama. Kiongozi mmoja alitamka neno ambalo
halikumfikia Kombora. Mwingine alitikisa kichwa. Kombora akainuka na kuwaaga.
Alipoifikia gari yake ndipo alipokumbuka kuwa ile barua ya vitisho bado alikuwa
nayo mkononi. Akaitia mfukoni na kuamuru gari limrudishe ofisini.
***
Kidole kimoja kamwe hakivunji chawa; Kombora aliwaza
akiwa kaketi ofisini mwake akifikiria afanye lipi zaidi kufanikisha vita hivi
ambavyo havikuwa na uelekeo maalumu. Akamwagiza opereta wake kumpatia viongozi
wa ofisi zote za usalama katika nchi za mstari wa mbele, pamoja na Naijeria.
Alipowapata alipanga nao kufanya mkutano wa dharura ambao ulikusudiwa kujadili
hali inayozikabili nchi zao. Ilikuwa kama wote walikuwa wakiusubiri kwa hamu
wito huu. Wakaafikiana kukutana Jijini Dar es Salaam siku mbili baadae.
Kombora, akiwa mwenyeji, alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano
huu uliofanywa kwa siri kubwa. Mkutano huu ulijumuisha watu wenye sura
mbalimbali, umri tofauti, viwango tofauti vya elimu; wote wakiwa na dhamira
moja. Kila mmoja alieleza tishio lililokuwa likiikabiri nchi yake na kila mmoja
alieleza hatua ambazo tayari zilikuwa zimechukuliwa. Lakini wote waliafikiana
kuwa matunda ya juhudi zao hayakuwa ya kuridhisha. Wote walifahamu kuwa matunda
ya maafa yaliyokuwa mbele yao siku za usoni, endapo yasingekomeshwa,
yangesababisha maafa na vilio ambavyo historia haikupata kuvishuhudia.
"Jambo linalotisha zaidi ni maoni au hisia za
wanasayansi wetu," mjumbe mmoja alieleza. "Wanaamini kuwa moto huu
unatokea angani katika chombo ambacho hakionekani kwa macho. Hivyo, jukumu letu
ni kukilipua chombo hicho. Tutawezaje wakati hatukioni?"
"Labda tuilazimishe Afrika ya Kusini
ikiteremshe."
"Hilo ndilo tatizo. Tutawezaje kuilazimisha?
Tumejaribu kutazama uwezekano wa kuishambulia kijeshi kwa pamoja na kuona si
rahisi. Wao wamejiimarisha sana kiulinzi angani, majini na nchi kavu. Nasi
Waafrika umoja wetu unalegalega kiasi kwamba hatuwezi kuafikiana mara moja.
Vilevile, wakati tutakapokuwa tukijiandaa kwenda huko madhara waliyotishia
yatakuwa yakiendelea kutukia."
"Lakini haiwezekani tukubali kuwa hatuwezi
kufanya kitu," Kombora alieleza kwa sauti. "Lazima tufanye jambo.
Jema au baya, lazima tulifanye mapema."
Aliungwa mkono.
Mara simu ikaroma katika meza ya Kombora. Akaitazama
saa yake na kuona kuwa zilikuwa zimesalia dakika nane kutimia saa kumi za
alfajiri. Akainua simu hiyo na kusikiliza. Ilipigwa na msaidizi wake ambaye
alimwomba atoke nje mara moja. Kombora akawataka radhi wageni wake na kutoka.
Dakika chache baadaye alirudi ndani akiwa kaandamana
na mgeni mmoja ambaye alikuwa katika hali ya kusikitisha. Mgeni huyo alikuwa
mtu mweupe, aliyevaa mavazi yaliyochakaa. Mwili wake ulikuwa umejaa majeraha na
mikwaruzo mingi kiasi cha kumfanya aonekane mahututi. Hata hivyo, macho yake
yalikuwa na uhai.
"Huyu ni mgeni ambaye amekamatwa huko mpakani mwa
Malawi na Tanzania leo," Kombora alieleza. "Amesema ametoroka kutoka
Afrika ya Kusini kuja baada ya kuponea chupuchupu. Maelezo yake nadhani
yatatufaa katika kikao hiki," alimaliza akimwashiria mtu huyo kujieleza. "Kwanza
ningependa ieleweke kuwa mimi sio mzungu, "mtu huyo alisema. "Mimi ni
mtu mweusi, mzaliwa wa Soweto," alisema akifungua vifungo vya shati lake.
Kila mmoja alitokwa na macho ya mshangao kwa kuona kuanzia tumboni alikuwa na
ngozi nyeusi. "Ngozi hii nyeupe iliyokaa usoni na mikononi ni matokeo ya
plastic surgery ambayo nilifanya miaka kumi iliyopita ili niweze kuingia
miongoni mwa makaburu na kuiba siri zao ili zitusaidie katika vita vyetu vya
kujikomboa," alisita kidogo. Kisha akaendelea. "Nimefanya kazi
mbalimbali katika jeshi hilo, daima nikiwa macho kupeleleza hiki na kile.
Majuzi ndipo nilipogundua jambo la kutisha zaidi. Niligundua kuwa umejengwa
mtambo ambao unaendesha Setilaiti ambayo haionekani kwa macho inayotumiwa
kuteketeza majumba na sehemu muhimu za kiuchumi katika nchi za kiafrika.
Nikaanza upelelezi wa makini kutafuta uwezekano wa kuangamiza tishia hilo. Kwa
bahati mbaya, walinishuku katika upelelezi wangu. Sikuwa na la kufanya zaidi ya
kuikimbiza roho yangu. Hata hivyo, nimeona mengi, nadhani naweza kutoa mchango
madhubuti ambao utatuwezesha kushinda."
Wakuu hao wa upelelezi walimtazama mtu huyo kwa makini
kisha wakatazamana. Mmoja alicheka, mwingine akatabasamu.
"Hatimaye...." mmojawao alinong'ona.
*****SURA
YA NANE*****
KATIKA jumba fulani, mtaa fulani, jijini Johannesburg,
makaburu wanne waliketi katika ofisi moja wakisikiliza taarifa za kijasusi
kutoka Tanzania. Jasusi moja lilikuwa likiwaarifu kwa kutumia chombo maalumu
juu ya msafara wake na mafanikio ya shughuli zake.
"Nimefika salama na kuwakabili nikiwa katika hali
ya kusikitisha iliyonifanya niaminike kama mmoja wao. Wameumeza kabisa uongo
wangu. Sasa hivi wananiamini sana. Wameniuliza mwaswali mengi na nimewajibu
kiume nikiwapa taarifa za uongo. Nadhani wamekusudia kuwatuma wapelelezi wao
huko, ingawa hawakupenda kunishirikisha moja kwa moja. Hata hivyo, msijali,
nitakuwa macho nikiarifu kila kitendo chao hatua kwa hatua."
Makaburu wakatazamana tena na kutabasamu kwa namna ya
kupongezana. Mmoja wao hakuona kama tabasamu linamtosha. Yeye aliangua kicheko.
Kisha aliona kicheko hakitoshi. Akainuka na kuliendea kabati lililokuwa nyuma
yake ambamo alitoa chupa kubwa ya pombe kali, aina ya JohnWalker na glasi nne.
Akazileta mezani na kuziweka mbele ya kila mmoja. Akaifungua na kumimina.
"Lazima tusherehekee ushindi." Baadae akaongeza, "Sitoi ruhusa
ya kunywa ofisini isipokuwa inapobidi kufurahi. Mwanadamu hana budi...
Cheers..."
Kaburu huyu kwa jina aliitwa Von Iron, kwa sura
hakutofautiana sana na mtoto mchanga ingawa kiumbo alikaribiana na kiboko
aliyeshiba vizuri. Yeye ndiye aliyekuwa kiongozi wa kamati hii maalumu ya BOSS
ambayo iliundwa kuzishughulikia kikamilifu nchi za kiafrika 'zinazojitia kichwa
ngumu.' Amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hili la kijasusi tangu
lilipoundwa miaka mingi iliyopita. Mara kwa mara kazi yake imekuwa nzuri kwa
wakubwa zake. Haikupata kutokea mpango aliouandaa ukashindwa kutoa mafanikio,
jambo ambalo lilimpa heshima na hadhi machoni mwa weupe na kumfanya jazanda ya
mauti katika fikra za weusi. Ni yeye aliyebuni uwezekano wa kuitumia nguvu ya nyuklia
kuwaangamiza Waafrika. Hakuwa Mwanasayansi, lakini alipewa jukumu la
kushirikiana nao, akiwa na uhuru wa kutumia kiasi chochote cha pesa hadi
majaribio yalipofanyika na kutoa matunda ya kupendeza. Kadhalika, ni yeye
aliyebuni mpango wa kuwapa ngozi nyeusi baadhi ya wapelelezi wao, kwa kupoteza
pesa nyingi katika hospitali zinazofanya Plastic Surgery. Watu hao waliingizwa
kwa hila katika vikundi vya wapigania uhuru na kujifanya wenzao huku wakitoa
siri zote na hata kuua inapobidi. Mmoja wa watu hao ni huyu ambaye alikuwa
akiwafurahisha sana kwa taarifa zake kutoka Tanzania.
Yeye alifanyiwa mabadiliko ya ngozi yake miaka mitano
iliyopita, akawa mweusi na kutibua mambo mengi katika chama cha SWAPO na ANC.
Majuzi alirudishwa Ulaya ambako alirudishiwa ngozi ya mtu mweupe usoni na
mikononi, kisha akatumwa Tanzania ambako waliona ni chimbuko la misukosuko yote
dhidi ya utawala wao, na hasa ili wajue nini kinafanyika katika kutapatapa kwa
Serikali na wananchi wa Tanzania juu ya mtambo wao wa aina yake ulioko angani
baada ya kutoeleweka kilichomtukia mtu wao, Chonde, hata akafa katika hoteli
moja. Zaidi, huyu alikuwa amepewa akiba ya kutosha ya zile gololi zinazouongoza
mtambo huo kulipua miradi teule ili wakati utakapowadia waachie pigo hili
walilokusudia kulifanya, "Pigo la mwisho."
Umaarufu wa Von Iron dhidi ya ngozi nyeusi ulichipuka
katika roho yake tangu utotoni baada ya kukua katika familia ya kitajiri ambayo
iliwatenda waafrika kama wanyama. Hayati baba yake alikuwa na mgodi wa dhahabu.
Watumishi wengi walifanya kazi humo huku wakilipwa ujira hafifu mno kiasi cha
kuwafanya washindwe kuyamudu maisha. Jambo hilo hakuna aliyeonekana kulijali,
hata katika fikra za Von ikajengeka kwamba mtu mweusi ni chombo cha mtu mweupe,
ambacho hakina haki wala thamani.
Halafu ikatukia maafa katika mgodi. Baba yake alikuwa
katika moja ya ziara zake adimu wakati ilipotokea hitilafu hii ambayo hadi leo
chanzo chake hakifahamiki. Hitilafu hiyo ilisababisha maafa makubwa kwa
wafanyakazi wengi, weusi kwa weupe. Hayati Iron mwenyewe aliponea chupuchupu.
Kama asingejitokeza mtumishi wa Kiafrika, mzee mkongwe, ambaye alitumia nguvu
zake zote kumtoa katika chumba kilichokuwa kimefunikwa kwa mawe, siku hiyo
angeyapoteza maisha yake. Hata hivyo, jukumu hilo lilimgharimu mzee huyo maisha
yake kutokana na majeraha mabaya aliyopata. Kifo hicho kilimsikitisha sana mzee
Iron hata akajitolea kuishi na mtoto pekee wa mzee huyo ambaye alikuwa msichana
mzuri, ingawa uzuri huo ulipotoshwa na unyonge aliokuwa nao rohoni. Uamuzi wa
kuishi na Mwafrika katika nyumba moja, ukiwa jambo geni sana wakati huo,
uliisababishia familia yake mgogoro mkubwa, hasa mkewe. Lakini Iron
hakulikubali hilo asilani. Badala yake akazidisha mapenzi kwa msichana huyo
huku akiahidi kumpeleka masomoni, nje ya nchi.
Halafu ikatokea. Mzee Iron akafumaniwa na msichana
huyo. Ilikuwa habari iliyojaa aibu kubwa masikioni mwa kila mtu mweupe. Lakini
Iron hakuona aibu. Alikitetea kitendo chake na kukataa matakwa ya mkewe kwamba
msichana huyo yatima afukuzwe. Hata mkewe alipotishia kujiua Iron hakukubali
kumtupia msichana huyo lawama ambazo hazikumstahili. Ikatokea tena.
Wakafumaniwa kwa mara ya tatu. Hapo mama Iron hakustahamili zaidi. Alirudi
chumbani ambako alichukua bastola na kumwua msichana yule mweusi.
Mzee Iron alizirai kwa hasira. Fahamu zilipomrudia
aliipokonya bastola hiyo kutoka mikononi mwa mkewe na kumpiga risasi mbili
kifuani. Kisha alijilenga kichwa na kufyatua risasi zote zilizosalia. Vifo vyao
vilikuwa simulizi kubwa mitaani kwa muda mrefu. Vilimwacha Von katika msiba wa
uyatima, msiba ambao ulizaa hasira dhidi ya mtu mweusi; akijua kuwa ni mtu
mweusi aliyemnyima haki ya kuwa na wazazi. Jambo hilo lilimfanya siku zote awe
mstari wa mbele katika kutukuza na kutekeleza taratibu zote za ubaguzi. Daima
alikuwa mkatili kuliko wakatili, mnyama kuliko wanyama dhidi ya mtu mweusi.
Matokeo yake yakawa kupata vyeo vilivyomwezesha kuwa na mamlaka juu ya uhai na
kifo kwa kila mtu mweusi katika shirika hili la kijasusi. Wengi waliuawa kwa
ajili yake, mengi yaliendelea kufanyika ili kumkomoa mtu mweusi kutokana na
mapendekezo yake. Lakini hakukoma kuendelea kubuni. Mtambo uliokuwa angani
ukisubiri kuiharibu Afrika huru ulikuwa moja tu kati ya ubunifu wake.
Pamoja na kutenda mengi ya kikatili, pamoja na
kuhakikisha watu weusi wengi wasio na hatia wakipoteza maisha yao, bado Von
hakuona kama viumbe hawa walielekea kumpigia mtu mweupe magoti. Badala yake
waliendelea kusimama kiume wakitetea haki yao. Alipokufa huyu, alizaliwa huyu,
wimbo uleule ukiwa mdomoni. Hata Mandela, ambaye alikuwa kifungoni, alipoteswa
bado aliendelea kuwa na msimamo uleule. Hilo, kiasi lilimtisha sana kaburu Von.
Hakuwaelewa kabisa watu hawa. Wana nini katika damu yao?
Swali hilo lilikuwa likimletea maswali mengine ambayo
yalijenga hisia fulani, maswali yaligongana kichwani mwake. Alikuwa akijiuliza:
baba yake aliona nini katika nywele kavu, ngozi nyeusi na sura ya kusikitisha
ya yule msichana wa Kiafrika hata akadiriki kumwua mkewe na kujiua mwenyewe!
Aliwahi kusikia hadithi ya mtu mwingine ambaye alimwacha mkewe na kukimbia na
msichana mweusi hadi Marekani ambako walifunga ndoa. Wana nini watu hawa? Iko
siri gani ndani ya ngozi zao zinazotisha? Labda ingebidi alifumbue fumbo hili
kwa kumpata mmoja ili aonje? Lakini...mweusi... Hapana. Mara kwa mara
aliyafukuzia mbali maswali hayo ambayo yalimjia bila taarifa, hasa
alipoukumbuka uyatima wake.
"Cheers," Von aliropoka tena.
Wenzake wakageuka na kumtazama kwa mshangao. Kisha
wakatabasamu kimyakimya, wakiendelea kunywa taratibu. Baada ya vinywaji hivyo,
Von aliamua waendelee na kikao chao.
Walivuta mafaili ya suala la Chonde na kuangalia
wamefikia wapi juu ya kisa cha kifo chake na mali zake zilielekea wapi. Bado
haikueleweka nani alimuua na maiti ya pili chumbani mle ilikuwa ya nani. Zaidi
haikufahamika vitu alivyokuwa navyo, ambavyo ni vya hatari na siri kubwa,
vilikwenda wapi. Kitu kimoja walikuwa na hakika nacho. Vitu hivyo havikufika
mikononi mwa polisi, jambo ambalo liliwafanya waafikiane kuwa watu waliomwua
Chonde na kumwibia pesa nyingi na vitu alivyokuwanavyo ni majambazi wa kawaida,
ambayo yangevitupa vifaa vile muhimu kama takataka na nyaraka za siri kama
uchafu. Kitu ambacho wangejua kukitumia ni pesa za Tanzania na za kigeni ambazo
zingewachukua miezi mingi kabla ya kuzimaliza.
Pesa hazikuwa tatizo kwa akina Von. Walilitupa suala
hilo kando bila kinyongo, hasa wakijua kuwa tayari mtu wao mwingine, Clay,
alikuwa nchini Tanzania akiwa na kila kitu kilichohitajika na tayari kwa yote
waliyohitaji kufanya. Alikuwa na nafasi nzuri zaidi ya Chonde kwani uongo
aliokwenda nao ungemfanya aonekane kama almasi machoni mwa maafisa wa usalama
wa nchi zote za mstari wa mbele za Kiafrika.
"Nadhani iliyobaki ni kuongeza ulinzi katika
mtambo wetu," Von aliendelea. “Ingawa Clay yuko kwao na atatuarifu kila
wanachokusudia kufanya, lakini kuna mengine watakayoshindwa kumwambia. Ni wazi
kuwa watatumwa wapelelezi waje, lakini sitaki warudi. Nadhani
tunaelewana." Akaungwa mkono.
Mara simu ya dharura ikaanza kulia. Ikiwa simu ambayo
hulia kwa nadra sana, Von aliinua mkono na kuidaka mara moja. "Von
hapa," akanguruma katika chombo cha kusemea.
"Bosi, hapa ni kikosi cha ulinzi wa anga. Ndege
zetu za ulinzi zimeizunguka ndege moja ambayo ina watu wanne tu, rubani na
msaidizi wake na abiria wawili ambao ni mwanamke na mwanamume. Rubani wa ndege
hiyo anaomba kutua, akidai kuwa ametekwa nyara na abiria hao ambao
wamejitambulisha kama Joram Kiango na mpenzi wake Nuru. Tunauliza kama
tuwaruhusu kutua au tuwalipue".
"Nani, Joram?" Von aliuliza.
"Ndiyo. Joram Kiango. Yule..."
Mara Von akalikumbuka jina hilo vizuri. Halikuwa jina
la kupendeza hata chembe masikioni mwake, ingawa siku mbili tatu zilizopita
limesikika kwa namna ya kupendeza kiasi. Joram kuja Afrika Kusini! Baada ya
kuharibu mipango yao mingi ya kuikomoa Tanzania! Bila shaka ni kujaribu kujificha
baada ya kuiibia nchi yake akiba yote ya pesa za kigeni. Vizuri. Tutampa
hifadhi ya kudumu. Anaweza kujificha milele katika makaburi yetu. Hatuna roho
mbaya.
"Umesema Joram siyo? Sikia. Huna haja ya kutumia
silaha kubwa. Anaweza kufa polepole. Mwambie atue."
Kwa Afrika Kusini ilikuwa kama nafasi ya dhahabu.
Vyombo vyote vya habari vilishangilia kwa nguvu kuwasili kwa Joram na Nuru
katika nchi yao. Waliipamba habari hiyo kwa kutia chumvi nyingi juu ya wizi
wake. Walieleza jinsi alivyopokonya pesa hizo, alivyozitumia kwa starehe sehemu
mbalimbali duniani, alivyofaulu kuwalaghai polisi wote wa dunia, na mwisho
alivyoona hana hila zaidi ya kukimbilia Afrika Kusini, ili ajifiche maisha.
"Huu ni mfano hai kwa watu weusi kote
ulimwenguni," mtangazaji mmoja wa televisheni alieleza. "Hakuna
asiyemfahamu huyu Joram. Alijifanya mpigania haki, usawa na usalama wa watu
wake. Amesababisha vifo vya watu wengi ambao walikuwa na nia njema ya kuikomboa
nchi yake. Ndivyo walivyo watu weusi wote. Wanawalaghai wenzi wao na kuwafanya
waote mikia misituni eti wakidai haki na uhuru. Matokeo yake ni kuwafanya, hao
wenzi wao, vijakazi, wakati wao wakituna matumbo mara tu baada ya kupata
madaraka. Natumaini watu weusi wote mnaodanganywa mtaitumia nafasi hii kuuona
ukweli wa mambo. Ngozi nyeusi ni dalili ya laana. Nywele fupi ni dalili ya
akili ndogo. Bila hekima na uongozi wa mtu mweupe Afrika ingekuwa bado gizani,
na endapo ataondoka mtu mweupe giza litarudi..."
Hayo yalisemwa baada ya watu kuwatazama Joram na Nuru
wakitoka katika ndege iliyowaleta, huku wakiwa wametanguliwa na rubani ambaye
walikuwa wamemshikia bastola. Nje ya ndege Joram aliitupa chini bastola yake na
kuweka mikono yake juu. Ndipo Polisi wa makaburu ambao walikuwa wameuzingira
uwanja wakiwasubiri, wakajitokeza na kuwakimbilia. Wakawavamia na kuwakagua
harakaharaka. Walipoona kuwa hawana silaha nyingine wakawaongoza kuliendea gari
lililokuwa likisubiri. Muda wote huo kamera za televisheni na zile za wapiga
picha wa magazeti ziliwaelekea Joram na Nuru kwa ukamilifu. Kama kuna chochote
kilichowashangaza watazamaji ni jinsi sura za vijana hawa zilivyoonekana
tulivu, nzuri, zisizo na dalili zozote za ugangwe kama walivyotegemea.
Msafara wa gari uliishia katika jumba moja kubwa lenye
ghorofa kadhaa. Humo, badala ya lifti waliyoingia kuwapandisha juu
iliwateremsha chini ambako walijikuta katika chumba kilichoelekea kuwa maalumu
kwa kuhoji mateka. Askari waliokuwa nao waliamuru kusubiri, kisha wakatoka na
kuufunga mlango nyuma yao. Baada ya muda waliletewa chakula na vinywaji. Wakala
na kunywa.
0 Comments