ILIPOISHIA................
Kumbe alikuwa fisi katika ngozi ya kondoo. Huyu,
Uingereza haiwezi kumstahamili. Lazima apatikane, ahukumiwe na kupokonywa kila
senti aliyobaki nayo.”
Nuru alimaliza kuisoma habari hii huku akitetemeka
kidogo. Lakini ilimshangaza alipoinua uso na kukutana na ule wa Joram ambao
ulikuwa ukichekelea. Hilo lilimshangaza. Akiwa mtu ambaye ameishi na Joram kwa
kipindi cha kutosha, alikuwa na hakika kuwa amemfahamu Joram vya kutosha.
Asingelaghaika kama watu wengine kung'amua wakati gani anacheka kwa hasira na
wakati upi anajifanya kuchukia hali amefurahi. Tabasamu hili, ambalo lilikuwa
likiendelea kuchanua katika uso wa Joram, halikuwa tabasamu batili, bali
tabasamu halisi, tabasamu ambalo huutembelea uso huu kwa nadra sana. Hivyo,
ilimshangaza sana Nuru. Alimtegemea Joram kujisingizia kucheka huku rohoni
akibabaika na kukata tamaa. Si kushangilia kama aliyepata tuzo au ushindi
mkubwa baada ya shindano gumu.
"Sijakuelewa Joram, sidhani kama hii ni habari
njema," alimwambia.
"Wala sidhani kama una haki ya kutegemea habari
njema tangu ulipokubali kuandamana na mwizi mkubwa kama huyu," Joram
alimjibu taratibu. Alipoona uso wa Nuru bado una maswali na dalili za
kutoridhika, aliongeza, "Kinachonichekesha ni huyu Mwingereza
anavyojifanya ana uchungu na nchi yetu kuliko sisi wenyewe. Utafiti aliofanya
hautokani na moyo wake wa kuwajibika bali ni nguvu alizonazo kiuchumi, uwezo
ambao ameuiba toka katika makoloni miaka nenda rudi." Alikohoa kidogo
kabla ya kuongeza, “Hawawezi kunitisha kabisa. Nitaishi hapa nikistarehe katika
jiji hili kubwa ambalo linapendeza kwa madini yaliyoibwa toka makwetu,
yaliyochimbwa kwa jasho la babu zetu. Nitaondoka hapa tu tutakapokuwa tayari
kuondoka. Sivyo, dada Nuru?"
"Nilichosema ni jinsi unavyoifurahia habari hii badala ya kuionea aibu. Sikutegemea. Au nakosea. Pengine hili ni fumbo jingine?" Joram hakumjibu.
SASA SONGA NAYO...................
Jioni hiyo maisha yaliendelea kama kawaida. Joram
alijipitisha hapa na pale akifanya hili na lile. Sasa ilikuwa dhahiri kwa Nuru
kuwa alikuwa katika shughuli kubwa na ngumu kinyume cha alivyoiruhusu sura na
sauti yake kuonyesha. Nuru hakujisumbua kumuuliza lolote akichelea kupoteza
muda wake kwani ingekuwa sawa na kumpigia mbuzi gitaa ukimtegemea kucheza
rumba. Hata hivyo, Nuru alipopata wasaa alimkabili Joram na kumwambia
taratibu,"Unadhani mwandishi yule anatania anaposema watafanya juu chini
kututafuta? Huoni kama tunaweza kupatikana? Hila hizi za kujibadili si zimekuwa
teknolojia ya kawaida siku hizi? Sidhani kama zinaweza kutusaidia."
"Najua, mpenzi. Ninachojivunia ni wingi wa watu
na ukubwa wa jiji hili. Itachukua muda hadi wafike hapa na kutukamata. Wakati
huo hatutakuwa hapa tena, bali tutakuwa angani tukimalizia kuitembelea nchi ya
mwisho ya dunia. Usijali Nuru. Starehe bila hofu yoyote..."
Joram hakuumalizia usemi wake kabla ya kuusikia mlango
ukigongwa. Wakatazamana huku wakisikiliza. Mlango uligongwa tena kwa nguvu
kuliko mwanzo. Joram hakuwa mgeni na ugongaji wa polisi. Kwa mara ya kwanza
akajikuta kuwa alikuwa amekosea sana kuwadharau polisi wa Uingereza kiasi
hicho. Akamtupia Nuru jicho ambalo lilibeba ujumbe ambao masikioni mwa Nuru
ulieleza waziwazi "Cheza nao." Papo hapo akatoka na kuingia bafuni
huku akiufunga mlango nyuma yake.
Mlango ulipogongwa tena Nuru aliinuka na kuufungua.
Kama alivyotegemea mlango ulipofunguka aliingia askari mmoja mwenye cheo cha
Sajenti akifuatana na mmoja kati ya maofisa wa hoteli hiyo.
"Samahani sana dada," afisa huyo alieleza.
"Tumelazimika kukusumbua kidogo. Nadhani utatuwia radhi. Huyu hapa ni
Sajini Brown kutoka Scotland Yard, yuko katika ziara ya kuwatembelea wageni
wote wa hoteli hii ili kutazama hati zao za usafiri na maswali madogo madogo
ambayo nadhani utamjibu. Ni mzunguko wa kawaida tu kwa ajili ya tukio dogo
ambalo wangependa kulikamilisha ili wasirudi tena katika hoteli hii."
"Bila samahani,"Nuru alijibu akimgeukia
polisi huyo ambaye alikuwa akitoa kitambulisho chake.
"Kwa kawaida hapa kwetu hatusumbui wageni,"
askari huyo alieleza. Tunatimiza ombi la INTERPOL tu," alisita akimtazama
Nuru kwa makini zaidi. Sijui dada unaitwa nani?"
"Mrs Prosy Godwin".
"Kutoka?"
"Naijeria".
"Yuko wapi bwana Godwin?"
"Ametoka, nadhani atarudi baada ya dakika
chache."
"Naweza kuona hati zenu za usafiri pamoja na
nyaraka nyingine kama zipo?"
"Bila shaka," Nuru alimjibu akiendea mfuko
ambao aliufungua na kutoa hati. Akazikabidhi kwa askari huyo ambaye alianza
kuzipekuapekua.
Dakika hiyohiyo mlango wa bafu ulifunguka. Askari
alipogeuka kutazama alikutana na pigo ambalo lilitua katika shingo yake
kikamilifu. Pigo lililokusudiwa kummaliza, lakini halikutimiza wajibu.
Lilimfanya apepesuke na kuegemea ukuta. Mkono wake ukapaa kukinga pigo la pili
huku mkono wake wa pili ukisafiri kuitafuta bastola. Joram hakuruhusu mkono huo
utoke na bastola. Aliachia judo ambayo ilitua ubavuni mwa askari huyo na
kumlegeza. Pigo lililofuata lilimlazimisha kuanguka sakafuni. Baada ya kazi
hiyo ndipo Joram alipomgeukia afisa wa hoteli ambaye alikuwa kaduwaa, mdomo
wazi, kama asiyeamini macho yake.
"Mwinue ndugu yako na umpeleke bafuni,"
Joram alimwamuru.
"Vipi bwana Godwin? Nadhani hukumwelewa huyu
bwana. Alikuwa hana nia mbaya zaidi ya... ya..."
Joram hakuwa na muda wa kuchezea. Alijua afisa huyu
alihitaji nini kumtoa mshangao. Pigo moja tu, ambalo halikutegemewa lilimfanya
afisa huyo aanguke chini kama gunia. Hima, Joram alianza kuwavutia bafuni mmoja
baada ya mwingine. Kisha aliufunga mlango wa bafu kwa funguo na kumfuata Nuru
ambaye pia alikuwa ameshangaa.
"Kwa nini umefanya hivyo Joram? Haikuwepo kabisa
haja ya kuwashambulia. Askari huyo asingegundua lolote. Sasa watajua kuwa uko
hapa na wataanza kututafuta kwa udi na uvumba."
Si kitu. Kwa nini tujikombekombe kwao? London si mji
mzuri pekee yake katika dunia hii. Bado tuna haja ya kuiona miji mingine."
***
"…Ni mtu wa hatari duniani. Ameidhihirishia dunia
kuwa hana tofauti na yule mwuaji mwingine anayetafutwa duniani kote, Carlos.
Sasa kinachotakiwa kufanyika si kumtafuta yeye bali roho yake. Vinginevyo,
dunia itakuwa imestarehe ikisubiri kuimarika kwa kiumbe mwingine wa hatari
zaidi ya faru mwenye wazimu.”
Hayo yalikuwa mapendekezo ya mwisho katika gazeti lile
lililohisi kuwepo kwa Joram Jijini London, na hatimaye kuandika juu ya tukio la
kutisha lililowapata askari wa Scotland Yard na Afisa wa hoteli. Watu hao ambao
walifunguliwa kutoka katika bafu saa kadha wa kadha baada ya Joram kuondoka
zake, walieleza jinsi walivyowakabili watu ambao mtu yeyote asingefahamu kuwa
wangeweza kuwa Joram Kiango na Nuru. Askari huyo alieleza hayo akiwa katika
chumba cha X-ray, kuangalia uwezekano wa kuungika kwa mbavu zake tatu
zilizovunjwa na Joram.
Baada ya kuongea nao kwa marefu na mapana ndipo waandishi wa gazeti hilo wakatoa habari hizo zikiwa zimepambwa kwa picha nyingi za kuchora, picha ambazo ziliwachora Joram na Nuru katika sura na mavazi tofauti; wakijaribu kuonyesha jinsi gani wanavyoweza kujibadili. Chini ya michoro hiyo kulikuwa na maelezo yaliyoandikwa kwa herufi nzito yakisema; "Unashauriwa kujihadhari nao. Ukimwona ua kwanza, uliza maswali baadaye."
Gazeti hilo lilisomwa kote duniani. Maelezo yake
yalidakwa na TV na redio zote duniani. Watu wengi, ambao walimchukia Joram
walizidi kushangilia, hali wale waliompenda walizidi kushangaa.
"Sijui amepatwa na nini mtoto huyu,"Inspekta
Kombora alifoka huku akilitupa gazeti hilo mezani. "Yuko London na
anafanya anavyojua. Anazidi kulipaka matope jina lake ambalo tayari
amelichafua.”
Ilikuwa dhahiri kwa yeyote amtazamaye Kombora machoni
kwamba alikuwa hajapata usingizi wa kutosha kwa muda mrefu. Mambo mengi yalimkabili
kichwani kiasi cha kumpokonya hata hamu ya kula. Angewezaje kustarehe wakati
siku zilikuwa zikisogea huku halijapatikana lolote la haja katika kukomesha
tishio kutoka nchi adui ambalo lilitaka serikali iache msimamo wa kimapinduzi,
la sivyo ajali zingeendelea kutokea. Tanzania kuacha kuzisaidia nchi
zinazopigania haki na uhuru wake ilikuwa ndoto ya kupendeza. Kamwe isingetokea.
Lakini kuendelea kusaidia nchi hizo huku ukisubiri maafa ya hatari sana, kwa
nchi yake na rafiki zako hali huna uwezo wa kufanya lolote ilikuwa ndoto ya
kusikitisha sana, ndoto ambayo ingeweza kutokea.
Walikuwa wamefanya yote ambayo wangeweza kufanya
katika juhudi za kuhakikisha usalama. Yote; mema kwa maovu. Magereza ya Keko na
Ukonga yalikuwa yamejaa wageni wengi ambao ama waliingia nchini kinyume cha
utaratibu, au hati zao zilitia mashaka. Wote hawa walihojiwa kwa maneno na
vitendo. Waliokuwa watakatifu waliachiwa, wenye madhambi ya magendo na
uzururaji wakifunguliwa mashitaka. Ni mtu mmoja tu ambaye alielekea kuwa na
mengi au machache ambayo yangehusiana na usalama wa nchi.
Huyu alikamatwa katika hoteli ya New Africa baada ya
kulala hapo kwa siku moja. Wapelelezi walimshuku baada ya kumsikia
akiulizauliza maswali juu ya watu walikufa katika hoteli hiyo; ni wa aina gani
na walikufa vipi. Alipokamatwa na kutakiwa kutoa vitambulisho, hati zake
zilionyesha kuwa ni mwanachama wa ANC ambaye ametoroka kutoka Namibia. CID
waliwasiliana na ofisi hizo. Jina la Kweza halikuwemo katika orodha ya
wanachama wa ANC. Ndipo lilipofunguliwa bomba la maswali dhidi yake. Na ni hapo
ilipodhihirika kuwa hakuwa mtu wa kawaida jinsi alivyoweza kuyajibu maswali
yote kwa ukamilifu kama ambaye alijiandaa kuyajibu.
Begi lake ambalo lilikaguliwa harakaharaka bila ya
kuonekana chochote, lilipekuliwa tena. Baada ya jitihada kubwa iligundulika
mifuko ya siri ambayo ilificha silaha, vyombo vya mawasiliano na vitu
mbalimbali vya kijasusi. Alipoulizwa alikovipata alikanusha kuwa havifahamu,
wala hakupata kuviona vitu hivyo. Ni majibu hayo ambayo yalimuudhi Kombora hata
akaamua apelekwe katika chumba cha mateso ili, kama hasemi, autapike ukweli.
Taarifa zilizomjibu Ispekta Kombora zilisema kuwa alikuwa hajasema lolote.
Ndipo alipolitupa gazeti alilokuwa akisoma habari za
Joram, na kumtoa akilini kwa muda. Akaondoka na kuingia katika lifti ambayo
ilimteremsha chini ya ardhi kiliko chumba cha mateso. Kombora hufika katika
chumba hiki kwa nadra sana. Harufu ya mchanganyiko wa damu, kinyesi, jasho na
machozi ni jambo moja ambalo humfanya aape kuwa asingerudi tena kila anapofika
humu. Jambo jingine ni sura za watesaji. Sura hizi humtisha zaidi ya mateso
yenyewe, zikimfanya aamini kuwa watu hao kama kweli wana roho, basi wana roho
za chuma. Nayo macho ya wanaoteswa si jambo ambalo macho ya mtu mstaarabu
yatapendezwa kuangalia.
Leo hii alimkuta Kweza, au kilichosalia katika umbo la
aliyekuwa Kweza; akiwa amelala sakafuni, sura yake ikiwa haitambuliki kwa
kuvimba na kuchubuka. Vidole vyake vyote tayari vilikuwa vimevunjika, jicho
moja limetumbuka na meno manne yamepotea. Watesaji walikuwa wamemwinamia
wakimdunga sindano ambayo ilikuwa na waya, iliyotokea katika soketi ya umeme.
"Mwachieni kidogo," Kombora aliamuru
akikiendea kiti na kuketi. "Mleteni hapa."
Kweza alisimamishwa mbele ya Kombora, akitetemeka kwa
uchungu na maumivu makali. Nusura Kombora amhurumie, huruma hiyo ilimtoka mara
moja mara alipomfikia mtu huyo; mtu mweusi; kibaraka, msaliti wa juhudi za
weusi wenzake katika kujikomboa kutoka kwenye udhalimu ambao umewaandama miaka
nenda rudi. Mtu kama huyu ahitaji kuhurumiwa hata chembe.
"Wewe!” Akafoka. "Kwa nini hutaki kusema
ukweli? Kama ukisema ukweli tutakuacha uende zako."
Pamoja na maumivu aliyokuwanayo mtu huyo, alicheka,
"Nimekwisha sema kila kitu. Tatizo lenu ni kwamba hamtaki kuelewa
ninachosema. Na juu ya kuniacha niende zangu nimewaambieni mara nyingi kuwa
sihitaji kwenda popote. Naomba mkichoka kunitesa, mniue."
"Umesema ukweli? Ukweli gani?"
"Nimesema kuwa mimi sifahamu chochote juu ya
maswali mnayoniuliza. Nilichofuata ni kumtafuta rafiki yangu Chonde ambaye
inasemekana amefariki. Nilitaka kufahamu amefariki vipi ili niitulize roho
yangu.
"Chonde rafiki yako vipi?"
"Alikuwa rafiki wa kalamu. Sikuwahi kuonana naye
ana kwa ana."
Kombora alimtazama kwa makini. Macho yake makali
yalimfanya Kweza aangue tena kicheko dhaifu huku akisema, "Mnaupoteza bure
muda wangu na wenu. Mimi sifahamu chochote. Nanyi hamna lolote ambalo mnaweza
kufanya zaidi ya kusubiri maafa kama nilivyoambiwa. Mwenye akili ningemshauri
aikimbie nchi hii mapema badala ya kusubiri kifo cha kutisha cha moto mkali
utakaokuja na ufukara wa kutisha baada ya moto huo." Akaangua kicheko
kingine dhaifu. Safari hii alicheka kwa muda hata akateleza kutoka mikononi mwa
askari waliomshika na kuanguka chini. Hapo chini alitulia kwa muda kisha akapapatika
na kukata roho.
Kombora na wenzake walisogea na kuimana wakimtazama. Hakuna aliyefahamu kama alikuwa na sumu kinywani au aliitapika roho yake. "Miujiza, iliyoje!”
WALIKUWA wameitembelea miji mingi maarufu ya dunia.
Walionja anasa na starehe za kila mji. Baada ya kutoroka kutoka London kwa hima
walikwenda Ufaransa ambako walipitia miji mbalimbali na kuingia Paris. Toka
Paris walikwenda New York ambako hawakukaa sana kabla ya kuruka tena hadi
Washington, HongKong, Moscow na kwingineko.
Ingawa ziara yao ilikuwa ya starehe, lakini ilikuwa
ziara ngumu kiasi cha kumtatanisha Nuru na kumsisimua Joram. Safari zao nyingi
zilikuwa za kujifichaficha usiku na mchana kuwaepuka polisi na wapelelezi ambao
ama walimhitaji Joram kwa makosa ama kuzishuku hati zao za usafiri, ambazo mara
kwa mara zilikuwa za bandia. Hila za hali ya juu, pamoja na ruswa nzito, ni
njia pekee iliyowafanya wafanikiwe kuiepuka mitego yote ya CID, KGB, INTERPOL
na wapelelezi wa nchi mbalimbali.
Katika tukio moja kwenye mji mmoja, ilimlazimu Joram
kujifanya mwanamke malaya ili kuwaepuka polisi ambao waliizingira hoteli
aliyokuwemo. Polisi hao walipoingia katika chumba ambamo walitegemea kumnasa
Joram walijikuta wakirudi nje kwa aibu baada ya kukuta wasichana wawili,
waliofanana kwa uzuri, wakiwa nusu uchi juu ya kitanda chao kwa namna ya
kufanya mapenzi ya wao kwa wao. Wakati askari hao wakisubiri nje ili kuwahoji
vizuri, Joram na Nuru walitumia dirisha kuondoka zao na kila kilichokuwa chao.
Katika tukio jingine Joram alilazimika kuiteka nyara
ndege ndogo ya abiria na kuilazimisha kutua katika uwanja ambao haukukusudiwa
jijini New York. Kutoka uwanjani hapo walipata kinga kwa risasi za askari
walioizingira ndege hiyo kwa kuwachukua rubani na msaidizi wake huku
wakizielekeza bastola katika vichwa vyao. Polisi walikuwa wakiwafuata kwa
mbali, televisheni ikiwaona na kuwaonyesha kwa kila mtu. Lakini ilifika mahali
ambapo si polisi wala rubani waliojua kilichotokea. Polisi waliikuta ndege hiyo
ikiwa imesimama kando ya nyumba, marubani wakiwa usingizini kwa kunusa dawa
fulani bila kutaraji. Watu walioshuhudia tukio hilo, wakiwa hawajui
kinachotokea, walidai kuwa waliwaona "vijana wazuri" msichana na
mvulana wakishuka kutoka ndege hiyo na mizigo yao na kuingia katika jumba la jirani
ambamo hawakuonekana wakitoka tena.
Harakati na machachari yao katika miji mbalimbali
ziliondokea kuwa habari ambazo ziliwavutia sana waandishi wa habari. Mara kwa
mara televisheni, redio na magazeti zilitoa habari zinazowahusu; Leo kaonekana
hapa; hapa kafanya hivi; pale alifanya vile, na kadhalika.
Habari hizo zilipambwa kwa picha zao zinazovutia,
kurudiwarudiwa kwa historia ya maisha ya Joram kiango pamoja na kutiwa chumvi
nyingi ili kugusa masikio ya watu wote na kumsisimua kila mmoja. Hivyo, jina
lilipanuka na athari kuneemeka. Ilikuwa kama dunia imesita kushughulikia
masuala yaliyo muhimu na kuandamana na Joram katika ziara yake hii ndefu, jambo
ambalo lilimfanya kila mpelelezi kuwa na hamu kubwa ya kubahatika kumtia
mikononi Joram ili amfikishe kunakohusika.
Jambo ambalo lilimshangaza Neema katika mkasa huo
mzima ni jinsi ambavyo alielekea kufurahishwa na jinsi habari hizo za aibu juu
yake zilivyopata nafasi kubwa katika vyombo vya habari. Iliendelea kumfurahisha
Joram badala ya kumchukiza. Nuru ambaye alimfahamu Joram asivyopenda sifa
alijikuta akijawa na msgangao kwa mabadiliko hayo ya Joram.
Hata hivyo mshangao wake ulianza kupungua pale Joram
alipoanza au alipolazimika kumshirikisha katika baadhi ya mambo aliyokuwa
akiyafanya. Jambo la kwanza lilikuwa mazoezi ya viungo. walifanya kila starehe,
lakini baada ya starehe, wakiwa chumbani kwao, walifanya mazoezi makali ya
viungo. Mazoezi ambayo awali yalimtoa Nuru jasho, machozi na damu. Lakini baada
ya muda machozi na damu vilikoma na jasho kupungua. Akawa hodari, akiwa bega
kwa bega na Joram katika kila jambo. Zoezi la pili lilikuwa la matumizi ya
silaha mbalimbali ambazo Joram alikuwa akizinunua kwa siri sana.
Alimwelekeza Nuru namna ya kuzificha mwilini, namna ya
kuzitumia na kumfundisha jinsi ya kulenga shabaha kwa ukamilifu. Nuru alikuwa
mwepesi wa kuelimika.
Hayo yaliufanya moyo wa Nuru uwe na tumaini kubwa.
Sasa aliamini kuwa Joram alikuwa na jambo fulani zito la muhimu ambalo alikuwa
akishughulikia. Pengine katika safari hiZo za mji hadi mji alikuwa akimhitaji
mtu kwa madhambi fulani. Mtu gani huyo? Na ni madhambi gani aliyoyafanya?
Maswali ambayo yaliimarika hasa kutokana na simu
nyingi ambazo Joram alikuwa akipiga kwa rafiki zake sehemu mbalimbali
ulimwenguni, ambazo mara kwa mara zilikuwa katika mafumbo ya aina aina. Japo
alimsikiliza kwa makini Nuru hakuambua chochote cha haja, zaidi ya kuishia
kuhisi tu. Wakati wote huo Joram hakukoma kujifungia.
Halafu ikaja jioni ya leo, ambapo Joram alionekana
mtulivu kuliko ilivyokuwa siku zote. Sigara ziliteketea mdomoni mwake moja
baada ya nyingine, macho yake yakimtazama Nuru ambaye alikuwa ameketi juu ya
meza ya kuvalia akishughulikia nywele zake. Joram alimtazama kwa makini kwa
dakika kadhaa, kisha alimsogelea na kumshika bega.
"Nilichoshika hapa ni kipande murua cha kazi ya
sanaa ambayo ni mfano halisi wa kazi ya Muumba. Nadhani hana budi kujivunia
mafanikio yake", alisema akitabasamu.
Nuru aliinua uso kumtazama.
"Kwa bahati mbaya kazi hii ya sanaa iki katika
hatari ya kuharibika endapo itandelea kuandamana na binadamu wenye akili mbaya
kama Joram Kiango".
Hilo lilimfanya Nuru atabasamu. Alijua Joram anaelekea
wapi. Siku hizi mbili alikuwa akimchunguza kwa makini na kuona mabadiliko
katika fikira zake. Alikuwa akiona na kushuhudia kutoweka kwa ile starehe ya
kujisingizia katika nafsi ya Joram na badala yake starehe kamili kuchukua
nafasi yake. Mfano wa mtu ambaye yuko katika jahazi hafifu katikati ya bahari
iliyochafuka anapobahatika kufika pwani salama. Hivyo alijua kuwa Joram ana
neno. Akamhimiza kulisema kwa kumwambia, "Unachotaka kufanya Joram ni
kunitisha... Lazima uelewe kuwa sitishiki ng'oo. Tumekuwa nawe katika heri na
shari. Tutakuwa pamoja jehanamu na peponi. Usijisumbue kuniambia lolote lenye
dhamira ya kututenga".
Joram akacheka. "Una akili nyepesi sana
Nuru", akamwambia. "Nilichokuwa nikielekea kukuomba ni kukushauri
urudi nyumbani, uniachie kazi iliyoko mbele yangu. Ni kazi chafu, ya hatari,
yenye nuksi, ambayo sidhani kama itanifanya nirudi nyumbani na roho
yangu".
"Nimekwisha sema usijisumbue kunitenga. Nina hamu
na kazi nzito, chafu yenye damu. Sijasahaun nilivyoshirikishwa kuwaangamiza
wakuu wa nchi wasio na hatia. Nahitaji kujitakasa. Ni damu pekee
itakayonitakasa. damu ya adui wa Afrika.
Joram aliduwaa huku akimtazama msichana huyo. Hakuwa
na shaka kuwa msichana huyo ni shujaa. Lakini hakujua kuwa ni shujaa kiasi
hicho. Ndiyo, alimtegemea sana katika msafara wake. Lakini hakukusudia
kumwingiza katika mkasa ambao ilikuwa dhahiri kuwa pamoja na ugumu wa
maandalizi yake ya muda mrefu hadi sasa matekeo yake yalikuwa gizani. Yeye
alikuwa tayari kwenda, tayari kufanya kazi inayompeleka; uwezekano wa kurudi
haukumsumbua. Kufa kusingemtisha sana mradi atakuwa ameifanya kazi yake. Kifo
chake ni jambo moja, kusababisha kifo cha mtoto wa watu, mzuri kama Nuru, ni
jambo jingine.
"Sikia Nuru. Labda huelewi... Nakusudia kwenda
toka hapa sio nchi ya kawaida. Ni nchi ambayo kuna watu wenye kiu kubwa ya damu
ya mtu mweusi na njaa kubwa ya roho zetu. Na ninahitaji kujipeleka moja kwa
moja mikononi mwao. Kwa ufupi nategemea kwenda Afrika Kusini...".
"Tutakwenda pamoja".
...Na ninachokwenda kufanya ni hujuma. Wakinigundua
watanitafuna mbichi".
"Watatutafuna pamoja".
Joram akaduwaa. "Labda nikufunulie kila kitu
kilivyo Nuru", Joram akamwambia. ""Nisubiri", alisema
akiliendea begi lake lililokuwa limefurika kwa vitabu aina aina pamoja na
encyclopedia ambazo Joram alikuwa akizitumia kwa muda mrefu kujaribu kuyasoma
yake maandishi ya kijasusi ambayo aliyapata katika mfuko wa hayati Chonde. Humo
alitoa karatasi ndefu, iliyoandikwa kwa mashine, ikiwa tafsiri ya maandishi
hayo. Alimkabidhi Nuru na kumwabia asome haraka haraka.
0 Comments