ILIPOISHIA............
"Hata hivyo, sauti yako haifanani kabisa na madai
yako Joram. Kuna watu ambao silika yao ni kukesha katika mabaa na madansi, wewe
si mmoja wao. Kuna wanaostarehe kusubiri maafa ya kusikitisha, wewe si mmoja
wao, Joram. Kuna wanaofurahia ladha ya pombe na utamu wa muziki zaidi ya kazi
na ushujaa, wewe si mmoja wao vilevile."
"Zamani, Inspekta. Sasa hivi mimi ni mmoja wao na
nitaendelea kuwa mmoja wao. Na kama huna maongezi mengine zaidi ya haya mzee
nitashindwa kuendelea kukusikiliza," Joram alimaliza akitoa sigara yake na
kuiwasha.
Kombora hakujua afanye nini ili amshawishi Joram. Alimtazama Nuru kama aliyehitaji msaada wake. Akayaona macho yake mazuri yaliyojaa huzuni katika hali ya kukata tamaa. Hilo, kiasi lilimfariji Kombora. Alifahamu kuwa anaye msaidizi ambaye angesaidia katika juhudi zake za kumrejesha Joram Kiango katika dunia ya Joram Kiango. Akiwa si mgeni katika dunia hii Kombora alielewa kuwa mwanamke mzuri ni silaha. Hivyo, akamtupia Nuru jicho la kumtaka aelewe kuwa anautegemea msaada wake. Kisha akainuka na kuaga bila ya kumaliza kinywaji chake.
SASA SONGA NAYO...........................
"Hukufanya vizuri, Joram," Nuru alimwambia.
"Mfuate mkafanye vizuri".
"Sivyo, sikia..."
Nuru akavunjika moyo. Uchungu mkubwa ukamwingia
rohoni. Akajilazimisha kuendelea kunywa pombe, lakini haikumuingia. Baada ya
jitihada nyingi alimtaka Joram radhi, akaondoka kutangulia chumbani kwao.
"SAMAHANI, naweza kuketi hapa?" mtu mmoja
alisema akimsogelea Joram mara tu Nuru alipoondoka.
Alikuwa mtu wa umri wa kati. Sura yake ilionyesha
dalili zote za kutosheka, macho yake yakionyesha kila dalili ya kuelemika.
Kiasi alionekana kama ambaye pombe ilianza kumshinda nguvu, japo alitembea kwa
uhakika.
Joram alimtazama kwa makini kabla ya kumjibu,
"Una haki ya kukaa popote. Nchi huru hii."
"Asante," mtu huyo alijibu huku akijibweteka
kitini. Baada ya dakika mbili tatu za kunywa na kuvuta kwa utulivu alimgeukia
Joram na kumwambia, "Samahani. Sinabudi kulitoa dukuduku langu. Siku zote
nimekuwa na hamu ya kuipata fursa hii ya kuketi nawe meza moja. Kama sikosei ni
Joram Kiango." Joram alimtazama mtu huyo kwa makini. Alipochelewa kumjibu
mgeni wake aliendelea, "Tumekuwa tukikutana mara kwa mara katika majumba
ya starehe. Kilichonifanya nikufahamu ni msichana huyo mzuri unayefuatana nae.
Kwa kweli, sina budi kukupa pongezi zako. Wazuri nimewaona wengi, wa aina yake
sikupata kumwona. Ulimpataje yule dada, Joram?"
Jambo moja lilimvutia Joram katika kumsikiliza mtu
huyu. Jambo la pili lilijitokeza. Sauti. Ilikuwa sauti ya kawaida, ikizungumza
kiswahili cha kawaida katika masikio ya watu wa kawaida. Lakini katika masikio
ya Joram Kiango, Joram ambaye sasa alikuwa amekaa chonjo, sauti hiyo ilificha
uhalisia fulani.
"Unadhani una haki gani ya kunifahamu, na
kumfahamu msichana wangu hali mimi sikufahamu hata kidogo?" Alimwuliza. Kama
ambaye alilitegemea jibu hilo mgeni huyo alijibu mara moja, japo kwa
kusitasita, "Mimi! kwa jina naitwa Ismail Chonde. Ni mfanyabiashara wa
siku nyingi. Nimezaliwa na kukulia hapahapa ingawa siku hizi naishi
Nairobi."
"Na unawezaje kunifahamu kwa urahisi kiasi
hicho?"
"Nasoma vitabu, nasoma magazeti. Hakuna
asiyekufahamu Joram." Sauti iliendelea kuwa na walakini katika hisia za
Joram. "Inaelekea bado una maswali uliyotaka kuniuliza bwana Chonde.
Nataka kumuwahi huyo msichana unayemwita mzuri".
"Kweli. Inaonyesha aliondoka hapa akiwa
amechukia."
Joram alitabasamu. "Naona umeona mengi zaidi ya
hilo."
"Ndiyo, nimeona na kusikia mengi. Kwa kweli,
endapo hutaniona mlevi, nilichokusudia kuongelea ni yule mzee aliyekuacha muda
uliopita. Namfahamu yule. Ana madaraka makubwa serikalini. Kama sikosei alikuwa
akikushawishi utoe mchango wako katika kupeleleza matukio haya. Na niliona
akiondoka bila furaha. Yaelekea umemkatalia. Hivi kweli umekataa
katakata?"
Joram alimtazama kwa makini zaidi. "Sielewi
maswali yako yanaelekea wapi," baadaye alisema.
"Inashangaza," Chonde aliongeza. "Joram
ninayemfahamu mimi hawezi kuipoteza nafasi nzuri kama hii ya kuonyesha ushujaa
wake. Afrika iko katika mashaka makubwa. Watu wanakufa hovyo. Majumba
yanalipuka hovyo. Bara zima liko mashakani. Joram ninayemfahamu mimi angeitoa
hata roho yake kujaribu kupambana na hali hii."
Joram aliipima sauti hiyo, akiilinganisha na uso wa
msemaji. Ingawa aliongea kama mtu mwenye uchungu kwa nchi na bara lake, bado
hisia fulani zilimfanya Joram aone kitu kama kebehi katika macho yake, kama
kwamba alikuwa na hakika kuwa Joram na U Joram wake wote asingeweza kufanya
lolote. Wazo hilo lilimuongezea Joram hamu ya kuendelea kumsikiliza.
"Bado sijaelewa unalotaka kusema,"
alichochea.
"Sidhani kama wewe ni mzito wa kuelewa kiasi
hicho."
Wakatazamana, kila mmoja akimsoma mwenzake. Kisha
Chonde aliangua kicheko kirefu kilichomwacha Joram akitabasamu. Baada ya
kicheko hicho akaongeza, "Samahani endapo umeniona mhuni au mlevi. Sikuwa
na nia mbaya zaidi ya kuzungumza nawe na kufahamiana. Kwa kheri." Aliinuka
na kuondoka akielekea maliwatoni. Mwendo wake ulikuwa wa kilevi zaidi ya sauti
yake. Joram aliendelea kunywa taratibu. Alipomwona rafiki yake huyo mpya
akitoka nje ya hoteli na kusikia mlio wa gari likiondoka, akaenda mapokezi
ambapo alimsalimu tena msichana aliyekuwa hapo na kumuuliza kwa upole,
"Samahani dada. Hivi huyu bwana aliyetoka sasa hivi anakaa hoteli
hii?"
"Yule, hakai hapa. Huwa anatokeatokea tu. Kila
mara huja na msichana. Leo ndio kwanza nimemwona peke yake. Sijui wamekosana
nini na msichana huyo, maana huyu bwana anaonekana pesa si moja kati ya
matatizo yake," msichana huyo alieleza.
"Pengine hawajakosana," Joram alimchokoza.
"Wamekosana. Bila hivyo asingenikonyeza mara
mbili."
Joram alicheka. Maongezi hayo yalikatizwa kidogo kwa
simu ambayo msichana huyo alikuwa akiijibu. Alipotaka kuanza tena maongezi
iliingia simu nyingine. Ambayo msichana huyo alionekana kuifurahia zaidi.
Alizungumza kwa furaha huku akitabasamu. Baada ya kutoa chombo cha kuongelea alimgeukia
Joram na kusema, "Unaona? Nimekwambia leo hana mtu. Ananiambia nikimaliza
kazi nimkute hoteliya New Africa, chumba namba 104."
"Ndipo anapokaa?" Joram alihoji.
"Bila shaka."
Baada ya mazungumzo hayo Joram aliirudia meza yake na
kuendelea kunywa. Mawazo yake yalimfikiria Chonde. Hakuelewa dhamira ya
maongezi yake yote yale ilikuwa nini hasa. Alishuku kuwa pengine alikusudia
kupata undani wa Joram na uamuzi wake. Kwanini? Zaidi Joram alishuku kuwa mtu
huyo hawakukutana kuzungumza kiajaliajali, bali alikuwa akimfuata yeye au
Kombora kwa ajili hiyo. Juu ya yote hayo zile hisia za Joram katika sauti ya
mtu huyo zilizidi kujiimarisha akilini mwake. Aliona kama ulikuwemo walakini fulani
katika sauti ya kiswahili chake ambao uliutia dosari Utanzania wake. Hayo na
kile alichoona katika macho ya mtu huyo vilimtia Joram hamu ya kumfahamu
vizuri.
Hivyo, dakika tano baadaye alijikuta mitaani akielekea
New Africa. Alipofika hapo alimwendea mfanyakazi wa mapokezi na kujitia
akizungumza naye hili na lile huku macho yake yakiwa kazini kutazama endapo
ufunguo wa chumba namba 104 ulikuwepo. Aliuona. Akauliza juu ya mtu wa chumba
fulani ambacho aliona ufunguo wake haupo.
"Yuko ndani. Ameingia sasa hivi."
"Ngoja nikamwone."
Badala ya kwenda chumba hicho, Joram alipanda gorofani
hadi chumba namba 104 ambacho kilikuwa kimefungwa. Kuacha kwake tabia ya
kutembea na bastola hakukumfanya aache kutembea na vifaa vyake vidogovidogo,
kama funguo malaya ambazo hazishindwi kuifungua kufuli yoyote ya kawaida.
Hivyo, kitasa hicho cha mlango wa Chonde kilimpotezea nusu dakika tu.
Chumbani humo, Joram aliurudisha mlango na kuufunga
kwa ndani. Kisha aliangaza huku na huko kwa makini. Kilikuwa chumba cha kawaida
kama vilivyo vyumba vingine vya hoteli. Hivyo, Joram hakuwa na kazi ngumu zaidi
ya kupekuwa magodoro na viti. Hakuona chochote. Ndipo alipoliendea Kabati na
kulifungua. Ndani ya kabati hilo mlikuwa na sanduku kubwa ambalo pia Joram
alilifungua. Mlikuwa na pesa za kutosha pamoja na mavazi. Vitu hivyo
havikumvutia. Macho yake yalivutiwa na makaratasi mbalimbali ambayo aliyapekua
kwa makini. Mengi yalikuwa makaratasi ya kawaida ambayo yalimwezesha kumfahamu
mtu wake kuwa aliitwa Afith Chonde. Baada ya kupekuwa zaidi aliipata hati yake
ya usafiri. Aliifunua harakaharaka huku akisoma mihuri mingi iliyopigwa katika
hati hiyo kuonyesha nchi Chonde alizozitembelea. Alikuwa anatembea sana. Mihuri
ya Nairobi, Lagos, Lusaka, Harare, London, New York, Hong Kong, Tripol n.k ilionekana
waziwazi. Hilo lilimfanya Joram azidi kuvutiwa na mtu huyo. Hakuonekana kama
mfanyabiashara mkubwa kiasi hicho. Zaidi ya vipindi alivyokuwa akitumia mji
hadi mji vilikuwa vifupi mno kiasi kwamba Joram alishuku kuwa hakuwa akifanya
biashara za kawaida. Hivyo, akaongeza umakini katika upekuzi wake.
Kama alivyotegemea, Joram aliigundua mifuko ya siri
katika begi hilo, mifuko ambayo maafisa wa forodha wasingeweza kuipata bila ya
ujuzi maalumu. Katika mifuko hiyo, Joram alipata bastola moja aina ya revolver,
maandishi mbalimbali ambayo alijaribu kuyasoma hakagundua kuwa hawezi kwani
yaliandikwa kimafumbomafumbo katika hali kamili ya kijasusi. Pamoja na kijaluba
kidogo cha chuma ambacho kilikuwa kimefungwa kwa ufunguo. Kijaluba hicho
kilimvutia Joram zaidi. Alihisi kuwa kilikuwa kimeficha mengi zaidi ya yale
aliyokwishayaona. Hivyo, akaanza kuzijaribu funguo zake malaya. Zilimchukua
dakika kadhaa kugundua kuwa kamwe asingeweza kukifungua kijisanduku hicho.
Kilitengenezwa maalumu kupambana na hila zozote za kufunguliwa pasi ya utaalamu
wa mwenyewe. Kiu ya Joram juu ya kumjua vyema mtu huyu ikazidi kuneemeka.
"Vipi awe na kisanduku kama hicho? Kilificha nini? Na maandishi haya ya
siri yanasema nini? Siyo bure. Liko jambo," aliropoka.
"Ndiyo. Kuna jambo," sauti ilizungumza nyuma
ya Joram. Akageuka hima na kukutana na uso wa Chonde ambao ulikuwa ukimtazama
kwa kebehi. Alikuwa kaketi juu ya kochi. Alivyoingia chumbani humo kwa ukimya
kama jini na kuketi kwa utulivu kwa kipindi chote hicho ni jambo ambalo lilizidi
kumwongezea Joram ushahidi kuwa alikuwa hachezi na binadamu wa kawaida. Joram
akageuka na kumtazama Chonde huku akiruhusu moja ya zile tabasamu zake za
kishujaa, tabasamu ambalo lilifuatwa na sauti yake tulivu akisema, "Tuseme
nimefumaniwa".
"Umefumaniwa. Na una bahati mbaya kuwa
umefumaniwa na kifo. Binadamu hanichezei mimi na akaendelea kuishi,"
Chonde alisema akianza kuinuka taratibu. "Ulijifanya umeacha maisha yako
ya kuingilia mambo yasiyokuhusu. Kumbe ulikuwa ukijifurahisha kwa kujidanganya
mwenyewe. Umekosea sana." Akamtazama kwa dharau na kebehi. "Huwa
nafurahia zaidi kuwaua watu wangu kwa mikono," alisema akizidi kusogea.
Mzaha haukuwemo katika macho na sauti ya Chonde.
Alionekana mtu anayejua anachokifanya, jambo ambalo lilimfanya Joram asogeze mkono
kuiendea ile bastola ambayo ilikuwa imelala kando yake. Kama alikuwa ameuhisi
wepesi wa Chonde basi alikuwa hajauona. Mara tu mkono huo ulipoifikia bastola
tayari mguu wa Chonde ulitua juu ya mguu huo. Wakati huo huo Joram alipokea
ngumi mbili ambazo zilizomfanya apepesuke na kuisahau bastola. Chonde hakuwa na
roho mbaya kiasi hicho. Alimpa muda wa kujiandaa. Joram akavuta pumzi kwa nguvu
na kuanza kumwendea Chonde. Alimshitua kwa mkono wa kulia, Chonde aliudaka na
wakati huohuo kumkata Joram judo ya mgongo ambayo ilimfanya aanguke kifudifudi.
Alipoinuka Chonde alikuwa akimsubiri huku akicheka, "Wanasema Tanzania
kuna mtu mmoja tu wa kujihadhari nae, ambaye anaitwa Joram Kiango. Niko naye
chumbani, sioni Ujoram wake."
Maneno hayo yalimwuma Joram zaidi ya kipigo
alichopokea. Akainuka ghafla na kumwendea Chonde akitumia mitindo yake yote ya
kupigana. Vipigo kadhaa vilimpata Chonde. Lakini kwa jinsi vipigo hivyo
vilivyopigwa kwa hasira havikuwa na madhara makubwa kwa Chonde. Dakika chache
baadaye Joram alijikuta chali sakafuni, kasalimu amri. Chonde akaendelea
kutabasamu.
Sasa Joram alimtazama Chonde kwa mshangao zaidi ya
hasira. Ni mtu wa aina gani huyu anayeweza kumwadhibu kama mwanae? Bila shaka
si mtu wa kawaida. Amejifunza mengi kama anavyoonekana kujua mengi. Pamoja na
kwamba kipindi kirefu kilikuwa kimepita bila ya Joram kufanya mazoezi ya viungo
wala akili, pamoja na kule kuzoea starehe za mahotelini na ulevi mwingi, bado
hakuona kama binadamu yeyote angekuwa na haki au uwezo wa kumfanya apendavyo kama
Chonde alivyokuwa amemfanya.
Ile hamu iliyokuwa imelala usingizini ikaibuka upya
katika moyo wake, hamu ya mapambano, vitisho, maafa, damu, na mikasa, hamu ya
kuwatia adabu watu wanaopenda kuwafanya vibaya binadamu wenzao. Chonde
alionekana kama mmoja wao. Joram akamtazama tena na kutabasamu kwa uchungu huku
akisema, "Haya, umeshinda. Kinachofuata?"
"Kifo chako," Chonde alimjibu kijeuri.
"Siwapendi vijana watundu kama wewe. Kufa, huna budi.”"Kosa
langu."
"Unapenda
kufa?"
Joram alifikiri kwa makini angefanya nini kuiahirisha
hukumu hiyo ya kifo. Muda. Alihitaji muda ili ikiwezekana itokee njia moja au
nyingine ya kuyaokoa maisha yake. Akaanza maongezi kwa sauti ambayo aliifanya
dhaifu kuliko ilivyokuwa, akimwuliza Chonde hili na lile. Chonde alikuwa mgumu
wa kutoa habari kama jabali. Kati ya maneno ya kashfa na matusi kwa Joram, nchi
na bara zima hakutamka neno lolote ambalo lilimfanya Joram amjue yeye ni nani
na anafanya nini katika ulimwengu wa ujasusi. Alichoambulia ni zile hisia tu
kwamba Chonde hakuwa raia wa kawaida.
"Umeahirisha sana kifo chako," Chonde
alisema baadaye kama aliyekuwa akizisoma fikra za Joram. “Sasa iliyobaki ni
kazi ndogo ya kukutoa uhai. Nitakuua kwa mkono wangu wa kushoto. Maiti yako
itaokotwa kesho ikiwa imevunjikavunjika kama mtu aliyeanguka toka ghorofani.
Kwa jinsi ulivyobadilika kitabia watu hawatashangaa kusikia kuwa umejirusha
dirishani.”
Baada ya maneno hayo, aliinuka na kumwendea tena Joram
kwa utulivu kama awali, lakini macho yake yalitangaza kitu kimoja tu, kifo.
Joram alijiandaa, akijua kuwa vita vilivyokuwa mbele
yake vilikuwa vikubwa kuliko vyote alivyowahi kupambana navyo, vita vya
kuitetea roho yake. Akaikusanya akili yake yote na kumsubiri Chonde kishujaa.
Mara mlango ukagongwa.
Chonde aligutuka kwa mshangao na kuutazama mlango huo.
Joram hakuipoteza nafasi hiyo. Aliruka na kuufanya mguu wake utue katika shingo
ya Chonde. Lilikuwa pigo ambalo Chonde hakulitegemea. Likamtia mweleka. Lakini
pigo la pili alilitegemea, akalikwepa na kuachia judo ambayo Joram aliikinga. Papo
hapo mlango ukagongwa tena na kufunguka ukiruhusu sura ya msichana mzuri
kuingia.
Alikuwa yule msichana wa mapokezi wa hoteli ya
Embassy. Alitokwa na macho ya mshangao kuona miili yenye jasho, michubuko na
damu, ya wanaume hao, ikiwa tayari kuvamiana. Wote walimtazama msichana huyo,
Chonde akimlaani, Joram akimshukuru. Akiwa kama hajui lipi la kufanya msichana
huyo aliduwaa mlangoni, Mdomo wazi.
"Karibu ndani. Tulikuwa tukifanya mazoezi ya
viungo na huyo rafiki yangu," Chonde alimhimiza akivaa tabasamu ambalo
lilificha kabisa mauaji yaliyokuwa katika uso huo dakika iliyopita.
"Karibu ndani. Nawe ndugu yangu nenda zako sasa. Tutakutana siku
nyingine".
Joram aliyarekebisha mavazi yake na kutoka chumbani
humo taratibu. Hakuwa amesahau kumwachia msichana huyo tabasamu jingine la
shukrani.
********
"Nadhani hakuna njia nyingine zaidi ya
kumlazimisha," Kombora alikuwa akifoka katika kikao cha dharura
kilichofanyika usiku huo. "Hawezi kuachwa aendelee kustarehe katika mabaa
huku taifa na bara zima likiwa mashakani. Mchango wake unahitajika."
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wote wa ngazi za
juu katika idara zote za usalama nchini. Kiliitishwa ghafla baada ya kuokotwa
barua moja ya vitisho katika ofisi ya Waziri Mkuu, barua ambayo iliandikwa kwa
ufupi sana ikidai kuwa ajali za kimiujiza zingeendelea kuipata nchi ya Tanzania
na zote zilizo mstari wa mbele, endapo serikali isingechukua hatua za haraka
kukomesha msimamo wake wa kupinga utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Barua
hiyo iliongeza kwamba safari hii moto ungeiteketeza hospitali ya Muhimbili,
hoteli ya Kilimanjaro, Jengo la Kitega Uchumi na baadae Ikulu.
Aliyeiokota barua hiyo na kuisoma aliwaonyesha wakubwa
wake ambao waliikabidhi kwa Waziri Mkuu. Baada ya kuisoma yeye pia, alikwenda
Ikulu ambako alimpa Rais.
"Upuuzi ulioje huu. Hatutaacha kuwatetea ndugu
zetu wanaoteswa bila makosa kwa ajili ya vitisho hivi. Havikuanza leo. Wala
haviwezi kwisha leo. Tutapigana hadi mtu wetu wa mwisho katika kuilinda hadhi
ya mtu mweusi katika bara letu hili." Pengine Rais alijibu hivyo akifoka
kwa hasira. "Barua hiyo wakabidhi watu wa usalama. Nadhani hawatakubali
kuendelea kuchezewa kiasi hiki. Waambie kwamba hatutaki upuuzi wowote
ulioandikwa katika waraka huu haramu utokee." Huenda Rais aliongeza hayo.
Hakuna aliyeshiriki katika maongezi yao ya faragha,
isipokuwa hisia hizo zinakuja kwa jinsi Waziri Mkuu alivyomwita Inspekta
Kombora katika ofisi yake na kumkabidhi barua hiyo. Baada ya Kombora kuisoma
kwa makini Waziri Mkuu alimwambia, "Ni barua ya khatari sana. Na imeandikwa
na watu khatari, watu wenye kichaa. Kufuatana na hali ilivyo hatuwezi kukubali
kuwa watumwa au mateka wa Makaburu kwa kuhofia ukatili wa vitisho vyao. Lazima
tupambane nao ana kwa ana kama tunavyopambana nao katika uwanja wa mapambano.
Tuliwashinda Msumbiji, Angola na Zimbabwe. Kwa nini tusiwashinde Namibia na
Afrika Kusini? Tutawashinda. Wao wanajua hivyo, ndiyo sababu inayowafanya
wakimbie toka katika uwanja wa mapambano na kuja huku kupigana kiuoga."
"Kama tulivyoshuku kitambo, mikasa hii haikuwa ya
kawaida. Kulikuwa na mkono wa mtu, mkono wa mtu huyu ambaye ameandika barua hii
na kuthubutu kuipenyeza katika ofisi yangu. Ingawa haijafahamika mbinu gani
wanatumia kuweza kuanzisha mioto hii, nadhani hutashindwa kufanya juu chini ili
uugundue na kuukomesha kabisa upuuzi huu."
Akijua uzito wa jukumu hilo ndipo Kombora aliporudi
ofisini na kuitisha kikao hiki kilichokuwa kikiendelea. Walijadiliana kwa
mapana na marefu kulikuwa na nini hasa hata majumba yalipuke moto ilihali
uchunguzi kamili ulionyesha kuwa haikuwepo kasoro yoyote ya umeme. Hawakupata
jibu. Walijaribu kuzijumuisha taarifa zote za upelelezi juu ya nani anaweza
kuwa alihusika katika kusababisha mioto hiyo lakini bado hazikuwepo dalili
zozote zilizoleta matumaini. Wakapanga mipango mipya. Wakawaandaa wapelelezi na
vyombo kadha wa kadha katika majumba yaliyotajwa. Wakawekwa watu katika
mahoteli, viwanja vya ndege na vituo vyote vya usafiri kuchunguza nani
anaingia, nani ametoka na ameleta nini. Zaidi ya yote hayo, ndipo lilipotolewa
tena pendekezo la kumshirikisha kila mtu mwenye uwezo wa kuchangia katika
upelelezi. Hapo ndipo jina la ‘Joram’ lilipowatoka midomoni. Ikawashangaza
wajumbe kusikia kuwa hata baada ya kuombwa na Kombora alikataa katakata
kushiriki katika kazi hiyo. Joram waliyemfahamu alikuwa hangoji kuombwa au
kutumwa bali alijituma. Vipi Joram huyu?
Ndipo mzee Kombora alipoibuka na uamuzi wa
kumshurutisha. "Lazima tumlazimishe. Kama ameacha upelelezi kwa ajili ya
mwanamke, basi atarudia upelelezi kwa ajili ya mwanamke. Yote hayo niachieni
mimi," Inspekta Kombora aliwaambia.
Baada ya kikao hicho, alimchukua msaidizi wake mmoja
na kumpeleka chemba. "Sikia," akamweleza, "Nakutaka uwe msiri
wangu, wewe peke yako. Unaweza kutunza siri?"
"Bila shaka. Isipokuwa ya wizi na mauaji
tu."
"Hii si ya mauaji wala wizi. Nataka unisaidie
kumteka mtu nyara."
"Kuteka mtu nyara? Hiyo mbona haiko mbali sana na
wizi? Na kama sikosei ni hatari zaidi ya wizi."
"Ndiyo. Lakini mtu tunayemtaka atafurahi sana.
Bado ni msichana mzuri sana," Kombora alivuta pumzi kwa nguvu kisha
akaongeza, "Nataka tumteke yule msichana wa Joram. Hiyo ndiyo njia pekee
ya kumlazimisha."
Baada ya kujadiliana kwa muda walielewana. Wakaandika
barua ambayo ilikusudiwa iwe imetoka kwa mteka nyara akidai kuwa amemteka
msichana huyo na angemwua endapo Joram angethubutu kujihusisha na upelelezi
unaoendelea nchini dhidi ya maafa ya kutatanisha. Licha ya barua hiyo, pia
waliandaa damu ambayo ilipatikana kwa msaada wa daktari mmoja wa hospitali yao
Ocean Road ili waidondoshe chumbani humo kuonyesha kuwa kulikuwa na mapambano
ambayo yalisababisha damu kumwagika.
"Tunacheza mchezo mchafu sana, mchezo wa aibu.
Lakini hatuna budi," Kombora alisema baada ya matayarisho yote ya kwenda
katika chumba cha Joram.
Uchunguzi uliwapa fununu kuwa Joram alikuwa akiishi
katika hoteli hiyo ya Embassy. Habari za mwisho usiku huo zilieleza kuwa Joram
alipoachana na Kombora usiku huo alikuwa peke yake akinywa bia wakati msichana
wake alipoondoka kwenda chumbani, na kwamba baada ya muda mrefu Joram
alionekana akitoka nje na hadi sasa alikuwa hajarudi. Kombora alitegemea kuwa
muda huo ulitosha kumfikia msichana huyo, kumshawishi na akikataa, kumlazimisha
kisha kuondoka naye kwa siri kabla Joram hajarudi.
Walifanya hivyo.
Waliifika hoteli na kukiendea chumba chake kwa siri
kubwa. Mlango waliukuta ukiwa wazi. Wakaufungua na kuingia huku wakiufunga
nyuma yao. Macho yao yalivutwa na dalili za vurugu katika chumba hicho. Vitu
vilikuwa vimetupwa ovyoovyo, matandiko yakiwa yamepinduliwa na masanduku
kufunguliwa. Juu ya meza kulikuwa na karatasi yenye damudamu. Upande wa pili wa
karatasi hiyo kulikuwa na maandishi ambayo yalikuwa barua ya wazi kwa Joram
Kiango, barua ambayo haikutofautiana sana na ile ambayo Kombora aliiandaa: Ndugu
Joram,
Tunayo furaha kukufahamisha kuwa tumemchukua msichana
wako na tutakuwa nae hadi hapo tutakapomaliza shughuli zetu. Hii ni kwa ajili
ya kukuonya usithubuti kujihusisha na mambo yoyote yanayoitokea nchi hii.
Endapo utakuwa mtoto mtiifu kama ulivyo siku hizi, hatadhurika, nawe utakuwa
salama. Vinginevyo, utakipokea kichwa chake kwa njia ya posta na kisha
kitafuata kifo chako.
Amri
Kombora aliisoma tena barua hiyo, kisha akamgeukia
msaidizi wake na kumnong'oneza, "Tumechelewa sana. Wenzetu
wametuwahi." akampa barua hiyo ili aisome.
"Sasa tutafanya nini?" askari huyo aliuliza
baada ya kuisoma.
"Rudisha kila kitu kama kilivyokuwa. Fanya hima
tuondoke hapa haraka," alimhimiza akianza kusogea mlangoni.
"Nilidhani tungemsubiri Joram!"
"Hakuna haja. Akirudi atajua la kufanya."
Wakatoka na kuifuata njia ya kawaida. Wakiwa katika mavazi ya kiraia, watu
wachache sana waliwatupia macho zaidi ya mara moja. "Jambo moja la
kupendeza ni kwamba," Kombora alikuwa akisema. "Wamemchokoza Joram.
Hawamfahamu vizuri. Wataujutia uamuzi wao"
0 Comments