![]() |
YUL EDOCHIE & MAY EDOCHIE |
Kuna, Asubuhi, Mchana na Usiku. Nyakati zote hizi
zinapotokea lazima kuna matukio mengi sana yametokea katika nyakati zote hizo.
Wapo waliolia, wapo waliocheka, wapo waliozaliwa na wapo waliokufa. Wapo
walioachana na wapo waliooana, hivyo ndivyo ilivyo na lazima dunia izunguke
katika mhimili wake.
Kama wewe ni mfuatiliaji wa filamu za Nigeria utakuwa
umekutana na taarifa nyingi sana zinazomhusu mwigizaji maarufu nchini humo na
Afrika kutoka katika kiwanda cha filamu kiitwacho Nollywood. Wahenga walisema
vya sirini ipo siku vitamulikwa. Mwaka 2022 mwishoni, muigizaji huyu alikuwa
katika vichwa vya habari vya magazeti, mitandao na blog zote za burudani baada
ya kuibuka taarifa kuwa alikuwa katika mahusiano ya siri na mwigizaji mwenzake
aitwaye Judy Austin tangu mwaka 2012. Taarifa hizi zilifuatiwa na taarifa
nyingine kuwa Yul Edochie ambaye ni mtoto wa mmoja wa magwiji wa filamu pale
Nollywood Pete Educhie, tayari mahusiano hayo yameleta mtoto wa kiume.
Taarifa hizi ziliwafanya Yul na Judy kuwekwa kikaangoni na
mashabiki zao ambao walikerwa na kitendo chao hicho. Wapo walimshambulia Yul
kwa kumuumiza mkewe, May Yul Edochie ambaye amekuwa naye tangu akiwa
underground actor hadi sasa amepata mafanikio makubwa katika kiwanda hicho na
tayari wana watoto wanne, Kambi Edochie, Dani Edochie, Karl Edochie na Victory
Zane Chukwubuike Edochie. Judy alikuwa na wakati mgumu zaidi kwani mashabiki
zake walimuita majina yote ambayo waliamini anastahili. Mashabiki hao na
waigizaji wenzake walimtaja kama mwanamke ambaye kazi yake ni kuvunja ndoa za
wenzake baada ya ndoa yake mwenyewe kumshinda.
Baadaye Yul Edochie alitupia picha zake na za mtoto wake
wakiume ambaye alizaa na Judy. Yul aliamua kumuoa Judy na kuwa mke wa pili
kitendo kilichozidi kuwachefua wananzego na kuhatarisha ndoa yake na mahusiano
na familia yake. Baba wa Yul Edochie, Mzee Pete Edochie alipoulizwa na
mwandishi mmoja alikaririwa akisema kuwa maamuzi ya mwanaye huyo wa mwisho
yalimfanya ajisikie vibaya.
Wakati wote huo mke wa Yul Edochie, Bi. May Edochie alikuwa
mkimya na mstahimilivu japo wambea walikuwa hawanywi maji yakapita vizuri kooni
kwa kuwa muda wote walitaka kusikia Bi. May atasema nini. Lakini uzalendo
ulimshinda baada ya mumewe kumu-unfollow kwenye mtandao wa Instagram, Bi. May
aliandika, “Mungu anaona yote.”
Ni ukweli usiofichika kuwa Yul Edochie ni moja ya waigizaji
wanaofuatiliwa sana na wanahabari na mashabiki wa filamu Nigeria na Afrika kwa
ujumla wake, lakini maisha yake yaliongezewa umakini mkubwa na wanahabari.
Chochote alichofanya mitandaoni kiliandikwa kwenye blogs na majarida ya
burudani nchini humo.
Matarajio ya wengi waliamini kuwa Yul na May wataachana
wakibet kuwa May hawezi kuvumilia kuletewa mke wa pili. Naweza kusema kuwa
mkeka wao ulichanika kwani May na Yul Edochie waliendelea kuwa pamoja na Mwezi
September mwaka jana Yul alionekana akimsupport mkewe ambaye ni mjasiliamali
katika shughuli ya kurudisha kwa jamii wakati akizindua Foundation yake iitwayo
Oasis.
![]() |
JUDY AUSTIN |
Drama zikaendelea na ikawa zamu ya Judy ambaye alibadili
jina lake la mwisho kutoka Judy Austin Muoghulu na kuwa Judy Austin
Yul-Edochie! Hilo lilimfanya aongeze wafuasi katika mtandao wa Instagram kutoka
156K hadi 233K!
𝗠𝗔𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗬𝗔
𝗝𝗨𝗗𝗬
𝗔𝗨𝗦𝗧𝗜𝗡
𝗛𝗔𝗗𝗜
𝗞𝗨𝗞𝗨𝗧𝗔𝗡𝗔
𝗬𝗨𝗟
𝗘𝗗𝗢𝗖𝗛𝗜𝗘
Kuna kale kamsemo kanasemwa sana hasa kuwaeleza wanaume kuwa
"mchumba hasomeshwi." Wakati mtifuano wa ndani kwa ndani kati ya Yul
na Mkewe wa kwanza, mume wa zamani wa Judy akafunguka kuhusu mwanzo hadi mwisho
wake na mkewe wa zamani ambaye kwa wakati anazugumza tayari Judy alikuwa mke wa
pili wa Yul Edochie. Mume huyo wa zamani wa Judy aitwaye Mr. Obasi alifunguka
kuwa Judy akiwa na miaka 19 na yeye akiwa na miaka 29, walianza kuishi pamoja
kwa kuwa Judy alipata ujauzito.
Akajifungua mtoto wao wa kwanza wa kike, mwaka 2007. January
18, 2009 wakapata mtoto wa pili. Mr. Obasi akapendekeza kwa Judy kuwa inabidi
akajifunze kufanya biashara kuliko kukaa tu bila kuwa na kitu chochote cha
kufanya. Judy akakataa na kusema kuwa anataka kurudi shule. Mr. Obasi akamlipia
Judy ili akafanye mtihani wa kuingia chuoni lakini hakufanya vizuri. Mr. Obasi
akatumia Naira 500 sawa na Tshs. 2,551 kupata collage iitwayo Institute of
Management and Technology (IMT) kilichopo Enugu nchini Nigeria.
Judy akasoma kwa muda mfupi tu kwenye chuo hicho kisha
akaacha! Mr. Obasi hakumkatia tamaa mama wa watoto wake, akamlipia tena Naira
100,000 sawa na Tshs. 510,348 Judy akaishia katikati, Mr. Obasi akalipa tena
Naira 300,000 sawa na Tshs. 1,531,044 lakini Judy akagoma kabisa kuendelea na
chuo na ukumbuke kuwa yeye ndiye aliyetaka kurudi shule.
Mr. Obasi kwakuwa alikuwa anampenda sana mama watoto wake
akamuuliza, “Unataka kufanya nini?” Judy akajibu anataka chuo kikuu. Hatimaye
ombi lake likakubalika kwa Mr. Obasi na Judy akaingia chuo baada ya jamaa huyo
kutoa rushwa.
MATATIZO YANAANZA
YUL EDOCHIE, MR. OBASI & JUDY AUSTIN |
Judy alipokuwa anaingia chuoni ntayari alikuwa amefunga ndoa na Mr. Obasi na hapo ndipo kimbembe kikaanza. Judy akiwa chuo akakutana na Yul Edochie mwaka 2012. Wawili hawa wakaazimia kuanzisha mahusiano, mume wa Judy akagundua hilo na kwenda kutoa taarifa kwa wazazi wa Judy. Kikao kikaitishwa na wazazi wa Judy kisha akaulizwa juu ya tuhuma hizo, Judy akakana kwa sauti kuu kuwa hana uhusiano na Yul na akadai kuwa anampenda sana mumewe. Mgogoro ukasuluhishwa na wakarudiana lakini siku moja mume wa Judy akawafuma wakiwa pamoja kwenye mkutano ulioashiria kuwa watu hao wako na mahusiano. Mr. Obasi alikuwa anampenda sana mkewe na hakuwa tayari kuachana na mkewe kwakuwa pia wanawatoto wawili hivyo hakutaka kuwaumiza watoto wake hivyo akaamua kumsamehe.
Mr. Obasi akiwa hana hili
wala lile, mkewe akamwambia anataka mapangie chuma huko Enugu kwakuwa walikuwa
wanaishi Onitsha. Mumewe akamuuliza, “Kwanini unataka kuhamia Enugu wakati
tumejenga na kuwekeza hapa? Kwanini unakuwa msumbufu namna hii, kila kitu
nimefanya kwako, ulitaka kurudi shule nikalipa pesa ukafail, nikatia rushwa
uingie collage ukaishia njiani, nikatoa rushwa ukarudi collage ukakomea njiani.
Ukasema unataka chuo, hukua na sifa nikatoa rushwa ukaingia chuo sasa uko mwaka
wa pili nalipa ada, vitabu na kila kitu sasa unataka nikupangie nyumba!”
Mwanamke huyu alikuwa amedhamiria na kwakuwa alikuwa anajua jamaa anampenda,
akamjibu, “Utachagua kunipangia nyumba au nikuache.”
Tarehe 25 December 2012
Mr. Obasi akamuomba mkewe waongozane kwenye sherehe za krismas, Judy akakataa.
Mr. Obasi akaona isiwe tabu, akaenda mwenyewe kwenye sherehe ambako alialikwa
Mara baada ya sherehe, akarejea na kukuta nyumba iko tupu, hakuna kitu wala
mtu. Akapiga simu kwa mkewe haikupokelewa na baadae ikazimwa, alipouliza
majirani, wakampa taarifa ambazo ziliuvunja moyo wake vipande vipande. Majirani
walimweleza kuwa ilikuja gari ya mizigo na gari ndogo SUV ambayo ilikuwa
inaendeshwa na Yul Edochie, wakapakia vitu na kisha wakaondoka. Mr. Obasi
akaenda kutoa taarifa kwa wazazi wa Judy lakini akajibiwa kuwa hawana cha kufanya
kwakuwa Judy si mtoto ambaye anasikia chochote, akapewa pole na kushauriwa
kupiga moyo konde na kuendelea na maisha yake.
Mr. Obasi anasema
alimshukuru kwa uhai na akaendelea kuhudumia watoto wake lakini baadaye Judy na
Yul Edochie walimkatia mawasiliano yake na watoto wake. Baada ya muda mrefu
kupita alipigiwa simu na watu wa Judy kuwa Yul anakwenda kutoa mahari, na
kuulizwa yeye anamsimamo gani?
Mr. Obasi akawajibu kuwa
yeye alishaendelea na maisha yake na kwakuwa mke wa Yul amekubali mumewe kuoa mke
mwingine yeye nani hata azuie? Ombi lake likawa kurudishiwa watoto wake awalee
lakini hakupata msaa wowote. Akaamua kupeleka malalamiko yake kwenye shirika la
Onitsha Human Rights, Hakupata msaada. Akapeleka kwnye shirika la Ogidi Welfare
lakini kote huko hakukuwa na majibu.
MAY EDOCHIE
![]() |
MAY EDOCHIE |
Kabla ya Yul kumuoa Judy, May, aliweka msimamo wake kuwa hatokuwa tayari kuwa kwenye ndoa ya mume mmoja wake wawili. Baada ya siku na wiki kadhaa, Yul Edochie alijitosha mtandao na kumuomba radhi mkewe kwa mambo yote aliyomfanyia na kwamba chochote alichomfanyia hakukifanya kwa lengo la kumuumiza. Yul akaendelea kujitetea kuwa yeye si mkamilifu hivyo amsamehe na waendelee kuishi kwa amani. Baada ya ujumbe huo wa Yul Edochie akimuomba Msamaha, mkewe akajibu kwa njia ile ile ya mtandao kupitia akaunti yake ya Instagram May Edochie aliandika kuwa, “Makosa ni sehemu ya uwepo wa binadamu. Tunawajibika katika makossa yetu. Kwamaneno mengine, msamaha ni jambo moja na kusahihisha makossa ni jambo jingine.”
May akaendelea, “MSAMAHA
ni jambo zuri sana kwangu na ni ishara ya upendo. Hakuna Upendo kama hakuna
msamaha na kwa kuwa uamuzi wangu wa kusamehe makosa yaliyopita, ya sasa na ya
baadae na kwa heshima ya jambo lililopo linahusu afya yangu ya akili na amani
ya moyo”
Maya akaongeza, “Nimeamua
kusimama na upendo, Chuki si jambo zuri na siko tayari kutengeneza chuki kwa
mtu yeyote. Ukweli utabaki kuwa mtu yoyote anaweza kuchagua kuwa kwenye ndoa ya
wake wengi mume mmoja lakini hakuna mtu anayetakiwa kulazimishwa kwenye aina
hiyo ya ndoa kabla ya majadiliano.”
May hakuishia hapo,
“Naomba kufikia mwisho wa maonesho juu ya suala hili kwenye mitandao ya
kujamii, ambako watoto wetu wanakua na watakuja kuona haya. Hebu tuwalinde
watoto wetu wapendwa na hizi drama series ambazo zinaweza kuwaathiri moja kwa
moja au kinyume chake.”
Kisha akamalizia kwa
kumuomba Mungu awaongoze katika njia iliyosahihi na kisha kuwatakia watu wote
kheri ya krismas.
Baada ya krismas, Mke wa
kwanza wa Yul Edchie, Bi. May Edochie alichapisha picha mtandaoni ambayo ni
Photoshopped ambayo ilimuonesha mke mkubwa (May), mke mdogo (Judy), watoto wa
mke mkubwa na mtoto wa mke mdogo.
![]() |
PICHA ILIYOCHAPISHWA NA MAY EDOCHIE (KUSHOTO) |
Maisha yakaendelea bila
migogoro, mwezi March 26, mwaka 2023, Yul akatupia ujumbe kwenye Instagram kuwa
ni mwanaume mwenye wake wawili ndiye anajua mke yupi mwenye nafasi kubwa zaidi
moyoni mwake.
PIGO KWA YUL & MAY
EDOCHIE
March 30, mwaka 2023
zikatoka taarifa mbaya zilizowashitua mashabiki na wapenzi wa Yul na May
Edochie kuwa mtoto wake wakiume wa kwanza aitwaye Kambilichukwu Yul Edochie!
Taarifa kutoka kwa dada wa May zilinukuliwa na mtandao wa Vanguard kuwa, Kambi
alidondoka ghafla alipokuwa akicheza na wenzake. Alikimbizwa haraka hospitalini
lakini baadae taarifa zilitoka kuwa amefariki!
![]() |
KAMBILICHUKWU AKIWA NA BABA YAKE, YUL EDOCHIE |
Kama kawaida wananzengo hawakutaka jambo hili lipite hivi hivi, wakamtupia shutuma Judy Austin Yul Edochie ambaye ni mke wa pili wa Yul Edochie, kuhusika moja kwa moja na kifo cha mtoto wake wa kambo. Tomi_b123 aliandika, hongeza sana…Umefanikiwa.
Mj_luxury_hairs
akaandika, Umefanikiwa kumuua kijana nwa watu, Mungu atakuhukumu.
Unique_temmie akaandika,
Umechukua mume wa mtu, umetumia pesa na jamaa na kumuacha (Mr. Obasi) na haya
ndiyo matokeo yake…Naomba mashemeji wa mtandaoni wasije kukutafuna mbichi.
Si wote walikuwa na
mawazo yanayofanana, wapo baadhi walikuwa na utofauti wa mawazo kama
Patucheagwu ambaye aliandika, Baadhi yenu mnatakiwa kuomba msamaha kwa wazazi
wenu kwa kupoteza pesa kuwapeleka shule. Tazama ushetani na maoni ya kishetani.
March 31, mwaka 2023 Yul
alienda kutoa taarifa katika kituo cha polisi kuhusiana na kifo cha mwanaye.
Kambi (16) alifariki siku ya Alhamisi ya tarehe 30 mwezi March 30 mwaka 2023.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya umma ya jeshi la polisi jimbo la Lagos, SP
Benjamin Hundeyin alithibitisha kutokea kwa kifo cha Kambilichukwu Yul Edochie.
SP Hundeyin alisema kifo cha kijana huyo kilitokea shuleni baada ya kudondoka
ghafla na kukimbizwa katika Hospitali ya Mama na Mtoto iliyo katika Jimbo la
Lagos.
Kwa mujibu wa Polisi,
jambo hilo lilikabidhiwa kwenye Idara ya Polisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai
ya jimbo hilo.
Tangu kutokea kwa kifo
hicho, Yul na mkewe, May walikuwa watulivu sana hasa katika mitandao ya
kijamii. Lakini ukimya huo haukudumu sana kwani Tarehe 10 mwezi April, mwaka
2023, Yul alifuta picha zote za mkewe wa pili na mtoto wao kwa mke wa pili,
Judy. Pia alifuta picha aliyoichapisha mwezi April 2022 kuwa ameongeza mke wa
pili. Haikufahamika wazi kwanini Yul aliamua kufuta picha hizo za mkewe wa pili
na mtoto wao.
Siku 5 baada ya Yul
kufuta picha za mkewe wa pili au mke mdogo na mtoto wao, mwandishi wa habari za
kiuchunguzi, Kemi Olunloyo alichapisha habari mtandaoni ikisomeka, “I just heard that, DNA test revealed that
Judy Austin’s son was not fathered by Yul Edochie” Kwa tafsiri isiyo rasmi,
“Nimesikia kuwa, vipimo vya DNA vimethibitisha kuwa mtoto wa Judy Austin, baba
yake siyo Yul Edochie.” Wananzengo wakaanza kuunganisha doti na kupata mstari
ulionyooka kuwa kitendo cha Yul kufuta picha za mke mdogo na mtoto wao ni
kwasababu aligundua kuwa mtoto si wa kwake! Mashabiki wengi wa Yul walionekana
kufurahishwa na jambo hilo na kumshauri atulie na mkewe mkubwa na walee watoto
wao.
Siku ya juzi usiku April
27 mwaka 2023, Yul Edochie alivunja kimya kirefu na kuweka ujumbe wa majonzi
akiomboleza kifo cha kijana wake. Aliandika, “Siku ya Jumatano asubuhi, ulikuja
chumbani kwangu ukiwa umevaa tayari kwa kwenda shule. Ukaniambia kuwa siku ya
Ijumaa kutakuwa na michezo ya Inter-House, na nikakuahidi nitakuwepo. Ukafurahi
sana. Ukaniambia umeshinda medali ya dhahabu kwenye mchezo wa kuogelea.”
“Nikakupongeza.
Nikakutania kuhusu kimo chako, kisha ukaondoka kwenda shule ukiwa mwenyefuraha
kuliko siku zote. Na hukurudi tena. Siwezi kumlaumu Mungu. Kijana wangu mpendwa,
yaani tumekuwa pamoja kwa miaka 16 tu hapa duniani, lakini umeacha alama yako.
Kijana bora. Mtulivu, mzuri, mwenye akili, muda wote mchangamfu, mchezaji mzuri
wa mpira, mtanashati, na mwenye roho ya upendo.” Huu ulikuwa ujumbe
uliowaumioza wengi hasa wale waliokuwa wakifuatilia maisha ya nguli huyu wa
filamu.
Nihitimishe kwa kusema,
Dunia inazunguka kwenye mhimili wake, kukiwa asubuhi, kukiwa mchana, kukiwa
usiku, tambua mambo mengi yanatendeka katika ulimwengu huu. Mambo haya yote
yana TAMU na CHUNGU. Kuna mafunzo, kuna maonyo ni kazi kwako kuchagua
kikufaacho kukifuata katika kila tukio linalotokea katika ulimwengu huu.
Imeandikwa na Geofrey
Dismas
0 Comments