MTUNZI: BEN R. MTOBWA
Siku chache baadae maongezi yalibadilika.
"Umesikia? Makaburu wanadai kuwa wataendelea kuwaadhibu viongozi na wananchi wote wa nchi za mstari wa mbele ambao wanajifanya vichwa ngumu."
"Kweli? Washenzi sana wale. Wanaweza kufanya lolote".
Na baada ya siku chache mambo yalianza kutukia. Duniani kote magazeti yalikuwa na habari ya kutisha:
Watu mia nne wamefariki, mia tisa kujeruhiwa na maelfu kuponea chupuchupu katika ajali isiyo ya kawaida iliyotokea huko Lagos Naijeria. Watu hao walikuwa katika uwanja wa mpira wakitazama shindano kati ya timu ya taifa ya nchi hiyo na Zaire. Dakika chache kabla ya mchezo huo kwisha, moto mkali ulilipuka na kuubomoa uwanja mzima na kusababisha maafa hayo. Wachunguzi wa mambo wanahisi kuwa huenda utawala wa Afrika Kusini unahusika.
Kabla watu hawajaisahau habari hiyo, ilifuata nyingine ya kutisha vilevile.
SASA SONGA NAYO........................
Harare.
Maghala manane ya serikali, ambayo yalikuwa yamehifadhi chakula, yameungua moto kwa pamoja. Chanzo cha moto huo hakijajulikana. Jambo la kushangaza ni jinsi maghala hayo yalivyoungua kwa pamoja ingawa yako katika wilaya mbalimbali za nchi hiyo. Kuna mashaka kuwa tukio hili kwa njia moja au nyingine linahusiana na yale maafa ya Nigeria.
Na baada ya siku chache; Dar es Salaam.
Katika matukio ya kutisha na kushangaza yanayozidi kutokea nchi zenye msimamo wa kimapinduzi za Afrika, leo asubuhi Tanzania imepatwa na pigo zito la kusikitisha. Jengo la Benki kuu ambalo lilikuwa likikamilisha marekebisho, baada ya ule moto wa awali limeungua tena. Safari hii haielekei kuwa kuna matengenezo yoyote yanayoweza kulirekebisha zaidi ya kujengwa upya. Chanzo cha moto huu hakijafahamika.
Habari hizi ziliitisha Afrika na kuishangaza dunia. Kila mtu aliyezisikia redioni na kuzisoma magazetini alishangazwa na matukio haya ambayo mfano wake haukupata kutokea katika historia ya Afrika na dunia.
Ajali ni jambo la kawaida. Kadhalika, kuna watu wanaoamini kitu kinachoitwa ‘mkosi’ na ‘bahati mbaya.’Lakini mikosi mingi kiasi hiki na bahati mbaya kama hizi kuziandama nchi chache za Afrika, zenye msimamo mmoja katika suala la ukombozi, ni jambo ambalo lilisababisha nyongeza katika fikra za wasomaji na wasikilizaji wa vyombo vya habari. Kitu kinachoitwa ‘roho mbaya’ kilipenya katika fikra hizo, ingawa hakukuwa na hakika katika mawazo hayo. Baadhi hata waliwahi kutamka hadharani kuwa kuna mkono wa mtu katika matukio hayo.
Mawazo hayo yalifuatwa na hofu katika mioyo ya wananchi na serikali zao walipojiuliza, “Kipi kingefuata?”
"Joram, tutakaa kimya kusubiri maafa zaidi?" Nuru alimwuliza Joram baada ya kusoma habari hizi za tukio la Benki Kuu katika gazeti. Alijitahidi kustahamili kutosema lolote alipoyasoma matukio ya Lagos na Harare. Lakini hili la nyumbani lilimgusa zaidi. "Aibu iliyoje!" aliendelea. “Tuendelee kustarehe kwa vinywaji na muziki huku tukisubiri siku ambayo maafa mengine yatatokea! Haiwezekani Joram. Lazima tufanye jambo."
Ndiyo. Habari hizo hazikumpendeza Joram. Hata hivyo, alizisoma kama raia wengine, bila ya kudhihirisha dalili yoyote ya nia ya kufanya lolote kama alivyokuwa awali. Jambo hilo lilimfanya Nuru atokwe na machozi. "Serikali inao polisi na wapelelezi wake, ambao inawalipa pesa nyingi," Joram alisema. "Mimi ambaye nimeacha shughuli hizo nitasaidia nini?"
"Huwezi kusema hivyo Joram! Siamini kama moyo wako wa uzalendo umedidimia kiasi hicho."
"Haujadidimia. Uko palepale, kama ilivyo mioyo ya wazalendo wengine."
"Lakini wewe si mzalendo wa kawaida, Joram. Taifa linakuthamini na kukutegemea. Huwezi kulisaliti kiasi hicho bila sababu ya kuridhisha. Lazima ufanye jambo.”
"Ndiyo. Nitafanya jambo. Nitastarehe na kuendelea kustarehe kama wanavyofanya vijana wenzangu. Njoo kitandani, Nuru. Tafadhali, njoo tustarehe. Acha wenye shibe waendelee kulinda shibe yao. Wewe na mimi tuna nini katika nchi na dunia hii?"
"Joram..."
"Nuru, njoo tafadhali. Na kama umenichoka sema nimtafute Nuru mwingine ambaye hachoshwi na starehe.” Nuru angependa kukataa. Lakini asingeweza. Akamfuata Joram kitandani na kujilaza kando yake huku machozi yakimtoka kama kondoo anayesubiri kuchunwa.
*****
KATI ya watu ambao wameisumbukia nchi hii, wakiziweka roho zao katika minada ya maafa na kwato za mauti kuilinda nchi isimezwe na jangwa la misukosuko inayosababishwa na majasusi hatari, ni mzee huyu; Mkwaju Kombora. Tangu utoto wake baada ya kumaliza kidato cha sita, alijikuta akitoka chuo hadi chuo, akifundishwa mbinu mbalimbali za kupambana na adui. Baada ya kuhitimu vizuri alijikuta kava magwanda ambayo mabega yake hayakukoma kubadilikabadilika hadi alipojikuta Inspekta wa kikosi hiki maalumu. Kupanda kwake ngazi mara kwa mara kulitokana na moyo wake wa kishujaa na juhudi zisizo kifani katika kuwakabili adui wa nchi. Mara kwa mara aliwashinda adui zake isipokuwa safari chache ambazo alielekea kukata tamaa. Hata hivyo, asingekosa kumshukuru Mungu kwani nyakati hizo alitokea kijana yule ambaye alisaidia kuwanasa adui kwa hila zake za kutatanisha, kijana ambae jina lake lisingeweza kumtoka akilini; Joram Kiango.
Kombora asingeusahau mchango wa kijana huyu katika mikasa ile ambayo Mswahili mmoja ameamua kuandika vitabu ili apate chochote kile na kuviita Dimbwi la Damu, Mikononi mwa Nunda, Najisikia kuua tena na Salamu kutoka Kuzimu. Hata hivyo, kama polisi wengine, Kombora asingeweza kutamka hadharani kuwa Joram alifanya lolote la haja isipokuwa alibahatisha na kuhatarisha maisha yake.
Lakini leo Kombora alitamani kumbembeleza Joram, hata kwa kumuangukia miguuni, endapo ingebidi, ili amsaidie kuutatua mkasa huu uliokuwa ukimtoa jasho yeye na polisi wenzake wote wa nchi zilizo mstari wa mbele kwenye ukombozi Kusini mwa Afrika.
Mambo mengi, yalikuwa yakitokea mazito na ya kutisha zaidi ya walivyoyafahamu wananchi wa kawaida ambao wanategemea gazeti, redio na televisheni ziwape habari. Kila mmoja alisikia mikasa ya kuteketea kwa mamia ya maisha ya watu wasio na hatia ambao walipata ajali ya kutatanisha katika uwanja wa mpira huko Naijeria. Pia, ni wengi waliosikia juu ya kuungua kwa maghala ya chakula bila sababu mahususi inayoeleweka huko Harare. Zaidi, hakuna Mtanzania ambaye hakupata kuzisikia habari za kuungua tena kwa jengo la Benki kuu lililokuwa likikamilishiwa shughuli za kujengwa upya.
Hayo ni maovu yaliyosikika katika vyombo vya habari na mitaani. Hayakumtisha sana Kombora. Lakini kulikuwa na haya ambayo bado yalikuwa siri mioyoni mwa wakubwa wachache wa ngazi za juu katika idara ya usalama, ambayo hayasemeki wala kutangazika.
Viongozi wanane wa vyama kadhaa vya wapigania uhuru wa Afrika Kusini na mwakilishi wa PLO hapa nchini, ambao walikuwa wakikutana kwa faragha katika jengo moja jijini Dar es Salaam, walifariki ghafla katika moja ya ajali hizo zisizoeleweka. Hakuna anayefahamu kikamilifu chanzo cha vifo hivyo, isipokuwa kwamba walikufa kwa kuungua moto uliolipuka ghafla katika chumba chao cha mkutano. Juhudi zote za kutafuta chanzo cha moto huo hazikuwa na mafanikio.
Zaidi ya hao, kuna wale mawaziri wa nchi zisizofungamana na upande wowote ambao walinusurika katika ajali ambayo haikutofautiana na hiyo ya Dar es Salaam. Mkutano wao uliandaliwa kufanyika katika chumba fulani katikati ya jiji la Lusaka. Wakati wakijiandaa kwenda huko lilitukia suala jipya ambalo liliuchelewesha msafara wao kwa zaidi ya nusu saa. Kuchelewa huko kuliyaokoa maisha yao kwani chumba hicho kililipuka kwa moto mkubwa uliyoyapoteza maisha ya wafanyakazi wawili wa chumba hicho na kuharibu vifaa vyote. Kama awali, chanzo cha moto huo hakikupata kufahamika.
Hayo ni baadhi tu ya mambo yaliyokuwa yakitokea. Kulikuwa na hisia kuwa mkono wa utawala wamakaburu wa Afrika Kusini ulikuwamo katika vitendo hivyo. Lakini hisia hizo hazikuwa na uhakika kamili, hasa baada ya ushahidi mdogo ulikuwa ukielekea kutoweka kwa njia nyingine ya kusikitisha.
Ushahidi huo ulielekea kuchipuka baada ya ule moto ulioteketeza Benki Kuu. Yuko askari mmoja aliyesema kuwa aliamini moto huo ulisababishwa na mtu mmoja aliyefika katika jengo hili usiku na kujiita kuwa ni mmoja kati ya mafundi ambao walikuwa wakishughulikia jengo hilo. Jengo lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa askari huyo na alimwamuru kusimama mikono juu. Mtu huyo alisihi kwa maneno mengi kuwa, alisahau kitu muhimu sana kwake katika jengo hilo, jambo lililomfanya askari huyo amruhusu kuingia ndani baada ya kumkagua kwa makini. Mtu huyo aliingia harakaharaka na baada ya dakika kadhaa alirudi huku akiwa ameshika hirizi mkononi na kusema kwa furaha,"Nilikuwa nimesahau hii, ndugu yangu. Bila ya kuwa na hii mfukoni siwezi kuishi saa ishirini na nne."
Askari huyo hakumwamini sana mtu huyo, kutokana na jinsi alivyomuona mkakamavu asiyehofu hata kuelekezwa mtutu wa bunduki. Hivyo, jengo hilo lilipolipuka moto saa kadhaa baadaye, alilielezea tukio hilo kwa wakubwa zake ambao walimweka kati ya watu ambao walilazimika kuongea na Kombora ana kwa ana.
Baada ya kumsaili kwa mapana na marefu Kombora alielekea kuamini kuwa mtu huyo aliyeingia katika jengo hilo usiku alihusika, kwa njia moja au nyingine, katika janga hilo. Lakini pindi walipobuni mbinu za kuanzisha msako wakumtafuta, askari huyo aliyekuwa mtu pekee aliyewahi kumwona alikutwa akielea baharini pwani ya Magogoni, akiwa maiti. Hakuna aliyeweza kueleza kilichomtoa kwake Magomeni Mikumi na kuja kuogelea kwa mara ya mwisho Magogoni.
Ilikuwa dhahiri kuwa aliuawa.
Jambo hilo lilimfanya Inspekta Kombora na wenzake wazidi kuamini kwamba kulikuwa na namna katika ajali hizo zilizotokea katika miji mbalimbali ya Afrika huru. Juhudi zao za kutafuta chanzo na watendaji wa maafa hayo hazikuelekea kuzaa matunda yoyote zaidi ya hisia tu kwamba Afrika Kusini ilihusika. Hisia hizo ziliongezewa uzito na vitisho vilivyoletwa kwa njia mbalimbali zikitishia uhai wa maisha ya watu na nchi ambazo eti zingeendelea na msimamo wao wa kuibana Afrika Kusini. Licha ya kusababisha hofu na mashaka, vitendo hivyo, vingeweza kupunguza hamasa ya moyo wa kimapinduzi katika fikra za mashujaa endapo hisia hizo zingeachiwa kuendelea. Ni hapo ndipo Kombora alipozikumbuka silaha zote na kutamani zielekezwe Afrika Kusini. Ni hapo pia alipowakumbuka mashujaa wote na kutamani waelekee Afrika Kusini. Na kati ya mashujaa hao jina la Joram Kiango lilitangulia kumjia akilini.
Hiyo ilikuwa baada ya kuwasiliana na wakuu wote wa vikosi maalumu vya upelelezi katika nchi zote zilizokwisha husishwa na maafa hayo ya kutatanisha. Walishauriana kuwa kila nchi ifanye juu chini kuhakikisha kisa cha maafa hayo kinafahamika na, ikiwezekana, maafa hayo yakomeshwe. Ndipo Kombora alipoanza kufanya kila juhudi. Tumaini pekee ambalo lilielekea kumpatia walao fununu, yaani yule askari mlinzi wa benki kuu, sasa lilikuwa limeuawa kwa hila. Harakati za kupeleleza nani alihusika katika kumuua hazikuzaa matunda yoyote. Hivyo, Kombora alijikuta hajapiga hatua yoyote katika jukumu hilo. Badala yake alijiona kama kiwete au mtu aliyepooza, ambaye anasubiri maafa ya moto unaomjia kasi.
"Joram lazima ashirikishwe," Kombora alifoka kimoyomoyo.
Alikuwa na habari zote za Joram, kuwa tangu baada ya mkasa wa Salamu Toka Kuzimu aliiacha ofisi yake na kuanza maisha ya kipuuzi katika mahoteli na mabaa, akijistarehesha na yule msichana mzuri wa Arusha. "Yeye si mtu wa kuupoteza muda wake katika mabaa. Kipaji chake kinahitajika sana katika vita hivi. Lazima apatikane."
Alimtuma mtu ambaye alizunguka katika hoteli kubwakubwa na kumpata Joram. Lakini, kama Kombora alivyotegemea, majibu ya Joram yalikuwa ya kijeuri kiasi kwamba mtu huyo alijiona mjinga na kurudi akiwa amechukia, jambo ambalo jioni hii lilimfanya Inspekta Kombora ayavue magwanda yake na kuvaa mavazi ya kawaida, kisha akajitoma katika ukumbi wa hoteli ya Embassy ambamo aliambiwa kuwa Joram alikuwamo.
***
Akiwa mtu ambaye halewi kwa urahisi, tunaweza kusema kuwa Joram alikuwa amechangamka pale Kombora alipoikaribia meza yake na kuomba kuketi.
"Karibu sana Inspekta, karibu uketi," alisema kwa uchangamfu huku akimwita mhudumu wa hoteli hiyo. "Leo naweza kusema kuwa ni siku tukufu sana kwangu kutembelewa na Inspekta Mkuu. Habari za siku nyingi mzee?"
"Polepole kijana," Kombora alisema. "Wanasema siku hizi hata kuta zina masikio".
"Kwani kuna lolote la siri tunaloongea mzee? Siku hizi mambo yote ya siri nimeachana nayo. Nimeamua kuwaraia mwema na mtulivu kama ulivyokuwa ukinitaka niwe," Lilikuwa jibu la Joram.
Kombora hakutia neno. Akamgeukia Nuru na kumsalimu, "Bila shaka huyu ndiye yule dada ambaye alikuwa na balaa la kulazimishwa kushirikiana na yule mwuaji aliyekusudia kuwaangamiza viongozi wengi wasio na hatia?" Joram na Nuru waliitika kwa vichwa. "Ni msichana shujaa sana. Msichana wa kawaida angeweza kupoteza kichwa chake mara baada ya kukabiliwa na mkasa mkubwa kama ule," alimaliza akipokea kinywaji chake na kuanza kunywa. "Sivyo mzee," Nuru alijibu. "Kila nikifikiria kile kitendo naona aibu kubwa sana. Nisingestahili kukubali kulazimishwa kushiriki katika mauaji ambayo yangekuwa ya kinyama kama yale. Ingawa yule jasusi Proper alilaghai kuwa ungekuwa mzaha wa kawaida, lakini bado sikustahili kuafikiana naye. Uzalendo wangu ulitiwa dosari na kitendo kile. Najaribu kutafuta nafasi ya kuudhihirishia moyo wangu, lakini sijafanikiwa..."
"Joram ananinyima nafasi hiyo!" Nuru aliongeza baada ya kusita kidogo.
"Ni hilo tu ulilotaka kusema Nuru," Joram alidakia. "Na hata Inspekta nadhani amefuata kujadili hilo. Sivyo mzee?"
Inspekta aliimeza bia iliyokuwa kinywani mwake. Kisha akajibu, "Kiasi ni kweli kuwa niko hapa kujadili hilo, kiasi siyo kweli." Alisita kidogo na kuendelea,"Unajua hatujaonana kwa muda mrefu? Tangu ulipoondoka Arusha kwa hasira baada ya kuitupa bastola yako hatujaonana. Nilifika katika chumba cha dada huyu nusu saa baadaye na kuukuta ubongo ule na bastola. Nilidhani umemwua wewe. Lakini bastola yako haikuwa imefyatuliwa hata risasi moja. Mara kikatokea kile kitabu ambacho kilinifanya nielewe yote yaliyotokea. Ndipo nikaelewa kwanini umekasirika na kuamua kuwa mnywaji".
"Niite mlevi, Inspekta, sijali."
"Hapana. Wewe si mlevi na wala huwezi kuwa mlevi. Ni mnywaji tu, mnywaji ambaye hanywi kwa ajili ya kupenda kunywa, isipokuwa kwa ajili ya hasira baada ya kunyang'anywa fursa ya kuitia risasi kwa mkono wako katika kichwa cha yule mshenzi. Sivyo Joram!" Kombora alitulia akimtazama Joram. Mara akakumbuka kuwa alikuwa hajavuta sigara kwa muda mrefu. Akatoa moja na kuiwasha baada ya kuwataka radhi jirani zake.
"Kuacha hadhi yako ipotee kwa ajili ya kukosa nafasi ya kumwua mtu mmoja tu duniani!" Kombora aliendelea, "Sioni kama ni haki. Ziko nafasi nyingi za kufumua vichwa vya watu wenye haki kabisa ya kufumuliwa. Hati maalumu inatayarishwa ambayo itakuruhusu kufanya lolote kama afisa yeyote wa usalama mwenye jukumu maalumu. Zaidi kimetengwa kifungu maalumu cha fedha ambacho kitaingizwa katika akaunti yako ili pesa zisiwe kipingamizi..."
"Taratibu Inspekta," Joram alimkatiza. "Vipi? Mbona mnanitendea mema mengi hivyo? Kama sikosei unachotaka kusema ni kwamba unaniomba nishiriki katika kutafuta kiini cha maafa haya yanayotendeka katika nchi za mstari wa mbele. Na kama sikosei mtu uliyemtuma kwangu amekupa majibu yangu rasmi, msimamo wangu ni uleule. Na utaendelea kuwa uleule. Kama mlimfahamu Joram ambaye alikuwa mpenzi wa Tanzania na Afrikakwa ujumla, lazima muelewe kuwa Joram huyo amekufa. Aliye hai, mbele yako, ni Joram mpya, Joram ambaye wala hana kiu ya kushiriki kwa njia moja au nyingine katika masuala yoyote ya nchi. Aliyeko mbele yako ni Joram wa mastarehe, Joram wa kutumia. Hata dada yangu Nuru hapa nadhani anaelewa."
Ndipo Kombora alipoona ugumu wa kazi iliyokuwa mbele yake. Kumshawishi Joram ilikuwa sawa na kulilazimisha jabali lielee juu ya maji. Akiwa mtu ambaye hakuzowea kuwabembeleza binadamu wengine, hasa wanaume, Kombora alisema kwa sauti iliyoficha hasira na unyonge, "Pengine unajua unachokifanya. Lakini nadhani hujui kiwango gani cha madhara yanayolikaribia taifa hili endapo tutashindwa kuukomesha uovu huu unaonyemelea. Niruhusu nikusimulie mambo ya kutisha ambayo hayajavifikia vyombo vya habari. "Haitasaidia," Joram alimjibu. "Utaupoteza bure muda wako. Ninachohitaji kusikia ni habari za burudani tu. Kama kuna burudani mpya ambayo sijaiona, kinywaji kipya ambacho sijakinywa au muziki mpya ambao sijausikia, nitafurahia endapo utanisimulia. Juu ya vifo vya marais na raia wenye hatia na wasio na hatia, si kazi yangu tena."
"Hata hivyo, sauti yako haifanani kabisa na madai yako Joram. Kuna watu ambao silika yao ni kukesha katika mabaa na madansi, wewe si mmoja wao. Kuna wanaostarehe kusubiri maafa ya kusikitisha, wewe si mmoja wao, Joram. Kuna wanaofurahia ladha ya pombe na utamu wa muziki zaidi ya kazi na ushujaa, wewe si mmoja wao vilevile."
"Zamani, Inspekta. Sasa hivi mimi ni mmoja wao na nitaendelea kuwa mmoja wao. Na kama huna maongezi mengine zaidi ya haya mzee nitashindwa kuendelea kukusikiliza," Joram alimaliza akitoa sigara yake na kuiwasha.
Kombora hakujua afanye nini ili amshawishi Joram. Alimtazama Nuru kama aliyehitaji msaada wake. Akayaona macho yake mazuri yaliyojaa huzuni katika hali ya kukata tamaa. Hilo, kiasi lilimfariji Kombora. Alifahamu kuwa anaye msaidizi ambaye angesaidia katika juhudi zake za kumrejesha Joram Kiango katika dunia ya Joram Kiango. Akiwa si mgeni katika dunia hii Kombora alielewa kuwa mwanamke mzuri ni silaha. Hivyo, akamtupia Nuru jicho la kumtaka aelewe kuwa anautegemea msaada wake. Kisha akainuka na kuaga bila ya kumaliza kinywaji chake.
ITAENDELEA.............
--------------




0 Comments